2017-08-09 13:23:00

Usiposhikamana na Kristo Yesu, utazama kama jiwe majini!


Mungu katika kazi yake ya uumbaji ameviweka vitu vyote katika maelewano na ulinganifu. Amani, utulivu na uelewano katika jamii na mazingira yanayozunguka ni ishara ya uwepo wa Mungu kwani uwepo wake huviunganisha vitu vyote pamoja na kuvushirikisha utendaji wake au kuvipatia nafasi yake stahiki kwa ajili ya kuimarishana vyote kwa pamoja. Kinyume chake ni mahali panapokosa utulivu. Hii ni ishara ya kutkuwepo kwa muunganiko na ushirikiano baina ya vitu, watu au matukio yaliyopo. Mahali panapokosekana Mungu panakosa amani na utulivu.

Injili ya Dominika hii inatuonesha hali hizi zote mbili. Kwanza tunaiona hali ya vurugu, mawimbi na taabu wanayokumbana nayo mitume. Mitume wanapatwa na hali hii pale Kristo anapokuwa mbali nao. Lakini Kristo anapowakaribia hali inatulia. Kristo aliye Mungu kweli na mtu kweli anarejesha tena uwepo wa Mung kati yao, upepo na dhoruba yote vinakoma. Nabii Eliya anaitambua hali hiyo inayoletwa na Mungu. Aina ya upepo ambayo ilikuwa ni ya vurugu haikumfanya kuinuka lakini aliposikia “sauti ndogo ya utulivu… alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango”.

Jambo jingine tunaloliona katika Injili ni uhaba wa imani. Kwanza kwa mitume wote kwa pamoja. Walisema: “ni kivuli, wakapiga yowe kwa hofu”. Kinyume na Nabii Eliya Mitume wanashindwa kutambua uhusiano kati ya uwepo wa Mungu na utulivu au Amani. Hawa wanawakilisha jamii ya wanadamu ambao wanasongwa na kelele na misukosuko ya dunia hii kiasi cha kushindwa kuzitambua fursa chache za neema zinazomleta Kristo katikati yetu. Fursa hizi ni huduma za kikanisa katika Neno lake na Masakramenti. Fursa hizi zinauleta uwepo wa Kristo na hivyo kuwa jawabu kwa changamoto mbalimbali za kijamii. Tunaendelea kupiga yowe kwa hofu badala ya kumkimbilia Yeye anayejifunua kwetu kwa fumbo la Kanisa.

Pili ni kwa Petro ambaye pamoja na kuhakikishiwa na Kristo kuwa ni Yeye alianza kuona mashaka. Mashaka yake yalichagizwa na upepo uliokuwa unaendelea kuvuma, akaacha kumtazama Kristo, akaacha kumsikiliza Kristo na hivyo akaanza kuzama. Alipoacha kuwa mtii kwa uwepo wa Kristo na kuanza kujichanganya na yanayomzunguka ndipo alipoanza kuanguka. Hawa ndiyo wale ambao wanaonekana kumfuata Kristo lakini bado wanashindwa kujiondoa katika fujo kelele na vurugu za ulimwengu huu. Kristo ndiye utimilifu wa ufunuo wa Mungu kwetu. Tukibaki tunamkazia macho Yeye katika ukweli juu ya maisha yake hapa duniani tutapata njia ya kuufanya ulimwengu huu kuendelea kuwa bora zaidi na kuuepusha na fujo au vitisho vya aina yoyote.

Mungu hapatikani katika makelele, fujo na vurugu. Hii inamaanisha uwepo wa Mungu huleta utulivu na uelewano. Mungu huleta muunganiko na kila kitu kitaenenda kadiri ya mpango wa Mungu. Tunaposhuhudia dhoruba mbalimbali za kidunia ni udhihirisho wa kukosekana kwa mwenyezi Mungu. Dunia mamboleo ambayo haimpatii Mungu nafasi ni kitalu kizuri cha kuleta vurugu na fujo nyingi. Dunia ya leo ambayo imejiloweka katika huria ya kimaadili ni sababu ya kuwachanganya wanadamu. Kila mmoja anajiona yu mmiliki wa ukweli na matokeo yake tunaziona sura mbalimbali za ukweli kuhusu kitu kimoja. Hakika ni mchanganyiko na vurugu kubwa.

