2017-09-10 15:03:00

Papa Francisko: Mapadre na watawa muwe mashuhuda wa furaha ya Injili


Baba Mtakatifu Francisko anawataka wakleri, watawa, majandokasisi pamoja na familia zao kubaki wakiwa wameshikamana na kuambatana na Ubinadamu wa Kristo Yesu kwa njia ya huduma makini kwa watu wanaoteseka: kiroho na kimwili. Anawataka washikamane na Yesu ili kuabudu Umungu wake unaofichika katika Mafumbo ya Kanisa. Wabaki wamekiwa wameshibana na kulandana na Yesu ili kuishi katika chemchemi ya furaha ya Injili! Huu ni ushauri makini uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 9 Septemba 2017 wakati wa hija yake ya kitume huko Medellìn, nchini Colombia.

Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu kwenye Karamu ya Mwisho, aliwaonesha Mitume wake Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa kuwaosha miguu mitume wake! Aaliwataka kumkumbuka daima kwa kuumega mkate wanapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu. Bikira Maria alikuwa ameungana na Mitume wa Yesu, Siku ile Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume na hivyo kutoka kifua mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Huu ndio ushuhuda uliotolewa mbele ya Baba Mtakatifu Francisko na Sr. Ledy wa Mtakatifu Yosefu, Maria Isabel pamoja na Padre Juan Filipe walishuhudia chemchemi ya miito yao na kwamba, kumfahamu Kristo Yesu ni zawadi kubwa sana inayopita zawadi zote duniani! Kwa kukutana na Yesu katika hija ya maisha ni tukio kubwa sana linaloshuhudiwa kwa maneno matendo ya wafuasi wake, sababu ya furaha yao ndani na Kanisa katika ujumla wake! Vijana wengi wameweza kumgundua Kristo Yesu kwa njia ya shuhuda zenye mvuto na mashiko zilizotolewa na jumuiya za wakleri na watawa, hali ambayo inawajaza vijana ari na moyo wa kutaka kujisadaka kwa ajili ya Kristo ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda, kielelezo makini cha imani tendaji!

Baba Mtakatifu Francisko anasikitishwa sana na madhara yanayosababishwa na biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Si haba, Medellìn ni kitovu cha biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya duniani, hali ambayo imefifisha matumaini ya vijana wengi ndani na nje ya Colombia. Wale wote ambao wamekuwa ni sababu na vikazo vya matumaini ya vijana kwa kuwatumbukiza katika ombwe na matumizi haramu ya dawa za kulevya wanapaswa kufanya toba na kuomba msamaha mbele ya Mungu. Jumuiya za Kikristo zishikamane ili kuwasaidia vijana kutoka katika mazingira haya hatarishi kwa kuwajengea msingi thabiti wa Imani, matumaini, mapendo, maadili na utu wema. Waguswe na upendo wa Kristo ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili kati pamoja na vijana wenzao. Imani inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha, ili kuwawezesha vijana kuwa ni sehemu endelevu ya watu wa Agano la Mungu kama walivyokuwa Manabii wa Mungu: Yeremia, Isaya na Ezekieli.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, licha ya mazingira magumu na tete katika maisha na utume wa Kanisa nchini Colombia, lakini bado miito inaendelea kuchipua kama Mtende wa Lebanoni. Hata katika kinzani na maporomoko ya kanuni maadili na utu wema, Mwenyezi Mungu bado anaendelea kuita vijana ili wajisadake katika maisha na wito wa kipadre na kitawa. Hata katika mazingira ambamo Injili ya familia inakabiliwa na changamoto za utepetevu wa Imani, ukarimu, uaminifu na udumifu, hata huko bado anaendelea kuwaita vijana ili wamtumikie! Colombia ni nchi ambayo imelowanishwa kwa vita, ghasia na mateso ya watu wasiokuwa na hatia, kama inavyosimuliwa hata katika Maandiko Matakatifu! Lakini, hata katika mazingira kama haya, Mwenyezi Mungu anaendelea kufanya miujiza yake kwani kila binadamu anao udhaifu unaomsumbua katika maisha yake. Waamini mjini Medellìn wanapaswa kuchakarika ili kuhakikisha kwamba, familia zao zinakuwa walau ni chemchemi  ya miito mitakatifu kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Colombia! Siri ya mafaniko inafumbatwa katika ushuhuda makini, katika ukweli na haki; kwa kuwasaidia vijana kuweza kutimiza ndoto zao, daima wakijifananisha na Kristo Yesu, Mchungaji mkuu!.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, miito mitakatifu ya maisha ya upadre na utawa inakauka na kunyauka kama maua ya kondeni kutokana na baadhi ya mapadre na watawa kupenda mno: unasa kwa kujitafuta na kujikweza; kwa kuwa na uchu wa madaraka, mali na utajiri wa haraka haraka. Baba Mtakatifu anawakumbusha watawa kwamba, fedha ni fedheha katika maisha na wito wao, wasipende sana kumezwa na malimwengu, kwani haiwezekani kuwatumikia mabwana wawili, yaani Mungu na mali. Ukavu na uchakavu wa maisha na wito wa kipadre na kitawa unaojionesha katika ”udaku” kwa kutumia vibaya wema na upendo wa watu wa Mungu kwa ajili ya kujinufaisha binafsi; kwa kuwakosesha fursa wazee, wagonjwa na watoto nafasi ya kuonja huruma na upendo wa Mungu ndani ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, hata katika mazingira ya ukavu na uchakavu wa maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili, bado watu wa namna hii wanapewa nafasi na Mwenyezi Mungu ili kutubu na kumwongokea, ili waweze kuzaa tena matunda mema kwa wakati wake. Colombia ina mifano ya watakatifu kama Mtakatifu Laura Montoya, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutetea na kulinda utu na heshima ya wananchi mahalia wa Colombia. Kuna Mwenyeheri Mariano wa Yesu Euse Hoyos, moja wa wanafunzi wa kwanza kabisa wa Seminari ya Medellìn, bila kuwasahau mapadre, watawa na waamini walei ambao mchakato wa kuwatangaza kuwa wenyeheri na watakatifu bado unaendelea! Hawa ni mashuhuda wa Injili ya Kristo na Kanisa lake! Hata leo hii, bado kuna uwezekano wa kuzaa matunda mema kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa nchini Colombia!

