2017-08-23 10:24:00

Yanayojiri katika ziara ya kizazi ya Kardinali Parolin nchini Russia


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika ziara yake ya kikazi nchini Russia kuanzia tarehe 20 hadi tarehe 24 Agosti 2017 anasema, ni wakati muafaka wa kupembua kwa kina na mapana: fursa, changamoto na vikwazo vilivyopo katika mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Russia. Ni wakati wa kujenga na kuimarisha mahusiano haya kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa upande wake, Bwana Sergiey Lavrov, Waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa nchini Russia anasema, kuna mambo ambayo Vatican na Russia wana msimamo wa pamoja au ule unaokaribiana hasa kuhusiana na changamoto katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Bwana Sergiey Lavrov anasema: umuhimu wa kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu ni changamoto inayovaliwa njuga kati ya Vatican na Russia. Kwa pamoja wamekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha haki jamii kati ya watu wa Mataifa bila kusahau tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Kwa sasa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Russia unaendelea “kuimarika zaidi”. Itakumbukwa kwamba, hii ni ziara ya kwanza kabisa kutekelezwa na Katibu mkuu wa Vatican katika karne hii, kumbe ziara ya Kardinali Parolin nchini Russia ni tukio la kihistoria linalopania kuacha alama ya kudumu katika mahusiano ya kidiplomasia baina ya pande hizi mbili.

Ni matumaini ya Vatican kwamba, Russia inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa suluhu ya kudumu ya mgogoro wa kisiasa na machafuko ya kijamii nchini Venezuela. Hii inatokana na ukweli kwamba, Russia ina uhusiano mzuri wa kidiplomasia na Venezuela na kwa njia hii inaweza kusaidia kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; mambo ambayo anasema Kardinali Parolin ni muhimu sana katika kurejesha tena amani, usalama na utulivu nchini Venezuela ambayo kwa sasa inaendelea kutumbukia katika ombwe kubwa la ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula na dawa kwa watu wake, kiasi kwamba, maelfu ya watu kwa sasa wanalazimika kuikimbia nchi yao ili kutafuta: hifadhi na usalama wa maisha yao.

Katika ziara yake ya kikazi nchini Russia, Kardinali Pietro Parolin, Jumanne, tarehe 22 Agosti 2017 amekutana na kuzungumza na Patriaki Cyril wa Moscow na Russia nzima. Jumatatu, tarehe 21 Agosti 2017, Askofu mkuu Ilarione Volokolamsk, Rais wa Idara ya uhusiano na ushirikiano wa Kimataifa wa Kanisa la Kiorthodox la Russia alikutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, ambaye alikuwa ameambatana na Askofu mkuu Celestino Migliore, Balozi wa Vatican nchini Russia pamoja na maafisa wa Ubalozi wa Vatican nchini humo. Viongozi hawa wawili wamejadili pamoja na mambo mengine, kuhusu uekumene wa damu unaoshuhudiwa na Wakristo huko Mashariki ya Kati.

Wamekubaliana kimsingi kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe ili kupambana na hatimaye, kung’oa kabisa vikundi vya kigaidi huko Siria, vinavyoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao na kwamba, huu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na kashfa kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Makanisa haya mawili yaendelee kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya uekumene wa huduma, kwa wakimbizi, wahamiaji na waathirika wa vita na ghasia huko Mashariki ya Kati. Mateso na mahangaiko ya wananchi wa Ukraine; shida na changamoto za Wagriki Wakatoliki huko Ukraine zimejadiliwa kwa kina na mapana!

Kardinali Pietro Parolin anasema, Vatican inasubiri kwa hamu suluhu ya kudumu katika mgogoro huu ambao unaendelea kusababisha mateso na mahahaiko makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia. Kanisa Katoliki litaendelea kujikita katika majadiliano ya kiekumene, kama nafasi muafaka kwa waamini wa Makanisa mbali mbali kuweza kufahamiana, kuheshimiana na kushirikiana katika maisha na utume wa Kanisa, ili kuweza kutoa ushuhuda wa pamoja kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. Anatambua vikwazo na changamoto zilizopo, lakini, nia njema iliyooneshwa na viongozi wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Russia nzima inatia matumaini makubwa.

Askofu mkuu Ilarione Volokolamsk kwa upande wake amekazia umuhimu wa utekelezaji wa Tamko la Havana, Cuba, lililotiwa sahihi kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Cyril wa Moscow na Russia nzima kunako mwaka 2016. Hizi ni sera na mikakati inayofumbatwa katika tunu msingi za kiinjili zinazopania kukuza na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Kardinali Pietro Parolin, Jumatatu, tarehe 21 Agosti 2017 amekutana na Maaskofu mahalia pamoja na kuadhimisha nao Ibada ya Misa Takatifu. Ametumia fursa hii kuwasilisha salam na matashi mema ya Baba Mtakatifu Francisko kwa familia ya Mungu nchini Russia.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Paolo Pezzi wa Kanisa kuu la Bikira Maria Mama wa Mungu, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa salam na matashi mema sanjari na uwepo wa Kardinali Pietro Parolin, kama alama ya uwepo endelevu wa Mwenyezi mungu anayetaka kuwaimarisha watoto wake katika imani, matumaini na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.