2017-09-15 12:06:00

Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni chombo cha uinjilishaji Afrika


Ujenzi na uimarishaji wa Jumuiya ndogo ndogo za kikristo ni changamoto ya kichungaji iliyovaliwa njuga na Mababa wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki, AMECEA na Kati tangu mwaka 1973 na kupewa kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kunako mwaka 1974. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni sehemu muhimu sana ya Kanisa Mahalia; mahali ambapo Wakristo wanasali, wanasikiliza na kutafakari Neno la Mungu; wanashiriki adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu wanalolimwilisha katika: imani, matumaini na mapendo yaani ”Koinonia”. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni mahali pa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma”. Hapa ni mahali ambapo imani ya Kikristo inamwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji yaani “Diakonia”.

Lengo kuu ni kuwawesha Wakristo kuwa kweli ni mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake sehemu mbali mbali za Bara la Afrika. Kimsingi, Jumuiya ndogo za Kikristo ni chombo makini cha uinjilishaji, zinazosaidia kujenga na kuimarisha ujirani mwema, udugu na upendo wa Kikristo. Ni mhimili wa maisha na utume wa Kikristo katika kujenga imani, maadili na utu wema. Ni sehemu ya muundo wa Kanisa Mahalia Barani Afrika, katika maisha na utume wake. Ni mahali pia pa kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo zinakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika.

Hivi karibuni, Mtandao wa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo Barani Afrika umehitimisha Kongamano la Nne la Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo lililofanyika huko Kinshasa, DRC. Kongamano liliandaliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM na kuwashirikisha pia wadau wa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo kutoka nje ya Afrika. Kongamano hili lilikuwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa kongamano la Jumuiya ndogo ndogo lililofanyika Nairobi, kunako mwaka 2016, baada ya lile la Ouagadougou la mwaka 2015 na Accra, Ghana mwaka 2014. Kongamano lilipania kujenga jukwaa la kushirikishana uzoefu, mang’amuzi na rasimali watu na fedha; kupembua na kuona ufanisi katika utumiaji wa mitandao ya kijamii katika kukuza na kudumisha Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo.

Kuimarisha umoja na mshikamano wa familia ya Mungu Barani Afrika kwa njia ya Jumuiya ndogo ndogo hata ughaibuni. Imekuwa ni nafasi ya kupembua kwa kina ili kuangalia iwezekano wa kushirikisha Jumuiya ndogo za Kikristo katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa Mahalia! Wajumbe wamekiri kuhusu umuhimu wa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo kwani zinawajengea waamini uwezo wa kushuhudia, kutangaza, kuhudumia na kushikamana na watu mbali mbali, kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na changamoto za uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na Mababa wa Kanisa Barani Afrika, kuna haja kwa Kanisa la Afrika kuwekeza zaidi katika majiundo makini ya awali na endelevu ya Jumuiya ndogo ndogo; kukusanya na kuhifadhi kumbu kumbu na takwimu za Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo na kwamba, hii inapaswa kuwa ni sehemu muhimu sana ya majiundo ya majandokasisi katika seminari na nyumba za malezi Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.