2017-09-10 14:44:00

Papa Francisko: watoto wana upendeleo wa pekee machoni pa Kanisa


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Ndege wa Yohane Paulo II kwa kukazia maisha ya Kikristo kama ufuasi unaojikita katika kukumbatia mambo msingi katika maisha ya Kikristo, umuhimu wa kujipyaisha na kuambatana na Kristo Yesu, Jumamosi, tarehe 9 Septemba amekutana na kuzungumza na familia ya Mungu katika nyumba ya Mtakatifu Yosefu “Hogar de San Josè” mjini Medellìn. Amesikiliza ushuhuda na hatimaye, kumshukuru Mtoto Claudia Yesenea kwa ushuhuda wake jasiri ambao umemwezesha Baba Mtakatifu kuguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya watoto sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni wale wanaonyanyaswa na kudhulumiwa na watu wazima.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hata Mtoto Yesu alikumbana na “mkono wa chuma na udhalimu wa Mfalme Herode” kiasi cha kuwafanya wazazi wake kukimbilia uhamishoni Misri. Hata leo hii, kuna watoto wanafariki dunia kutokana na baa la njaa na utapiamlo mkali; magonjwa yanayoweza kuzuilika na kutibika pamoja na ujinga! Watoto hawa ni mboni ya Jicho la Kristo! Kanisa litaendelea kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, haki za watoto zinalindwa na kuheshimiwa na kwamba, watoto wanapewa haki ya kufurahia utoto wao katika mazingira ya amani na utulivu na kwamba, watoto hawa wasipokwe furaha na matumaini yao kwa sasa na kwa siku za usoni!

Baba Mtakatifu amewahakikishia watoto hawa kwamba, wanao upendeleo wa pekee sana machoni pa Yesu, kwani hata katika shida na mahangaiko yao, bado kuna Wasamaria wema wanaoweza kujisadaka na kujitoa kwa ajili ya kuwasaidia; hospitali wanakoweza kupata tiba muafaka na jumuiya wanamoweza kuishi na kufurahia maisha yao. Nyumba ya Mtakatifu Yosefu ni kielelezo upendo na uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati yao; hali inayojionesha kwa njia ya huduma makini ya afya, elimu na ustawi unaofumbatwa katika upendo.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya kuwahudumia watoto kama hawa ambao sasa wamekuwa ni sehemu ya familia yao, kwani wanawatambua na kuwapenda. Ndani ya nyumba hii, wanajihisi kupendwa, kulindwa, kukubalika, kutunzwa na kusindikizwa hatua kwa hatua katika makuzi na malezi yao! Nyumba hii imepewa jina la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi na Baba mlishi wa Yesu aliyemnusuru dhidi ya upanga wa Mfalme Herode, aliyekuwa katili; akawa ni Baba mlinzi na mhudumu wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Hivi ndivyo anavyofanya Mtakatifu Yosefu hata kwa watoto wanaotunzwa katika nyumba hii! Kumbe, hii ni nyumba inayotunzwa na Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha wale wote wanaowahudumiwa watoto sehemu mbali mbali za dunia kuhakikisha kwamba, wanawapokea, wanawatunza na kuwamegea upendo wa dhati, ili kusaidia mchakato wa kuponya madonda na magumu ya maisha ambayo wameonja tangu wakiwa na umri mdogo kabisa! Hii ni huduma inayotoa utambulisho wa Kikristo unaofumbatwa katika upendo unaothubutu kumwona Kristo Yesu kati ya watoto wanaoteseka na kwamba, wanao wajibu wa kuwapeleka watoto hawa kwa Yesu.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaweka wahudumu wote hawa chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu. Anawataka wajifunze kutoka kwake, ili aweze kuwasaidia kuwahudumia vyema watoto hawa wanaoishi katika mazingira magumu, ili hatimaye, watoto hawa kama ilivyokuwa kwa Mtoto Yesu wazidi kuendelea katika hekima na kimo, wakimpendeza Mungu na jirani! Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu iwasindikize, iwalinde na kuwakirimia wema, furaha na nguvu ya kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao. Mazingira haya yawe ni chemchemi ya upendo, amani na furaha; pawe ni mahali pa kutibu na kuganga madonda ya mwili na roho, daima Mwenyezi Mungu awalinde na kuwasaidia. Watambue kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anawabeba katika sakafu ya moyo wake na kwamba, anawaomba wao pia wamsindikize kwa sala na sadaka zao katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.