2017-09-16 14:56:00

Vita na machafuko ya kisiasa DRC ni chanzo cha uhaba wa chakula!


Vita ambayo imedumu kwa muda mrefu sasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, machafuko ya kisiasa; wimbi kubwa la watu wasiokuwa na makazi ya kudumu, sasa kuna hatari kubwa ya watu zaidi ya milioni 7.7 kukumbwa na baa la njaa ambalo limeongezeka kwa asilimia 30% ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kwa mwaka 2016. Taarifa mpya ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO pamoja na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP inaonesha kwamba idadi ya watu wanaohitaji msaada wa chakula cha dharura imeongezeka kutoka milioni 5. 9 hadi kufikia milioni 7.7 kwa wakati huu na kwamba, waathirika wakuu ni wananchi wanaoishi katika mikoa ya Kasai na Tanganyika ambako machafuko na ghasia yamekuwa ni chakula chao cha kila siku, kiasi hata cha kushindwa kufanya kazi mashambani.

Hali hii inachangiwa pia na milipuko ya magonjwa ambayo imesababisha watu wengi kupoteza maisha yao. Wakulima wanashindwa kwenda mashambini kwa zaidi ya misimu miwili na soko la ndani limeshindwa pia kukidhi mahitaji ya wananchi hawa. Bwana Alexis Bonte, Mwakilishi mkazi wa FAO nchini DRC., anakaza kusema, ikiwa kama chakula cha dharura hakitawasili mapema iwezekanavyo, watu wengi watakufa kwa baa la njaa nchini DRC. Lakini, amani na utulivu ndio kiu kubwa ya wananchi wa DRC, ili kuwajengea mazingira yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika kazi za kilimo, uzalishaji na huduma. Wanahitaji pembejeo za kutosha na kwamba, sehemu kumbwa ya wananchi wa maeneo haya ni wajane, kwani waume zao wengi wameuwawa wakati wa machafuko, ghasia na vita inayoendelea nchini DRC.

Kumbe hata hapa kuna changamoto kubwa ya kuweza kuzitegemeza familia katika mahitaji msingi. Kilimo kwa kwa wanawake hawa, ni sehemu ya mchakato wa kuwajengea uwezo wa kupambana na hali ngumu ya maisha, kwa kuzingatia utu na heshima yao, daima wakiwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 50% hadi 80% ya wananchi walioathirika kwa baa la njaa wanashindia mlo mmoja. Kuna zaidi ya watu wasiokuwa na makazi maalum nchini DRC wanaofikia milioni 3.7 na kwamba, sehemu kubwa ya nchi imekumbwa na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula.

Hali hii inagumishwa zaidi na mapigano yanayoendelea huko Kasai, mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kusaidia mchakato wa amani nchini DRC. Ni matumaini ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO pamoja na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itasaidia kuchangia kwa ajili ya kugharimia chakula cha dharura kwa wananchi wa DRC pamoja na kusitisha vita na ghasia ili wananchi waweze kurejea tena katika shughuli zao za kila siku.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.