2017-09-14 11:19:00

Iweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni!


Tukisoma Injili ya Mt. 18:21 – kuhusu kusameheana tunasikia – kisha Petro akamwendea, akasema, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Mtume Petro hakusema aliyenikosea aniombe msamaha mara ngapi. Ndugu zangu, katika injili tunasikia habari ya mtumishi anayesamehewa lakini yeye anashindwa kusamehe. Bado injili ya jumapili iliyopita inatuwajibisha hapa – kusahihishana makosa. Tuliona kuwa wajibu mkubwa wa kikristo ni kusameheana makosa na kuwa tayari kutafutana ili kuondoa wingu kati yetu. Sisi wakristo hatuna budi kusameheana kati yetu. Katika barua ya Mtume Paulo kwa Rum. 5:7 tunasoma hivi – bali Mungu aonesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Swali la Petro kwa Yesu nisamehe mara ngapi linajibiwa na Yesu akisema kuwa kusamehe ni tendo endelevu na msamaha wa Mungu unatuwajibisha sana. Ni lazima kusamehe vinginevyo itakuwa shida. Katika Mt. 18:35 tunasoma hivi; ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake. Ili usamehewe huna budi kusamehe. Katika Zab. 103:1-3,9-12 tunasoma neno hili – Bwana amejaa huruma na neema, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa fadhili.

Pengine swali linafuata ni hili… namna gani nisamehe? Tuangalie ushuhuda huu. Abraham Lincoln, rais wa 16 wa Marekani anatupata uwezekano wa kuishi msamaha na upatanisho. Wakati akifanya kampeni alitokea mpinzani aliyefanya kila aina ya mbinu ili kuharibu jina na sifa yake. Huyu aliitwa Edwin McMasters Stanton. Alikuwa tayari kufanya lo lote ili Lincoln asipate nafasi ya kushinda uchaguzi wa urais. Hata hivyo Lincoln alishinda na alipokuwa anaandaa baraza la mawari jina la Stanton likawepo. Wasaidizi wa rais walifanya juhudi kubwa ila bila mafanikio kumweleza rais chuki ya Stanton dhidi yake. Rais alionekana kuzijua wazi mbinu mbaya za Stanton dhidi yake wakati wa kampeni. Rais akasema huyu ananichukia mimi ila siyo Marekani. Huyu ana sifa za kuongoza Marekani na  watu wake. Akamfanya waziri wa ulinzi. Stanton aliifanya kazi ile kwa weledi mkubwa. Lincoln aliuawa. Wakati wa maziko yake Stanton alisema; hakika huyu asingeondoa chuki yake dhidi yangu, leo hii angezikwa akiacha adui duniani. Lakini kwa vile roho yake ilikuwa tofauti na yangu ameacha rafiki duniani.

Katika YBS 28:2 tunasoma hivi; umsamehe jirani yako dhara alilokufanyia, hivyo nawe utasemehewa dhambi zako wakati utakaposali. Ndicho tunachotakiwa kufanya leo kwani tusiposamehe nasi pia hatutasamehewa makosa yetu. Ili tendo la msamaha likamilike ni lazima tujifunze jinsi Mungu alivyotusamehe sisi – Lk. 23:34 – Yesu pale msalabani anasema – Baba uwasamehe kwa vile hawajui walitendalo. Hii ndiyo tofauti kubwa kati ya dini yetu na dini nyingine.

Ndugu zangu, kwa kawaida anayetenda kosa ana tabia ya kujificha na anakosa ujasiri wa kuonana na yue aliyemkosea – angalia Mwa. 3:7 – baada ya kula tunda, walijificha, waliondoka bustanini. Kwa upande mwingine tunaona jinsi Mwenyezi Mungu, ingawa alikosewa uaminifu, alivyowatafuta. Bahati nzuri hapa kwamba katika mahojiano yao na Mungu, waliweza kuelezea kosa lao na kukiri kosa lao. Wengi wetu hatuna ujasiri wa kukiri kosa na hata kuwa tayari kuomba msamaha. Hata hivyo wanabeba dhamana ya kosa na anawawajibisha. Swali ambalo twaweza kujiuliza ni hili – wewe umekosa mara ngapi? Umesamehe mara ngapi? Mtume Paulo katika 2Kor. 5:18 anasema, lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho. Huduma ya upatanisho ni lazima kwetu sisi waamini.

