2017-08-16 14:49:00

Umoja wa Mataifa: Kenya zingatieni haki msingi za binadamu!


Bwana Zeid Ra’ad Al Hussein Zeid Kamishina wa haki msingi za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa amesifia uchaguzi mkuu wa Kenya jinsi ulivyofanyika kwa amani na utulivu hapo tarehe 8 Agosti 2017, lakini baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutangazwa hali imebadilika kabisa kiasi cha chuki za kikabila na kimajimbo kuanza kuibuka kwa kasi kubwa na hivyo kusababisha baadhi ya wananchi kupoteza maisha pamoja na mali zao kuporwa na kuharibiwa vibaya kutokana na chuki zilizoibuliwa baada ya uchaguzi mkuu. Vyombo vya ulinzi na usalama pia vimeshutumiwa kwa kutumia nguvu kubwa kupambana na makundi ya waandamanaji. Sasa ni dhamana na wajibu wa viongozi wa kisiasa kutuliza machafuko na mipasuko hii ya kisiasa kwa kujikita katika sheria na kanuni za nchi badala ya watu kuamua kujichukulia sheria mkononi.

Bwana Zeid Ra’ad Al Hussein Zeid anasema, watu wanayo haki ya kukutana na kufanya maandamano ya amani kwa kuzingatia sheria za nchi na kwamba, Serikali inawajibu wa kuhakikisha kwamba, raia wanatekeleza yote haya kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kipaumbele cha kwanza kwa wakati huu nchini Kenya ni majadiliano katika ukweli na wazi na wala si ghasia, fujo na vurugu, kwani madhara yake ni makubwa mno kwa wananchi wote wa Kenya.

Maandamano yasiwe ni chanzo cha ghasia, vurugu na uvunjifu wa sheria na kwamba, wanasiasa wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, amani inarejeshwa tena nchini Kenya. Mashirika ya Kiraia na waandishi wa habari wanapaswa kutekeleza kazi zao bila kuingiliwa na Serikali anasema, Kamishina wa haki msingi za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa. Taarifa zinaonesha kwamba, hadi kufikia Jumatano tarehe 16 Agosti 2017 watu 17 wamekwisha kufariki dunia na wengine 177 kujeruhiwa vibaya kutokana na mapambano na vyombo vya ulinzi na usalama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.