2017-08-26 10:06:00

Yaliyojiri katika ziara ya kikazi ya Kardinali Parolin nchini Russia


Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican anasema, ziara yake ya kikazi nchini Russia kuanzia tarehe 20 hadi 24 Agosti 2017 imekuwa ni safari ya matumaini na yenye mafanikio makubwa katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene na mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Russia. Majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa la Kiorthodox la Russia na Kanisa Katoliki yamefungua ukurasa mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika kukabiliana na changamoto mamboleo: kiroho, kimwili na kimaadili.

Makanisa katika ujumla wake, yanayo dhamana kubwa ya kuchangia katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Makanisa yanapaswa kushikamana na kushirikiana katika harakati za kuwasaidia na kuwategemeza Wakristo huko Mashariki ya Kati na kwamba, hii ni sehemu ya majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika sala, ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake sanjari na huduma makini kwa waathirika wa vita, kinzani na nyanyaso za kidini huko Mashariki ya Kati.

Kardinali Parolin anapenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyemwezesha kukamilisha ziara hii ya kikazi ambayo ina mchango mkubwa sana katika maisha na utume wa Kanisa. Mazungumzo na majadiliano ambayo ameyafanya na viongozi wa Kanisa la Kiorthodox la Russia yamekuwa na mafanikio makubwa. Viongozi hawa ni Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Russia nzima na Askofu mkuu Ilarione Volokolamsk, Rais wa Idara ya uhusiano na ushirikiano wa Kimataifa wa Kanisa la Kiorthodox la Russia. Wengine ni: Bwana Sergiey Lavrov, Waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa nchini Russia pamoja na Rais Vladimir Putin wa Russia.

Kardinali Parolin anakiri kabisa kwamba, katika mazungumzo na viongozi wote hawa, kumekuwepo na hali ya amani na utulivu iliyojengeka katika utamaduni wa kusikilizana kwa makini sanjari na kuheshimiana kama ndugu wamoja. Ni mazungumzo ambayo yanapania kujenga zaidi na kwamba, kwa uwepo wake mwenyewe ameweza kujionea hali halisi ya maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Russia. Ameshuhudia furaha ya watu wa Mungu, matumaini, matatizo na changamoto zinazowakabili.  Mosi ni ombi la Kanisa Katoliki kurejeshewa tena nyumba zake za Ibada, ili kuwahudumia waamini wa Kanisa Katoliki nchini Russia.

Baada ya kuwasili mjini Vatican, Kardinali Parolin, amepata nafasi ya kufanya marejesho ya ziara yake ya kikazi nchini Russia kwa Baba Mtakatifu Francisko. Amewasilisha salama na matashi mema kutoka kwa viongozi wa Serikali ya Russia, Viongozi wa Kanisa pamoja na waamini wenye mapenzi mema aliobahatika kukutana nao wakati alipokuwa nchini Russia. Kwa namna ya pekee, amewasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Patriaki Cyril  anayekumbuka kwa heshima, ule mkutano uliofanyika kati yake na Baba Mtakatifu Francisko Februari, 2016 mjini Havana, Cuba na hatimaye, wakatoa tamko la pamoja linalojulikana kama Tamko la Havana, Cuba, linalotoa dira na mwelekeo sahihi wa ushirikiano na mshikamano wa kiekumene kati ya Makanisa haya mawili kama sehemu ya mchakato unaopania kukabiliana na changamoto mamboleo. Kimsingi, viongozi wote wameridhishwa na fursa za majadiliano walizobahatika kupata na hatimaye, kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ana kwa ana, hatua muhimu sana katika ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Kardinali Parolin anafafanua yale yaliyojiri katika mazungumzo kati yake na Patriaki Cyril kwamba: ni kuhusu majadiliano na ushirikiano wa kiekumene uliojengeka katika miaka ya hivi karibuni kati ya Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Katoliki; Tamko la Havana Cuba; Ibada kwa Mtakatifu Nicholaus wa Bari iliyowaunganisha waamini wa Makanisa haya mawili na umuhimu wa kuendeleza uekumene wa sala na ushuhuda wa maisha ya Kikristo hata kiasi cha kumwaga damu pale inapowabidi. Ni ushirikiano na mshikamano unaopaswa kuimarishwa na kudumishwa na wote katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, lakini, kubwa zaidi ni huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama kielelezo cha imani kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini wa Makanisa haya mawili wanajitahidi sasa kuanza kuandika historia mpya ya mshikamano baada ya kufanya mang’amuzi na upembuzi wa kina!

Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii nchini Ukraine ni kati ya mada tete ambazo Kardinali Parolin amejadili na viongozi wa Kanisa pamoja na Serikali ya Russia wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Russia. Utekelezaji wa Mkataba wa Minsk ni kati ya mambo yanayopewa uzito wa juu na Vatican, ili kuweza kupata amani ya kudumu nchini Ukraine. Msaada wa kiutu ni muhimu kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wanaoteseka huko Ukraine, hali inayoweza pia kufungua majadiliano ya kisiasa katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Ukraine. Kardinali Parolin anakaza kusema, wamejadiliana uwezekano wa kuwaachia wafungwa wanaoshikiliwa; umuhimu wa kusitisha vita ili amani, utulivu na hatimaye, kuanzisha mchakato wa upatanisho wa kitaifa katika ukweli na haki!

Kardinali Parolin anasema mazungumzo yake na Rais Vladimir Putin wa Russia yalipewa uzito wa juu na vyombo vya habari kimataifa na kitaifa hasa kutokana na umuhimu wa Russia katika upatikanaji wa suluhu ya kudumu huko Mashariki ya kati, ambako kumegeuka kuwa ni uwanja wa mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Vita na ghasia nchini Ukraine; machafuko ya kisiasa pamoja na mpasuko wa mafungamano ya kijamii nchini Venezuela ni kati ya mambo ambayo wamejadiliana kwa kina na mapana. Russia kutokana na historia, uwezo wake wa kiuchumi, kitamaduni na kisiasa, inao mchango mkubwa katika Jumuiya ya Kimataifa, hasa katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Kardinali Parolin, anamshukuru Mwenyezi Mungu aliyemwezesha kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na baadhi ya waamini wa Kanisa Katoliki nchini Russia. Ameshuhudia na kuguswa na ibada pamoja na imani ya watu wa familia ya Mungu nchini Russia. Walionesha ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Alipata nafasi ya kuwatembelea na kuwasalimia Watawa wa Shirika la Wamissionari wa upendo, maarufu kama Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta wanaofanya utume wao mjini Moscow. Ametembelea na kusali kwenye Kanisa kuu la Kristo Mkombozi, huko Moscow, lililobomolewa na utawala wa Kikomunisti, uliotaka kufutilia mbali imani na uwepo wa Mungu kati pamoja na watu wake, lakini hawakuweza na leo hii, watu wanaendelea kusali na kumwamini Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.