2017-08-05 14:57:00

Msimamo wa Vatican kuhusu machafuko ya kisiasa nchini Venezuela


Ili kuweza kukabiliana kikamilifu na machafuko ya kisiasa nchini Venezuela yanayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao; sanjari na ujenzi wa umoja, mshikamano na mafungamano ya kitaifa, kuna haja kwa pande zote zinazohusika kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimu na kuthamini haki msingi za binadamu sanjari na uhuru wa watu kujieleza. Haya ni kati ya mambo muhimu yanayopewa kipaumbele cha pekee na Sekretarieti kuu ya Vatican kuhusiana na machafuko ya kisiasa nchini Venezuela.

Vatican inasikitishwa  sana na mchafuko haya ya kisiasa ambayo yanaendelea kusababisha vifo vya watu wasiokuwa na hatia; baadhi ya raia kufungwa au kuzuiwa kizuizini pamoja na ongezeko kubwa la watu wanaojeruhiwa kutokana na mapambano kati ya raia na vyombo vya ulinzi na usalama. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufuatilia kwa ukaribu sana hali ya machafuko ya kisiasa nchini Venezuela na athari zake katika masuala ya: kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiutu na kiroho.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wananchi wote wa Venezuela uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema sehemu mbali mbali za dunia, kuunganika pamoja naye kwa ajili ya kusali ili kuombea amani, usalama na maridhiano nchini Venezuela. Vatican inawataka wadau, lakini hasa zaidi Serikali kuhakikisha kwamba haki msingi za binadamu, uhuru wa kujieleza na Katiba ya nchi inaheshimiwa na kutekelezwa kikamilifu.

Zoezi la sasa la kutaka kubadili katiba, kwa busara ya kawaida lingesitishwa, ili kusaidia kudumisha mchakato wa upatanisho, haki na amani, badala ya kuendelea kukuza kinzani, ghasia na machafuko ya kisiasa. Wadau waunde mazingira yatakayosaidia kupata suluhu ya machafuko haya kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi mintarafu mwongozo uliotolewa na Vatican tarehe 1 Desemba 2016. Wahusika wanapaswa kuzingatia hali tete ambayo wananchi wanakabiliana nayo kwa wakati huu. Baa la njaa linaanza kuwanyemelea sana wananchi wa Venezuela ambao kwa sasa wanakabiliwa pia na uhaba mkubwa wa dawa pamoja na ukosefu wa ulinzi na usalama.

Mwishoni, Vatican inapenda kuialika familia ya Mungu nchini Venezuela kuachana na tabia ya ghasia na vurugu; kwa kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwa makini wakati wa kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa raia. Wasitumie nguvu kupita kiasi dhidi ya raia kwani mwelekeo wa namna hii unajenga uhasama kati ya vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.