2017-09-10 15:43:00

Tanzia: Kardinali Valasio De Paolis amefariki dunia


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Kardinali Velasio de Paolis aliyefariki dunia, Jumamosi tarehe 9 Septemba 2017 baada ya kuugua kwa muda mrefu. Baba Mtakatifu katika salam zake za rambi rambi kwa Bwana Angelo De Paolis, kaka yake Kardinali Velasio anasema, Marehemu Kardinali Velasio aliweza kuvumilia ugonjwa wake katika hali ya utulivu na imani thabiti, akajiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapenda kutoa salam hizi za rambi rambi kwa familia nzima ya Kardinali Velasio pamoja na wale wote walioguswa na msiba huu mzito.

Baba Mtakatifu anamkumbuka kwa namna ya pekee kabisa kutokana na majiundo yake makini, weledi, umahiri na umakini mkubwa katika masuala ya Sheria; utume ambao aliutekeleza kwa dhati kabisa wakati akifundisha vyuo mbali mbali vya Kipapa hapa Roma, kwa ajili ya mafunzo na majiundo ya mapadre wapya na waamini walei katika ujumla wao! Ni kiongozi aliyejisadaka na kushuhudia huduma makini aliyoitoa bila ya kujibakiza kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Kwanza kabisa kama Katibu mkuu wa Mahakama kuu ya Kanisa, Rais wa Idara ya Uchumi ya Vatican pamoja na majukumu mbali mbali aliyoyatekeleza kwa imani thabiti kama ushuhuda makini wa Upadre na uaminifu kwa Injili ya Kristo.

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua nafasi hii kwa ajili ya kuiombea roho ya Marehemu Kardinali Velasio de Paolis, ili kwa njia ya maombezi ya Bikira Maria na ya Mwenyeheri Giovanni Battista Scalabrini, iweze kupata tuzo ya milele ambayo Kristo Yesu aliwaahidia watumishi wake waaminifu. Baba Mtakatifu anapenda pia kuwapatia wote wanaosikitika na kuomboleza kifo cha Kardinali Velasio de Paolis, baraka zake za kitume na kwa namna ya pekee kabisa anawaombea wale wote waliobahatika kumhudumia katika siku zake za mwisho, alipokuwa mgonjwa.

Wakati huo huo, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anapenda kuungana na wale wote wanaoomboleza kifo cha Kardinali Velasio de Paolis. Anapenda kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake, wale wote wanaosikitika na kuomboleza msiba huu mkubwa wa mtumishi wa Kristo Yesu na Kanisa lake! 

Itakumbukwa kwamba, Marehemu Kardinali Velasio de Paolis alizaliwa kunako tarehe 19 Septemba 1935 huko Sonnino, nchini Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 18 Marchi 1961. Tarehe 30 Desemba 2003 akateuliwa kuwa Askofu mkuu na Katibu mkuu wa Mahakama kuu ya Kanisa na baadaye kama Rais wa Idara ya Uchumi ya Vatican, dhamana aliyoitekeleza hadi tarehe 21 Septemba 2011 alipoamua kung’atuka kutoka madarakani kwa mujibu wa sheria za Kanisa. Tarehe 20 Novemba  2010, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Kardinali. Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemu Kardinali Velasio de Paolis itafanyika Jumatatu, tarehe 11 Septemba 2017, majira ya saa 5:00 kwa saa za Ulaya kwa kuongozwa na Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali. RIP. Amina.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.