2017-08-15 14:38:00

Yesu Kristo ni zawadi ya neema, chemchemi ya furaha, amani na utulivu


Katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, Mama Kanisa anaweka mbele ya watoto wake Injili inayomwonesha Bikira Maria akipashwa habari na Malaika Gabrieli kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu na baada ya tukio hili akaondoka kwa haraka kwenda mpaka mji mmoja wa Yuda ili kumsaidia binadamu yake Elizabeth aliyekuwa ni mjamzito na anakaribia kujifungua. Alipowasili, Elizabeth akamsalimia kwa salam ambayo imegeuka kuwa ni Sala kwa Bikira Maria “Umebarikiwa wewe katika wanawake wote, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa”.  

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko Jumanne, tarehe 15 Agosti 2017 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Kanisa linapoadhimisha Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni, mwili na roho! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Bikira Maria ndani mwake, alikuwa amebeba zawadi kubwa sana kwa ajili ya Elizabeth na ulimwengu katika ujumla wake. Kwa njia ya Bikira Maria, Neno wa Mungu alifanyika mwili na kukaa kwake, akawa ni Tabernakulo ya kwanza kabisa ya Neno wa Mungu, ili aweze kutekeleza dhamana na utume wake kwa ajili ya wokovu wa walimwengu!

Uwepo wa Bikira Maria katika familia ya Elizabeti na mumewe Zakaria, ukawa ni chemchemi ya furaha, kwani walikuwa wanatarajia kuzaliwa kwa mtoto ambaye atakuwa ni mkuu na ambaye ataitwa Yohane Mbatizaji; mtangulizi wa Masiha, atakayemwandalia mapito!  Uwepo wa Yesu kati yao unaotoa maana halisi ya maisha, familia na wokovu wa watu wa Mungu, kiasi hata cha Bikira Maria kusimama na kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa sababu amemtendea mambo makuu na jina lake ni takatifu kwani amewakweza wanyonge na wale wasiofahamika duniani kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria mwenyewe, Mtakatifu Yosefu mchumba wake na hata kijiji cha Nazareti, kilikuwa hakifahamiki na wengi.

Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria anatumia fursa hii kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wake wa “Magnificat” kuelezea sifa za Mwenyezi Mungu ambaye daima ni mwenye huruma na mwaminifu; anayetekeleza mpango wake wa ukombozi kwa kuwashirikisha maskini na wanyonge, wanaomwamini na kutumainia Neno lake kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria na Elizabeti anamwambia Bikira Maria heri kwake kwani amesadiki yale aliyoambiwa na Bwana. Nyumba hii, ikageuka kuwa ni nyumba ya furaha, umoja wa kidugu; chemchemi ya imani inayofumbatwa katika matumaini, sala na masifu!

Baba Mtakatifu anasema, haya ndiyo matamanio yake kwa ajili ya familia zote za waamini na watu wote wenye mapenzi mema, Kanisa linapoadhimisha Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni, ili aweze kuzisaidia familia, jumuiya za waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kupata zawadi ya neema ambayo ni Kristo Yesu. Bikira Maria kwa kumbeba Mtoto Yesu tumboni mwake, ameweza pia kuwakirimia waamini furaha mpya na timilifu na ambayo imesheheni maana nyingi: anawasaidia waamini kuweza kuvuka shida, magumu na changamoto za maisha kwa njia ya imani thabiti! Anawakirimia waamini uwezo wa kuambata huruma, ili kusamehe; kuelewa na kusaidiana. Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha fadhila na imani. Kwa kumtafakari Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha maisha yake hapa duniani; iwe ni fursa ya kumshukuru kwani anawatangulia katika hija ya maisha na imani. Waamini wamwombe Bikira Maria ili aweze kuwalinda na kuwatunza, ili hatimaye, waweze kuwa na imani thabiti; furaha na huruma; awasaidie kuchuchumilia utakatifu, ili siku moja waweze kukutana mbinguni kwa Baba wa milele!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.