2017-08-05 17:36:00

Watu wana kiu ya amani duniani!


Amani ya kudumu ni kielelezo makini cha maendeleo endelevu ya binadamu na kwamba, wanasiasa hawana budi kujenga na kudumisha mtindo wa siasa unaojikita katika amani badala ya kuendekeza vita, ghasia, chuki na mipasuko ya kijamii. Hapa kuna haja ya kusimama kidete, kulinda, kudumisha na kuendeleza utu na heshima ya binadamu; daima kwa kutambua kwamba, wafuasi wa Kristo wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani duniani.

Upendo wa kweli ni chachu inayoweza kudhibiti ghasia na machafuko kwani ndani ya familia kama alivyowahi kusema Mama Theresa wa Calcutta, watu hawana haja na mabomu wala bunduki zinazoharibu amani na mafungamano ya watu ndani ya jamii; watu wanataka kuonjeshwa amani, upendo na mshikamano wa dhati kama ndugu. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, linasema kwamba, Kanisa lilitambua udhaifu wake wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, lakini sasa linataka kujizatiti zaidi katika kutangaza na kushuhudia Injili ya amani, haki na upendo kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan kwa ajili ya kuadhimisha Siku kumi ambazo zimetengwa na Kanisa Katoliki nchini Japan kwa ajili ya kuombea amani duniani na kilele chake ni tarehe 6 Agosti 2017, Jumuiya ya Kimataifa inapokumbuka siku ile mji wa Hiroshima ulipoharibiwa kwa mabomu ya nyuklia. Tangu wakati huo, bado madhara yake yanaonekana miongoni mwa wananchi wa Japan. Amani ni kati ya mambo muhimu sana yanayotiliwa mkazo na Katiba ya Japan iliyochapishwa miaka sabini iliyopita.

Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linapenda kuihamasisha Serikali kujikita zaidi katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi ili kushughulia misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya nchi zilizoko Kaskazini Mashariki mwa Asia pamoja na ulimwengu katika ujumla wake. Vita, ghasia pamoja na vitendo vya kigaidi ni hatari sana kwa mafungamano ya kijamii. Japan inahitaji kuwa na kiasi katika masuala ya ulinzi na usalama, ili kudumisha amani na maridhiano kati ya watu!

Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linakaza kusema, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani ni fursa ya kukuza na kudumisha uekumene wa damu na huduma; sala na maisha ya kiroho. Tarehe 23 Novemba 2017, Baraza la Maaskofu Katoliki Japan litaungana na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri nchini Japani kwa ajili ya kuadhimisha kumbu kumbu ya mauaji ya kikatili ya Wakristo yaliyotokea huko, Urakami, mjini Nagasaki. Itakuwa ni siku ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene yanayopania kuleta mwamko mpya wa mahusiano miongoni mwa Wakristo kwa kuondoa uhasama na uadui kati yao na kuanza kujikita katika toba, msamaha na upatanisho, ili kweli Wakristo nchini Japan waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani duniani.

Baraza la Maaskofu Katoliki Japan limeanza maandalizi ya Jubilei ya Miaka 150 ya Madhulumu ya Wakristo Urakami Yoban Kuzure na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2018. Damu ya mashuhuda hawa wa Injili imekuwa ni mbegu ya ukomavu wa Ukristo nchini Japan. Wamekuwa kweli ni mashuhuda wa uhuru wa dhamiri, kiasi hata cha kukubali kukabiliana na kifo uso kwa uso. Japani inawakumbuka watoto wake milioni 20 waliopoteza maisha kutokana na vita, bila kuwasahau raia wa nchi jirani. Ni wajibu wa familia ya Mungu nchini Japan kuhakikisha kwamba, inajikita katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu; utu na heshima yake bila kusahau uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Athari za vita zimeacha kurasa chungu nchini Japan, kumbe, wananchi wengi hawataki kuona tena Japan ikijiingiza katika vita na ghasia.

Japana inapaswa pia kuwa mstari wa mbele katika masuala ya kimataifa: kwa ajili ya ulinzi na usalama dhidi ya vitendo vya kigaidi; haki na amani sehemu mbali mbali za dunia; huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji; mapambano dhidi ya umaskini, uharibifu wa mazingira nyumba ya wote; biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo sanjari na huduma makini kwa watoto, wazee na maskini. Baraza la Maaskofu Japan bado linaguswa na madhara makubwa ya uharibifu wa mazingira yaliyotokana na kuvuja kwa mtambo wa nyuklia wa Fukishima “TEPCO Fukushima Daiichi Nuclear Power Plant”. Zote hizi ni changamoto za ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki na amani. Maneno na ushuhuda wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu ushuhuda wa Injili ya amani, yawe ni dira na mwongozo katika maisha na utume wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.