Tunaweza kukiona kizazi cha wakati huu katika namna mbalimbali kwa jinsi kinavyoathiriwa na kelele na usumbufu mwingi wa dunia hii kiasi cha kushindwa kumwona Mungu. Mfano rahisi ni jinsi ambavyo tunakurupusha ibada zetu. Wangapi ambao huja katika ibada huku wamesongwa na fujo na hekaheka za dunia? Mara ngapi tunashuhudia watu wanaingia katika ibada ama wanaendeleza maongezi yao hata mbele za Mungu au wanaingia wakiwa na simu zao za mikononi zikingojea mpango fulani mahsusi? Kwa hakika katika hali hii ya fujo na tunapozidi kuvutwa na hali hizi tunazidi kuweka Mungu mbali na kuzikosa baraka na neema zake.

Wakati mwingine ndani ya mtu binafsi kunakuwa na fujo za kiroho. Watu wengi wanakosa nafasi za ukimya na kumtafakari Mungu kwamba ni nani kwao na ni ipi nafasi yake katika maisha ya kila siku. Akili zinakuwa hazijatulia na zinasongwa na mawazo mengi yanayozidi kumsukumizia Mungu pembeni. Wengi hawapo tayari kutafuta nafasi za mafungo au tafakari binafsi ili kuisikiliza sauti ya Mungu. Wengi wawapo nyumbani hawana fursa za kufanya mazungumzo na Mungu kwa njia ya sala. Hali kama hii inamuondoa Mungu na kwa hakika tutaendelea kuzama katikati ya bahari yenye upepo mkali na wa kutisha wa vituko vya dunia hii.

Kuwa na imani kwa Mungu kunajidhihirisha katika kujikabidhisha yote kwa Mungu. Utegemezi kwa Mungu unapaswa kuwa ni wa asilimia mia moja. Si suala la kuwa na mchanyato. Haupaswi kuwa vuguvugu. Mmoja anapojikabidhi kwa Mungu mzima mzima ndipo ataweza kuisikia sauti yake na atakuja na kukaa kwake. Huu ni mwanzo mpya wa kuwa na utulivu wa kiroho na kimwili. Ni mwaliko kwetu kuimarisha imani yetu na kumpokea Mwenyezi Mungu katika ukuu wake jinsi alivyo. Ni fursa ya kujifunza hulka yake ili kwa kumfahamu vema imani yetu iimarike na kuzidi kuungana naye. Tutazidi kumwelewa kwa kupitia ufunuo wake na kwa namna ya pekee kupitia Neno lake ambalo linakamilishwa katika nafsi ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Hivyo, tukaze macho yetu na kumwelekea Kristo bila hofu kwani kwake tutachota amani na utulivu. Kwake yeye tutaendelea kuungana na Mungu na hivyo kuviweka vitu vyote katika amani, utulivu na uelewano. Mtume Paulo anatuonya kutokuingia katika kosa la Wayahudi ambao pamoja na kwamba ufunuo wa Mungu ulipitia kwao na Kristo akazaliwa kutoka katika jamii yao lakini bado walimpinga. Mtume Paulo anamtamka Kristo kama “aliye juu ya mambo yote, Mungu mwenye kuhimidiwa milele”. Kwa sababu hiyo tujitahidi kuwa na yeye kwani ndiye njia pekee ya wokovu. Yeye ndiye anayetuunganisha kweli na Mungu. Pale tutakapoanza kuangalia pembeni, yaani asili yangu, uwezo wangu, tamaduni zangu, nafasi yangu ya kijamii na kumweka pembeni tutakumbana na hofu na vitisho na mwisho tutaanza kuzama mithili ya mtume Petro.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.