2017-09-06 14:26:00

Papa Francisko atuma salam na matashi mema kwa viongozi wakuu wa nchi


Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuondoka kwenye makazi yake ya Hostel ya Santa Martha mjini Vatican kuelekea nchini Colombia, Jumatano tarehe 6 Septemba 2017 amekutana na kusalimiana na familia mbili kutoka Italia ambazo hivi karibuni zilikumbwa na janga la moto ambao uliunguza makazi yao katika eneo la “Ponte Mammolo” mjini Roma. Kwa sasa familia hizi zinahudumiwa na Vatican kama, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya upendo! Baba Mtakatifu alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Fumicino amepokewa na hatimaye, kuagwa na viongozi wa Serikali ya Italia na Kanisa. Akiwa njiani kuelekea Colombia, Baba Mtakatifu ametuma salam na matashi mema kwa wakuu wa nchi kumi na mbili ambazo ni: Italia, Ufaransa, Hispania, Ureno, Marekani, Ocean, Porto Ricco, Antille, Netherlands, Venezuela, Barbados, Grenada, Trinidad na Tobago.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia, amemwambia kwamba, anakwenda nchini Colombia ili kuenzi utume wa Kanisa mahalia sanjari na kuwapelekea ujumbe wa matumaini wananchi wote wa Colombia. Anapenda kumtakia heri na baraka yeye na familia yote ya Mungu nchini Italia. Baba Mtakatifu anamwomba Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kumfikishia salam na matashi mema kwa wananchi wote wa Ufaransa. Anaitakia familia ya Mungu nchini Hispania: furaha, amani, ustawi na maendeleo.

Papa Francisko amewasalimia wananchi wa Marekani katika ujumla wao, chini ya uongozi wa Rais Donald Trump. Amewabariki wananchi wote wa Netherland wakati alipokuwa anapita juu ya anga la nchi yao. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu ameonesha mshikamano wake wa upendo na familia ya Mungu nchini Venezuela. Amewaombea mshikamano, haki, maridhiano na amani. Amewatakia heri na baraka wananchi wa Barbados na kuwahakikishia wananchi wa Grenada sala na uwepo wake wa kiroho hata kwa wananchi wa Trinidas na Tobago.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.