Kama wafuasi amini wa Yesu, bado wanaendelea na mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kristo na kwamba, wanahamasishwa kubaki wakiwa wameshikamana na kulandana na Yesu katika ubinadamu wake unaofumbatwa katika huduma makini kwa familia ya Mungu, inayoshuhudiwa na mifano bora ya Wasamaria wema. Wasimame kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; wapambane na umaskini wa hali na kipato kwa kuwajengea watu wa Mungu uwezo wa kiuchumi, kiutu na kimaadili; kwa kupinga rushwa, ufisadi, vita na ghasia. Wawe ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Kristo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kwa kutangaza Injili ya Kristo, kwa kupambana na dhambi na madhara yake pamoja na kujisadaka bila ya kujibakiza katika huduma katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa!

Wafuasi wa Kristo wajibidishe kumfahamu, kumpenda na kumtumikia kwa akili na mioyo yao yote! Mahali pa kwanza pa kuweza kukutana na Kristo Yesu ni kwa njia ya Tafakari ya kina kwenye Maandiko Matakatifu, chemchemi ya upendo, utii na huduma makini kwa watu wa Mungu. Asiyependa Neno la Mungu, kamwe hawezi kumpenda Kristo Yesu. Majiundo ya awali na endelevu yawasaidie kumwilisha huruma na upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu wanaowahudumia. Wawe makini kusoma alama za nyakati na kujibu kilio cha watu wao. Wawe ni watu wa sala inayowawezesha kuwa huru katika: kuomba, kushukuru, kusifu na kutukuza. Wajifunze kudumisha ukimya katika maisha, ili kutoa nafasi kwa Mwenyezi Mungu kuweza kuzungumza kutoka katika undani wa maisha yao! Mapadre na watawa wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upatanisho; matumaini na furaha ya watu wa Mungu.

Wafuasi wa Kristo lazima wawe ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili ambayo hakuna mtu awaye yote anayeweza kuwapokonya kutoka katika undani wa maisha yao anasema Baba Mtakatifu Francisko. Mwenyezi Mungu hafurahii kuwaona mapadre na watawa wenye nyuso zilizokunyamana kama ”matuta ya mihogo”. Ushuhuda wa furaha yao unapaswa kububujika kutoka katika upendo wa Mungu na kwamba, wao ni vyombo vya neema inayong’aa na kuwawezesha watu kukutana na Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wazazi wa mapadre, watawa na majandokasisi, kielelezo kwamba, bado Mwenyezi Mungu anatupia jicho kwenye jumuiya, familia na nchi ya Colombia katika ujumla wake. Wao ni kielelezo cha upendeleo wa Mungu kwa watu wake, changamoto ni kuendelea kujisadaka katika upendo kwa kuunganisha huduma yao na Kristo Yesu, chemchemi ya maisha na mwanzo mpya kwa nchi ya Colombia dhidi ya mafuriko ya vita, ghasia na machafuko ya kijami, ili kupandikiza tena matunda ya haki na amani; kwa kujenga madaraja ya watu kukutana na kushikamana katika ujenzi wa umoja wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.