2017-08-07 10:16:00

Papa Francisko: sanaa na utunzaji bora wa mazingira!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa ajili ya nia zake za jumla kwa mwezi Agosti, 2017 zinazosambazwa na Utume wa Sala, anaelekeza mawazo yake kwa wasanii, wanaoonesha ule uzuri wa imani sanjari na kutangaza Injili na ukuu wa Mungu katika kazi ya uumbaji. Pale mwanadamu anapopigwa bumbuwazi na kushangaa juu ya kazi ya Uumbaji, anatambua jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake na kuwashirikisha upendo wake usiokuwa na mipaka.

Kipindi hiki cha kiangazi, ni wakati muafaka kwa watu kujipatia muda wa kujipumzisha, ili kuweza kujichotea nguvu ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Iwe ni fursa kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufurahia uzuri wa kazi ya uumbaji, kama uzoefu wa imani unaotangaza ukuu wa Mungu. Ujumbe huu wa Baba Mtakatifu umetafsiriwa katika lugha nane za kimataifa na unasindikizwa kwa muziki mwanana, unaowashirikisha wasanii kutoka katika tamaduni, lugha, jamaa na dini mbali mbali duniani. Wasanii ndio wanaobeba uzito wa hali ya juu katika ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa njia ya video kwa mwezi huu wa Agosti, 2017.

Wasanii ni hazina muhimu sana inayohifadhi kazi ya uumbaji; wanayo dhamana ya kutibu na kuganga madonda yaliyomo ndani ya moyo wa binadamu na hivyo kumkirimia tena: imani na matumaini; hasa kwa wale wanaoishi katika mazingira magumu; hawa ndio kwa namna ya pekee kabisa, walengwa wa nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa mwezi Agosti, ili kwa njia ya kazi ya wasanii, watu hawa waweze kutambua uzuri wa kazi ya uumbaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.