2017-09-11 15:46:00

Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuhusu vurugu na mauaji


Baraza la Maaskofu Katoliki katika mkutano wake wa kawaida uliofanyika Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 8-9 Septemba 2017 linapenda kulaani vurugu, mauaji na uvunjifu wa amani ambao umekuwa ukitendeka nchini humo kwa siku za hivi karibuni. Maaskofu wanaungana wapenda amani wote nchini Tanzania kulaani vikali vitendo hivi vinavyohatarisha amani, umoja, mshikamano na mafungamano ya kitaifa.

Katika tamko lililotiwa sahihi na Askofu mkuu Beatus Kinyaiya, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, linasema, Tanzania kwa sasa inashuhudia matendo ya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kama ilivyotokea Mkuranga, Rufiji na Kibiti; utekwaji wa watu na kuteswa; utekaji wa watoto, ulipuaji wa ofisi za watu na hivi karibuni shambulio dhidi ya Mbunge Tunu Lissu. Baraza la Maaskofu Katokliki Tanzania linapenda kutamka wazi na kwa nguvu zote kuwa vurugu na mashambulizi ya aina yoyote ile yanalifedhehesha taifa. Matendo haya ni dhambi, ni uhalifu na si utamaduni wa watanzania. Maaskofu wanaomba yakomeshwe mara moja!

Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania linapenda kutoa pole na lina Sali kwa ajili ya kuwaombea wahanga wote wa vurugu hizi. Wanawakabidhi kwa Mwenyezi mungu wale wote waliopoteza maisha yao, ili Mwenyezi Mungu apende kuwarehemu. Wanawaombea majeruhi wote wapate kupona haraka. Maaskofu wanatamani kuona wale wote walio nyuma ya matukio haya ya vurugu, mauaji, utekwaji na utesaji wanatafutwa na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linahitimisha tamko lake kwa kuiombea Tanzania amani na utulivu, tunu ambazo ni matunda ya haki, uhuru na kuheshimiana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.