2017-09-09 15:32:00

Papa Francisko asema, ulemavu ni sehemu ya udhaifu wa binadamu!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 7 Septemba 2017 akiwa kwenye Ubalozi wa Vatican mjini Bogotà, nchini Colombia, alikutana na kuzungumza na walemavu kwa kuwatia shime kwamba, hii ni sehemu ya fumbo la maisha ya mwanadamu na kwamba, kila mwanadamu anakabiliwa na aina fulani ya ulemavu katika maisha yake. Baba Mtakatifu alipata fursa ya kusikiliza shuhuda za mateso na mahangaiko yao ya ndani; imani, matumaini na mapendo yao. Wote hawa amewaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, faraja ya wagonjwa.

Baba Mtakatifu katika hija yake anakutana na makundi mbali mbali ya watu ili kujionea mwenyewe hali halisi ya maisha ya familia ya Mungu nchini Colombia. Licha ya matatizo na changamoto wanazokumbana nazo katika maisha, wamekuwa ni watu wenye furaha, imani na matumaini makubwa walipokutana na kusalimiana na Baba Mtakatifu Francisko. Haya ni makundi ya watu wenye ulemavu wa kusikia, ambao walifikishiwa ujumbe kwa njia ya lugha ya alama; watoto wenye ulemavu na yatima.

Makundi yote haya yaliandaa video video kama ushuhuda unaoonesha jinsi ambavyo walijiandaa kwa sala na ushuhuda kwa ajili ya kumpokea na kumkaribisha nchini Colombia kama hujaji wa amani na upatanisho. Yamewahamasisha wagonjwa na wazee kutolea shida na mahangaiko yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Colombia ambayo imepata bahati ya kutembelewa na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amewashukuru kwa uwepo na ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha na utume wa Kanisa nchini Colombia. Hata katika udhaifu wa mwili, bado utu na heshima yao kama binadamu inapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote.

Ulemavu ni sehemu ya udhaifu wa kibinadamu unaopaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa na pale inapowezekana kupatiwa tiba muafaka. Ni Mwenyezi Mungu peke yake ambaye ni mkamilifu, mtakatifu, mwingi wa huruma na mapendo. Kutokana na udhaifu wa kibinadamu, watu wote wanahitaji huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwani kabla hujafa, hujaumbuka wanasema, waswahili! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapatia baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.