2017-08-29 14:55:00

Serikali ya Tanzania ina thamini mchango wa watawa katika huduma!


Shirikisho la Mashirika ya Watawa wa Kike Afrika Mashariki na Kati, ACWECA, kuanzia tarehe 26 Agosti hadi tarehe 2 Septemba 2017, linafanya mkutano wake wa 17 unaoongozwa na kauli mbiu “Kuimarisha umoja wetu katika uinjilishaji wa kina mintarafu mazingira changamani ya nyakati hizi”. Mkutano huu umefunguliwa rasmi, Jumapili, tarehe 27 Agosti 2017 kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali João Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume kwenye Kikanisa cha Makao makuu ya Sekretarieti ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Kurasini, Jijini, Dar Es Salaam. Katika mahubiri yake, aliwataka watawa kuepuka kishawishi cha uchu wa fedha na mali na badala yake, wageuze fedha na mali hizi kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa wajumbe hawa amewataka kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano kati yao; kugundua upya wa Injili unaowataka kujikita katika kipaji cha ugunduzi, ili kusoma alama za nyakati na kujibu changamoto za watu wa Mungu wanaowahudumia. Watawa wanapaswa kutambua kwamba, Kanisa linathamini mchango wao mkubwa katika huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo endelevu ya jamii. Wamekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa malezi, makuzi na majiundo ya watoto na vijana wa kizazi kipya.

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na walemavu, amewataka watawa kusaidia mchakato wa ujenzi wa jamii inayojikita katika: nidhamu, uwajibikaji, kanuni maadili na utu wema, ili kushiriki kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya watu: kiroho na kimwili. Serikali ya Tanzania inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na watawa katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo endelevu ya jamii.

Watawa wamekuwa kweli ni chachu ya mabadiliko na maendeleo katika jamii. Dhamana na mchango wa watawa hata ndani ya Kanisa lenyewe ni mkubwa, kwani wamekuwa wakitumia rasilimali watu na fedha kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa sanjari na kuwajengea wananchi uwezo: kiutu, kiuchumi na kijamii. Waziri Jenista Joakim Mhagama amewataka watawa nchini Tanzania kusaidia mchakato wa utekelezaji wa sera na azma ya Serikali ya kutaka kujenga jamii inayofumbatwa katika kanuni maadili, nidhamu, utu wema na uwajibikaji kama njia ya kupambana na saratani ya rushwa, ufisadi na vitendo vya jinai. Amesema, Serikali ya Tanzania inaangalia uwezekano wa Kuupatia Umoja wa Mashirika ya Kitawa Tanzania, TCAS, sehemu ya ardhi, ili kuanza mchakato wa ujenzi wa Makao yao Dodoma, wakati huu Serikali ya Awamu ya Tano inapoendelea kutekeleza uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma kama Makao Makuu ya Nchi ya Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.