2017-09-11 13:05:00

Papa Francisko anawataka waamini kuwa mashuhuda wa Injili ya upendo


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kubariki Jiwe la Msingi kwa ajili ya makazi ya watu wasiokuwa na makazi maalum yanayoendeshwa na kusimamiwa na Chama cha Kitume cha Talitha Kum, aliungana na familia ya Mungu kwenye Kanisa la Mtakatifu Petro Claver kwa ajili ya kusali Sala ya Malaika wa Bwana. Baba Mtakatifu amemshukuru Mungu kwa kumwezesha kumtembelea Mama Lorenza, mwanamke wa shoka ambaye kwa muda wa miaka hamsini amejitolea kwa ajili ya huduma kwa maskini, kielelezo makini cha huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu.

Baba Mtakatifu anasema, Sala ya Malaika wa Bwan, inawakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho, pale Neno wa Mungu alipofanyika mwili na kukaa kati ya watu wake kwa njia ya Bikira Maria, akawa mwanadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana wanaifanya kwa kumkumbuka Bikira Maria wa Chiquinquirà aliyekuwa na ujasiri wa kugusa kwa heshima kubwa Sanamu ya Bikira Maria iliyokuwa imeharibika sana, akaitunza na kuipatia hadhi yake iliyokuwa imefishwa!

Alifanikiwa kupata nafasi ya kumheshimu Bikira Maria aliyekuwa amembeba Mwanaye wa pekee mikononi mwake, Sanamu ambayo kwa baadhi ya watu haikuwa na maana yoyote katika maisha yao. Hii ndiyo changamoto inayofanyiwa kazi na wale wote wanaotaka kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hawa ndio wale waliojikwaa na kuanguka katika maisha kutokana na madonda makubwa yanayowasakama katika maisha yao. Hawa ni watu wanaopambana na kufa na kupona ili kuweza kufanya kazi na hatimaye, kujipatia makazi bora zaidi; kuwasaidia wasiokuwa na makazi, lakini ni watu wanaosali bila kuchoka ili kuweza kuokoa mng’ao wa utu na heshima ya watoto wa Mungu ambao wamepokwa na wajanja wachache.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu anapenda kuwafundisha waja wake kwa mifano na ushuhuda wa watu wa kawaida kabisa katika maisha kama alivyofanya kwa Mama Maria Ramos. Huyu ni mwanamke wa kawaida kabisa, lakini alibahatika kupewa neema ya kuweza kukusanya na kuhifadhi Sanamu ya Bikira Maria katika hali ya umaskini, Mama Isabela, mwanamke Mahalia na mwanaye Miguel walibahatika kupewa neema na baraka ya kuweza kukarabati joho la Bikira Maria; wakawa ni watu wa kwanza kuona kwa macho ya imani mambo mapya, mwanga angavu wa uwepo wa Mungu anayefunua upendo wake kwa ukamilifu sana. Watu hawa maskini walibahatika kuwa ni watu wa kwanza kumwona Bikira Maria wa Chiquinquirà, wakawa wamisionari wake, watangazaji na mashuhuda wa uzuri na utakatifu wa Bikira Maria.

Katika Sala ya Malaika wa Bwana, waamini wamesali na kumwomba Mtumishi wa Bwana na Mtakatifu Petro Claver; Mtumwa wa wananchi wa Colombia wenye asili ya kiafrika, kama alivyoitwa siku ile alipokuwa anaweka nadhiri zake za daima. Afrika ilikuwa ni mahali pa kuchukua watumwa waliokuwa wanapelekwa katika Ulimwengu mpya. Wakati mwingine alikuwa anatenda kazi hii kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji kutokana na kushindwa kuwasiliana na watu hawa kutokana na utofauti wa lugha. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ukarimu unavuka vikwazo vya lugha zote duniani na kwamba lugha ya huruma na upendo wa Mungu inaeleweka kwa wote.  Injili ya upendo inawasaidia waamini kutambua ukweli na ukweli unapaswa kumwilishwa katika upendo; kwani ukweli na upendo ni sawa na chanda na pete, daima ni mambo yanayoambatana na kukamilishana! Mtakatifu Petro Claver alijisadaka kwa ajili ya kuwahudumia watumwa waliokuwa katika mazingira magumu; akaganga na kutibu madonda yao! Hiki ni kielelezo cha hali ya juuu kabisa cha ushuhuda na ukarimu unaobubujika kutoka katika imani!

Lakini, baada ya kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini, Mtakatifu Petro Claver alifariki dunia katika hali ya upweke kabisa, huku akiwa amesahaulika! Waswahili wanasema, tenda wema, uende zako, usingoje shukrani! Mtakatifu Petro Claver alionesha ushuhuda wa nguvu na wajibu wa jinsi ya kuwahudumia jirani. Alishutumiwa sana na baadhi ya watu waliokuwa wanafaidika kutokana na biashara haramu ya utumwa. Hata leo hii anasikitika kusema Baba Mtakatifu nchini Colombia na sehemu mbali mbali za dunia kuna watu wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, hali inayowafanya kupoteza utu wao kama binadamu na haki zao msingi.

Baba Mtakatifu Francisko anasema Bikira Maria wa Chiquinquirà na Mtakatifu Petro Claver wanawahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; wahamiaji na wakimbizi pamoja na wale wote wanaoteseka na kunyanyasika kutoka na madhara ya utumwa mamboleo. Wote hawa wanao utu na heshima yao kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu!

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko amependa kuihakikishia familia ya Mungu Amerika ya Kusini, uwepo wake kwa njia ya sala, lakini kwa namna ya pekee wakati huu mawazo yake anayaelekeza nchini Venezuela. Amependa kuonesha uwepo wake wa pekee kwa wananchi wote wa Venezuela waliko nchini mwao na wale wote ambao wamelazimika kuikimbia nchi yao kutokana na machafuko ya kisiasa. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka wadau wote kuhakikisha kwamba kwa njia ya majadiliano ya kisiasa, mgogoro wa Venezuela unaweza kupatiwa suluhu ya kudumu, ili kuokoa maisha ya watu wengi wanaoathirika kutokana na machafuko yanayoendelea huko Venezuela.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.