2017-08-30 16:13:00

Simamieni rufuku ya utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha!


Baba Mtakatifu Francisko anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwajengea walimwengu matumaini kwa kufanya maamuzi magumu, yatakayoiwezesha dunia kuweza kuishi kwa amani na utulivu, pasi na hofu wala mashaka ya mashambulizi ya silaha za kinyuklia. Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujadili katika ukweli na uwazi, ili hatimaye, kuunda chombo cha kisheria kitakachoweza kusimama kidete kuzuia na hatimaye kupiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha ya kinyuklia ulimwenguni.

Ili kuweza kufikia maamuzi haya magumu, kuna haja ya kuzingatia mambo makuu yafuatayo, anasema Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa katika mkutano wa Umoja wa Mataifa uliofanyika hivi karibuni, ili kuratibu mchakato huu muhimu sana katika kudumisha ulinzi na usalama dhidi ya vitisho vya matumizi ya silaha za kinyuklia duniani. Anasema, kuna haja kuondokana na malumbano yasiyokuwa na tija wala mashiko kuhusu mahangamizi yanayoweza kusababisha na matumizi ya silaha za kinyuklia na badala yake, Jumuiya ya Kimataifa ijenge na kudumisha umoja na udugu unaosimikwa katika kanuni maadili, amani na utulivu.

Ili kukuza na kudumisha amani duniani, kuna haja ya kuendeleza majadiliano yanayojikita katika ukweli na uwazi kwa kuruhusu watu kukutana, kujadiliana na hatimaye, kuimarisha hali ya kuaminiana kati ya nchi moja na nchi nyingine kwani wasi wasi mkubwa unajengwa kutokana na mataifa kudhaniana vibaya, sumu kali katika majadiliano ya kimataifa. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kufanya maamuzi magumu katika historia kwa kuharibu silaha zote za atomiki, zilizopo na zile ambazo zimehifadhiwa sanjari na kupiga rufuku utengenezaji wake kwa siku za usoni. Maamuzi haya yanahitaji kwa namna ya pekee utashi wa kisiasa na kuchumi.

Mataifa yote yanapaswa kuunganisha sauti ili kulaani utengenezaji wa silaha hizi kwani unaweza kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Utengenezaji na hatimaye, matumizi ya silaha hizi za mahangamizi ni ukiukwaji mkubwa wa haki ya kimataifa na kwamba, mataifa yote yanapaswa kulaani vitendo hivi bila kumung’unya maneno! Nchi zitakazohusika kutengeneza na hatimaye kutumia silaha za kinyuklia ziwajibike kulipia madhara yatakayosababisha na silaha hizi kwa watu na mali zao pamoja na maeneo yale yote yatakayoathirika kutokana na majaribio ya silaha za kinyuklia.

Jumuiya ya Kimataifa anasema, Askofu mkuu Auza haina budi kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, inarithisha utamaduni wa haki, amani na maridhiano kwa vijana wa kizazi kipya ili kutambua kwamba, amani inaweza kupatikana duniani kwa njia ya majadiliano na wala si lazima kwa njia ya matumizi ya silaha za mahangamizi. Ili kweli haki, amani na maridhiano kati ya watu yaweze kupata nafasi katika akili na nyoyo za watu katika medani za kimataifa, kuna haja ya kuwekeza zaidi na zaidi katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu. Mkutano huu anasema Askofu mkuu Bernadito Auza ulikuwa unataka kupambana na changamoto dhidi ya woga na wasi wasi; mambo ambayo yanaendelea kutawala Jumuiya ya Kimataifa kutonana na utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.