2017-08-21 09:27:00

Rais Sergio Mattarella: wekezeni kwa vijana katika elimu na ajira


Bwana Emilia Guarnieri Rais wa “Mfuko wa Mkutano wa Urafiki Kati ya Watu nchini Italia” katika hotuba yake kwa wajumbe wanaoshiriki katika mkutano huu ambao umefunguliwa, Jumapili tarehe 20 Agosti 2017, kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Francesco Lambiasi wa Jimbo Katoliki Rimini, nchini Italia kama sehemu ya maadhimisho ya Mkutano wa Urafiki kati ya Watu nchini Italia amekazia kuhusu umuhimu wa ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wajumbe hao pamoja na ujumbe uliotolewa na Rais Sergio Mattarella wa Italia.

Viongozi hawa kwa pamoja wametoa changamoto endelevu kwa wajumbe kuangalia vinasaba asilia vya mkutano huu unao wawezesha kukuza na kudumisha majadiliano kwa kuthamini na kuendeleza kile ambacho ni: haki, chema na kizuri kati ya watu wa Mataifa, kama njia ya kutambua nyayo za uwepo wa Mwenyezi Mungu katika historia ya maisha ya mwanadamu! Rais Sergio Mattarella amekazia kwa namna ya pekee kabisa, umuhimu wa wanasiasa, taasisi, watunga sheria, wachumi na wanajamii kushirikiana na kushikamana katika kukabiliana na changamoto mamboleo zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Anasema, hii ni changamoto petu na changamani katika maisha ya watu, inayohitaji ushirikiano wa dhati ili kupata suluhu yake. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kupewa msukumo wa pekee ili kutumia mabadiliko makubwa yanayojitokeza mbele yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kutambua kwamba, wanapaswa kushiriki kikamilifu kwani hata wao ni sehemu ya jamii ya watu wanaowazunguka. Vijana wajengewe uwezo kwa njia ya elimu makini na endelevu; kwa kuwapatia haki na fursa za kazi; kiini msingi cha uhuru wa watu ndani ya jamii.

Rais Sergio Mattarella anaendelea kusema, kwa kuwekeza katika ustawi na maendeleo ya jamii kwa siku za usoni, watu wanakuwa na imani na matumaini ya kuweza kutumia vyema rasilimali walizo nazo kwa ajili ya kujiletea maendeleo endelevu: kiroho na kimwili. Ni wajibu wa wale wote  wanaohusika katika mchakato wa kuwarithisha vijana amana na utajiri wa maisha na historia yao kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana hii kwa ukamilifu, ili kuwawezesha vijana wa kizazi kipya kuwa ni wadau makini katika mchakato wa ujenzi wa jamii yao.

Ulimwengu mamboleo kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia umegeuka kuwa kama kijiji; na kwamba, unakabiliwa na mwendo kasi wa mabadiliko ambayo yanaacha athari zake katika maisha ya watu. Utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia yana faida na hasara zake hasa katika uhuru na utawala wa mtu binafsi. Haya ni mambo ambayo yanahitaji kuboreshwa kila wakati kwa kuzingatia dhana ya Jumuiya katika mchakato wa kuleta mabadiliko. Kutokana na changamoto hii anasema Rais Sergio Mattarella wa Italia kuna haja kwa vijana wa kizazi kipya kuwa ni wadau wa mabadiliko yanayojitokeza ulimwenguni kwa wakati huu. Mkutano huu unahudhuriwa na viongozi wa ngazi ya juu kutoka Umoja wa Mataifa, Jumuiya za Kimataifa pamoja na Serikali ya Italia katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.