2017-09-05 11:34:00

Papa Francisko ni mjumbe wa amani na mmisionari wa upatanisho Colombia


Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 6 – 11 Septemba 2017 anafanya hija ya kitume nchini Colombia kama sehemu ya mchakato wa kuenzi maridhiano, haki na amani, baada ya Colombia kuwa katika mapigano kwa muda mrefu. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu ataondoka mjini Roma, Jumatano tarehe 6 Septemba 2017 na kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Bogotà saa 10:30 Jioni kwa saa za Ulaya na kupatiwa mapokezi ya kitaifa.  Hija hii ya kitume nchini humo inaongozwa na kauli mbiu “Demos el primer paso” yaani “Tupige hatua ya kwanza”. Huu ni mwaliko kwa familia ya Mungu nchini Colombia kupiga hatua madhubuti katika mchakato wa ujenzi wa haki, amani na upatanisho kwa kufuata nyayo za Baba Mtakatifu Francisko ambaye amejipambanua kuwa kweli ni “Mmissionari wa upatanisho”.

Ni hija inayosimikwa katika ukweli na uwazi; huruma, upendo na upatanisho wa kitaifa ukizingatia kwamba,  katika kipindi cha miaka 50 ya vita ya wenyewe kwa wenyewe zaidi ya watu 260, 000 wamepoteza maisha; watu 600, 000 wamepotea katika mazingira ya kutatanisha na zaidi ya watu millioni 7 hawana makazi ya kudumu na wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ili kusalimisha maisha yao ugenini. Colombia bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano; bado madhara ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya yanaonekana miongoni mwa vijana wa kizazi kipya bila kusahau makovu ya vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Colombia!

Askofu mkuu Ettore Balestrero, Balozi wa Vatican nchini Colombia katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakaza kusema, licha ya mapungufu yote haya, Baba Mtakatifu mbele yake anatarajia kukutana na umati wa familia ya Mungu nchini Colombia, yenye utajiri mkubwa wa utamaduni na mapokeo hai; Colombia inayojitahidi kuchachamalia ustawi na maendeleo na kwamba, Kanisa linaendelea kuihamasisha familia ya Mungu nchini Colombia kujipatanisha na Mungu, jirani zao pamoja na kazi ya uumbaji. Colombia kwa sasa iko mstari wa mbele kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela wanaokabiliana na hali ngumu ya maisha.

Askofu mkuu Ettore Balestrero anasema, Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija ya kitume nchini Colombia kama hujaji wa matumaini na upatanisho; anataka kuwasaidia wananchi kupiga hatua madhubuti ya upatanisho kati yao na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao; tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya haki na amani; upendo na mshikamano. Huu ni mwaliko kwa familia ya Mungu nchini Colombia kutokubali tena kutumbukizwa kwenye kishawishi cha rushwa, fitina na kinzani zisizokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Colombia, bali wakiwa wameshikamana, wawe tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Colombia mpya inayomsikwa katika haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Hatua kubwa imekwishafikiwa kwa vikosi vya waasi kusalimisha silaha zao, changamoto bado ni ardhi ambayo bado inamilikiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya. Miaka 53 ya vita ya wenyewe kwa wenyewe imeacha makovu makubwa katika maisha ya watu, lakini sasa mchakato wa maendeleo unajielekeza zaidi mijini, ikilinganishwa na hali illivyo vijijini. Ghasia, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya bado ni changamoto kwa familia ya Mungu nchini Colombia. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko inapania pamoja na mambo mengine kuwahamasisha wananchi wa Colombia kupyaisha nchi yao kwa kuzingatia tunu msingi za Kiinjili, kanuni maadili na utu wema.

Vita, ghasia, utekaji nyara wa watu; utumikishwaji wa watoto jeshini na kwenye kazi za suluba, mashambulizi  dhidi ya miundombinu ya serikali ni mambo ambayo kwa sasa yameanza kupitwa na wakati. Kanisa pia limegharimia sana mchakato wa upatanisho, haki na amani na kwamba, waathirika wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Colombia, hawana budi kupewa kipaumbele cha kwanza kama suluhu ya mgogoro huu. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kusali kwenye Msalaba ambao ni kumbu kumbu ya mauaji Bojaya yaliyojitokeza nchini Colombia kunako mwaka 2002. Hii ni sala kwa ajili ya kuwaombea wahusika na waathirika wote; ili kwa njia ya toba na wongofu wa ndani; waweze wote kuwa tayari kukumbatia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Colombia mpya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.