Mojawapo ya mambo yamfanyayo mwanadamu kuwa mgumu kutoa msamaha ni kutokutambua nguvu ya msamaha. Na hii inagharimu sana maisha yetu. Dinari 100 kwa wakati ule ilikuwa ni sawa na mshahara wa siku 100 ambayo ingeweza kulipwa katika muda wa miezi michache. Talanta moja kwa wakati ule ilikuwa ni sawa na dinari 6000. Kwa maelezo haya, talanta 10,000 ni sawa ni dinari 60,000,000 alizosamehewa na ingechukuwa miaka 280 kulipa hilo deni kama bwana wake angemdai. Lakini kwa sababu ya ugumu wa moyo na tama ya kulipa kisasi yule mtumwa alisahau msamaha mkubwa aliopewa na kushikilia ubinafsi wake kwa kumdai mjoli wake dinari 100. Namna hii ya kutokuelewa maana ya msamaha ipo pia katika Yoh. 8:7 … juu ya habari ya mwanamke aliyekamatwa katika uzinzi. Baada ya Yesu kuhojiana nao, wote wale walijikuta wadhambi. Na Yesu anamwambia yule mama name sikuhukumu, enenda zako, usitende dhambi tena. 

Ndugu zangu, sisi tunatakiwa kusamehe kama Mungu alivyotusamehe sisi. Yesu alituonea huruma kuu na kwa kifo chake msalabani akatupatanisha nasi. Leo tutasali tena sala ya Baba Yetu. Je, kweli tunasamehe wadeni wetu kama yule mfalme alivyomsamehe yule mtumwa talanta elfu 10 na/au hata baada ya kusamehewa makosa yetu tunabaki na dukuduku kama yule mtumwa mwovu? Kwa kifupi msamaha usipokuwepo, dhambi hutawala na hukumu inatawala. Maisha yetu yana mhimili upi? Kosa-hukumu au kosa-msamaha? Katika somo la kwanza tunasikia habari la tangazo la adhabu ya Mungu. Lakini hii inatokea tu pale mwanadamu alipokataa msamaha wa Mungu.

Kwa mwito wa Mungu leo hii tunayo lazima ya kuuvuka ubinafsi na kuangalia dunia kwa mapana yake. Ni rahisi kuwa wagumu kwa wengine hasa wanapofanya kosa na kujihurumia wenyewe kwa kosa hilo hilo au pengine kubwa zaidi. Tunapendelea nafsi zetu hata katika makosa. Nimekusamehe lakini sitakusahau ni namna nyingine ya kusema sijakusamehe. Namna pekee ya kumaliza ugomvi ni kusamehe na si kinyume chake. Yoshua bin Sira katika somo la kwanza anaweka mbele yetu namna tunavyoweza kuonja nguvu ya msamaha – samehe kosa la jirani yako halafu unaposali dhambi zako zitasamehewa. Ndivyo tunavyodaiwa na injili ya leo. Tutaweza tu kuonja utamu wa msamaha kama tukiwasamehe wenzetu. Hakika yule mtumwa hakuelewa ukubwa wa msamaha aliopewa na hivyo anasahau kusamehe kidogo anachodai. Kwa kosa hilo anaishia kufungwa kifungoni. Na hali hii itatukuta sote siku ya hukumu katika kushindwa kwetu kutambua nguvu ya upendo wa Mungu. Mwandishi mmoja Anon anasema, ingefaa kila mmoja wetu awe na kaburi maalumu la kuzika kasoro zake na ya wenzetu na kuwa na bustani nzuri ya kuhifadhi mazuri yetu na ya wenzetu.

Leo Bwana Yesu atuambia tusameheane makosa yetu na ikiwa kuna deni kati yetu basi liwepo tu deni la upendo, anatukumbusha mtume Paulo. Mtume Paulo katika Kol. 3:12-15 anasema, basi kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwa, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkuchukuliana na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake, kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndicho kifungo cha ukamilifu, na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu, ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja, tena iweni watu wa shukrani. Naye Padre Cantalamessa, mhubiri wa nyumba ya Kipapa anasema, katika kutafuta mapatano tuwe pia tayari kusema nimesamehe, nimekosa na si tu nimekusamehe makosa yako. Hapa tunaweza kuona pia kuwa hata aliyekosa ana kitu cha kusamehe.

Tumsifu Yesu Kristo!

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S








All the contents on this site are copyrighted ©.