2017-09-15 13:30:00

Papa Francisko amefanya uteuzi kwa nafasi mbali mbali mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Matteo Visioli, kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Padre Visioli alizaliwa tarehe 20 Julai 1966 huko Parma, Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi akapewa Daraja Takatifu ya Upadre 9 Mei 1992. Baadaye akajiendeleza na masomo ya juu Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian katika masomo ya: Taalimungu, Sheria za Kanisa na Sheria za Kiraia na hatimaye, kunako mwaka 1999 akatunukiwa Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa.

Tangu wakati huo ametekeleza dhamana na wajibu wake Jimboni mwake na katika ngazi ya kitaifa. Hadi uteuzi wake ni Rais wa “Caritas Children Onlus” yaani “Chama cha Msaada kwa watoto”. Ni Jaalimu wa Sheria za Kanisa Chuo kikuu cha Kipapa cha Gregorian, Marcianum, huko Venezia na mwandishi maarufu katika medani za Sheria za Kanisa.

Baba Mtakatifu amemteua Mheshimiwa Padre Andrea Ripa kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri. Padre Ripa alizaliwa kunako tarehe 5 Januari 1972. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapdrishwa kunako mwaka 2004. Alibahatika kupata Shahada ya Uzamifu kuhusu Fasihi Andishi na Sheria za Kanisa. Ni mwandishi mahiri wa vitabu na majarida ya kisayansi. Ni wakili pia wa kujitegemea na katika maisha yake amebahatika kuwatumikia watu wa Mungu, Jimbo Katoliki la Rimini kama Paroko, Jaalimu wa Injili ya ndoa na familia, Sayansi ya dini na taalimungu kwenye Chuo Kikuu cha Lugano pamoja na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano. Tangu mwaka 2013 amekua akifanya utume wake katika Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amemtea Padre Angelo Accattino kuwa Balozi wa Vatican nchini Bolivia na kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu mkuu. Padre Accattino alizaliwa tarehe 31 Julai 1966, Jimboni Casale Monferrato. Alipadrishwa kunako tarehe 25 Juni 1994. Ana Shahada ya uzamivu katika Sheria za Kanisa. Alianza utume wake katika masuala ya diplomasia ya Vatican, tarehe 1 Julai 1999. Tangu wakati huo ametekeleza dhamana na utume wake huko Trinidad na Tobago, Colombia, Perù, Vatican na hatimaye, Marekani na Uturuki.

Baba Mtakatifu Francisko ametemua Askofu mkuu Emil Paul Tscherrig, kuwa Balozi wa Vatican nchini Italia. Kabla ya uteuzi huu, alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Argentina. Na habari zaidi zinasema, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Gabriele Giordano Caccia kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Ufilippini. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Caccia alikuwa Balozi wa Vatican nchini Lebanon.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.