2017-08-30 15:54:00

Acheni matumizi ya silaha duniani; wekezeni kwenye maendeleo endelevu


Kunako mwaka 2009 Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio kwamba, kila mwaka ifikapo tarehe 29 Agosti, itakuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Silaha za Atomiki, ili hatimaye, Jumuiya ya Kimataifa iweze kupiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi yake, kwani madhara ya silaha za atomiki ni makubwa sana. Baba Mtakatifu Francisko tangu mwanzo wa utume wake, amekuwa akiitaka Jumuiya ya Kimataifa kuachana na biashara pamoja na matumizi ya silaha duniani. Vitisho vya mashambulizi ya kijeshi, anasema Baba Mtakatifu, kamwe haviwezi kuwa ni msingi wa kanuni maadili; udugu, amani na utulivu kati ya watu wa Jumuiya ya Kimataifa.

Kuna kiasi kikubwa sana cha rasilimali fedha na watu kinachowezekwa katika kutengeneza na kufanya majarabio ya silaha za mahangamizi, lakini kwa bahati mbaya, hii ni rasilimali ambayo inapokwa kutoka kwa wananchi! Utajiri wote huu anasema Baba Mtakatifu Francisko ungeweza kutumika kwa ajili ya kupambana na baa la umaskini linaloendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu, ili kuweza kuboresha maisha ya watu wengi zaidi. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa hawana budi kuhakikisha kwamba, kweli dunia inakuwa huru pasi na vitisho vya silaha za mahangamizi, kwa kuhakikisha kwamba, Itifaki ya Makubaliano ya kupiga rufuku, utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia inatekelezwa kwa vitendo.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa Siku ya 50 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2017 iliyoongozwa na kauli mbiu “Kutotumia nguvu: mtindo wa siasa ya amani”, anaelezea kuhusu vita, kinzani na mipasuko ya kijamii duniani; umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; umuhimu wa kuzamisha mizizi katika siasa za kutotumia nguvu. Utu na heshima ya watu wanaoishi katika maeneo ya vita unapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa, kwa kushinda kishawishi cha kutumia siasa ya vita.

Miaka 50 iliyopita, Mwenyeheri Paulo VI alituma ujumbe wa amani kwa familia ya Mungu duniani kwa kuonesha kwamba, amani ni chachu ya maendeleo ya watu na kwamba, kinzani, misigano na utaifa usiokuwa na mashiko ni mambo yaliyokuwa yanatishia amani. Kumbe, vita, migogoro na kinzani mbali mbali zinaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kujikita katika: sheria, haki, usawa, upendo; ukweli na uhuru, tunu ambazo zinaonesha umuhimu wa pekee hata katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuachana na unafiki wa kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii katika misingi ya woga na hofu. Kumbe, lengo la kutokomeza silaha za mahangamizi ni wajibu wa kimaadili na kiutu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.