2017-08-28 08:25:00

Papa Francisko: Kila Mkristo ana thamani katika ujenzi wa Kanisa


Injili ya Jumapili ya XXI ya Kipindi cha Mwaka wa A wa Kanisa inaonesha mapito muhimu sana katika maisha, utume na mahusiano ya Yesu na wafuasi wake. Alitaka kuhakikisha imani yao kwake na jinsi ambavyo watu walijitahidi kumfahamu kama Nabii, lakini wakashindwa kuingia katika undani wa maisha na utume wake. Ndiyo maana Yesu anaamua kuwauliza wafuasi wake kwamba, wao wanamtambua kuwa ni nani? Yesu alitegemea kupata jibu la kina ikilinganishwa na majibu yaliyokuwa yanayotelwa na watu mbali mbali, kwani wafuasi wake walimtambua kwa karibu zaidi.

Mtakatifu Petro, mtume anatoa jibu la kina kwa kusema, “Wewe ndiye Kristo Mwana wa Mungu aliye hai”. Haya ni maneno mazito na ya kina yanayozidi uwezo na ufahamu wa Mtume Petro, mvuvi wa kawaida kabisa kama alivyofahamika na wengi! Kumbe, haya ni maneno ambayo yalikuwa yanabubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye alimfunulia Petro siri na utambulisho wa Kristo Yesu kwamba, alikuwa ni Mwana wa Mungu, Masiha aliyepakwa mafuta na kutumwa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Jibu la Petro Mtume ni kiini cha imani aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu na hapa kuna msingi thabiti ambao Yesu Kristo ana amua kuutumia ili kujenga Jumuiya yake, kujenga Kanisa lake. Ndiyo maana Yesu anamwambia Petro kwamba, ni mwamba na juu ya mwamba huu, atalijenga Kanisa lake. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 27 Agosti 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hata leo hii, Yesu anataka kuendeleza mchakato wa ujenzi wa Kanisa lake katika msingi imara, lakini kuta zake zinaonekana kuwa na nyufa, zinazopaswa kurekebishwa na kufanyiwa ukarabati.

Waamini leo hii, hawawezi “kujigamba” kuwa eti ni msingi wa Kanisa la Kristo, lakini wao ni mawe madogo madogo, lakini yenye thamani kubwa mbele ya Kristo, kwani anayaangalia, anayapima na kuyatengeneza kadiri ya Roho wake na kuliweka kila jiwe mahali pake, kadiri ya mapenzi yake na umuhimu wake katika ujenzi wa Kanisa. Wakristo katika ujumla wao ni mawe hai yanayoshiriki kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa! Mawe yote haya ni mali ya Kristo mwenyewe na yana utimilifu wa maisha ndani ya Roho Mtakatifu, ni maisha yanayofumbatwa katika upendo, kiasi kwamba, kila mtu anayo nafasi katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, Kanisa ni Jumuiya inayosimikwa katika maisha kutoka kwenye mawe yenye asili mbali mbali, lakini ambayo kwa pamoja yanajenga Kanisa moja alama ya udugu na umoja. Kristo Yesu, kwa utashi wake, ametamtaka Petro Mtume, kuwa ni kiini na kielelezo kinachoonekana cha umoja wa Kanisa! Hata Petro Mtume, “si mali kitu” anasema Baba Mtakatifu Francisko, ni jiwe dogo lililopata upendeleo wa pekee kutoka kwa Kristo Yesu na sasa limekuwa ni kiini cha umoja. Hii ni dhamana iliyotekelezwa na Petro Mtume, pamoja na wale wote ambao wangeendeleza dhamana na utume huu kama waandamizi wake! Baba Mtakatifu anasema hawa Kanisa limewatambua kuwa ni Maaskofu wa Roma, mji ambao Mitume Petro na Paulo, miamba wa imani waliweza kumshuhudia Kristo Yesu kwa kuyamimina maisha yao.

Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu, amewadhaminisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa Mitume na Mama wa Kanisa. Bikira Maria alikuwemo kwenye Chumba cha juu, pembeni mwa Mtakatifu Petro, pale Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume na kuwapatia nguvu ya kutoka nje kutangaza na kushuhudia kwamba, Yesu ni Bwana. Leo hii, Bikira Maria anaendelea kuwategemeza Wakristo, kwa maombezi na maongozi yake, ili kupata umoja ule ambayo Yesu alisali kwa ajili yake na Mitume wakauombea na hatimaye, kumwaga damu yao kwa ajili ya umoja huo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.