2017-08-08 14:15:00

Utume na maisha ya Kanisa ni wajibu wa waamini wote!


Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Msimamizi wa Maparoko duniani,  kwa muda wa miaka 40 alijisadaka kwa ajili ya kuwahudumia watu wake kwa Neno, Sakramenti za Kanisa na huduma ya upendo; akajitakatifuza mwenyewe kwa njia ya: tafakari ya Neno la Mungu, sala, toba na wongofu wa ndani uliofumbatwa katika maisha ya unyenyekevu. Aliwaongoza watu wa Mungu katika hija ya maisha, kuelekea kwenye furaha ya maisha ya uzima wa milele.

Naye Paolina Maria Jaricot, alikuwa ni mwamini mlei, lakini mwanamke wa shoka aliyejisadaka maisha yake, kiasi kwamba, yakawa ni chachu ya utakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Mtakatifu Yohane Maria Vianney na Paolina Maria Jaricot walikuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; wakajitosa kimasomaso kwa ajili ya Injili ya Kristo na wokovu wa watu wa Mungu. Hawa ni mfano bora wa maisha ya sala na ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Haya yamesemwa hivi karibuni na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu wakati wa kongamano la kufunga Mwaka wa Utume wa Kanisa Jimbo Katoliki Belley Ars, nchini Ufaransa. Anasema, hawa ni watoto wa Mungu kutoka Ufaransa, waliosaidia kwa kiasi kikubwa kuleta upyaisho wa maisha ya kiroho ndani ya Kanisa. Upendo wao wa dhati kwa Kristo Yesu, Bikira Maria na Kanisa, uliwahamasisha kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kulipyaisha Kanisa lililokuwa limekwaruzwa kutokana na Mapinduzi ya Ufaransa, likabaki na madonda makubwa ya uchungu ndani mwake!

Mtakatifu Yohane Maria Vianney alipyaisha maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya huduma makini kwenye Parokia yake; akasoma alama za nyakati, akasimama kidete kujibu kilio na matamanio halali ya watu wake: kiroho na kimwili: Kiroho, akahakikisha kwamba, anawapatia tafakari ya kina ya Neno la Mungu, lililogeuka kuwa ni taa na dira ya kuyaongoza maisha yao; akawaonesha kisima cha huruma na upendo wa Mungu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho! Waamini wakaboresha maisha yao kwa njia ya sala iliyofumbatwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; maskini, yatima na wajane wakipewa kipaumbele cha kwanza!

Kwa upande wake, Paolina Maria Jaricot, alijisikia ndani mwake, ile hamu ya kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kwa ajili ya kuwatangazia watu furaha ya Injili; akasaidia kukusanya rasilimali fedha kwa ajili ya utume wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Alishirikiana na watu mbali mbali ili kufanya toba kwa ajili ya wongofu wa ndani kwa wale ambao bado walikuwa hawajamwini bado Mwenyezi Mungu. Alikuwa ni chombo cha upendo na mshikamano kati ya waamini wa Jimbo Katoliki la Lione, waliohusishwa kwa karibu zaidi katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu, akawa ni mfano bora wa huduma kwa Kanisa na wamissionari waliokuwa wanajisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa.

Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu anasema, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walileta mageuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia kiasi kwamba, chachu ya uinjilishaji ikapewa mwelekeo mpana zaidi, kuliko ilivyokuwa hapo awali. Paolina Maria Jaricot akawa ni shuhuda wa mshikamano wa kimissionari, dhamana iliyokuwa inatekelezwa na Kanisa kwa wakati huo. Kimsingi, wote wawili wakawa ni baraka na chemchemi ya neema kwa Kanisa la Kristo kutokana ushuhuda wao wenye mvuto na mashiko!

Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kunako mwaka 1622 likaanzishwa na Papa Gregori XV ili kusaidia mchakato wa uinjilishaji kati ya watu wa Mataifa. Hiki ni kipindi ambacho miito kwa ajili ya Mapadre wa Jimbo ilikuwa inaongezeka na hivyo wamissionari wakalazimika kuwaachia nafasi Mapadre wa Majimbo na wao kuelekea kwenye nchi za kimissionari, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa!

Hapa anasema Kardinali Filoni, dhamana ya maisha na utume wa Kanisa ikaendelea kuwa na mwelekeo mpana zaidi, kiasi hata cha kuwahusisha waamini walei, ili kuchangia kwa hali na mali, ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa zima. Kila mtu alikuwa na jambo la kutoa na kupokea kutoka kwa jirani zake ndani ya Kanisa. Huu ni utume ambao unapata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, ambayo inawashirikisha Wakristo wote: Unabii, Ufalme na Ukuhani wa Kristo. Huu ni mchakato unaopaswa kuendelezwa hasa wakati huu katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo ambayo bado kuna changamoto kubwa ya uinjilishaji mpya sanjari na mwendelezo wa utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Kristo kwa wale ambao bado hawajabahatika kuisikia ikitangazwa na kushuhudiwa miongoni mwao.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wa “Lumen Gentium” yaani “Fumbo la Kanisa” wanasema, kimsingi Kanisa lina tabia ya kimissionari, kwani limeitwa na kutumwa ulimwenguni kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu: kwa kuwahubiri na kuwavuta watu waweze kukiri imani, huwaandaa kwa Sakramenti ya Ubatizo: hujitahidi kukuza na kudumisha mchakato wa utamadunisho, Hivyo, Kanisa husali na kutenda kazi pia ili ukamilifu wa ulimwengu wote uingizwe katika Taifa la Mungu, Mwili wa Fumbo la Kristo yaani Kanisa na Hekalu la Roho Mtakatifu, ili heshima, utukufu, sifa na ukuu viweze kutolewa kwa Mwenyezi Mungu.

Leo hii, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kusoma alama za nyakati, ili kuendelea kupyaisha sera na mikakati ya utangazaji na ushuhuda wa furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa; kwa kuboresha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kama anavyobainisha kwenye Waraka wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” ambamo kwa ufupi kabisa anasema, Kanisa lipo kwa ajili ya utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kanisa lipo kati pamoja na watu wa Mungu, mwelekeo wa kuwa na utambuzi mpya wa uelewa wa Kanisa, ili kuishi kama sehemu ya Jumuiya ya Kristo inayotumwa kuinjilisha na kuinjilishwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.