2017-08-04 15:18:00

Mtakatifu Yohane Maria Vianney ni "Jembe" la nguvu katika utume!


Mama Kanisa, tarehe 4 Agosti anaadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane Maria Vianeney, Msimamizi wa Maparoko duniani, ambaye kwa muda wa miaka 40 alijisadaka kwa ajili ya kuwahudumia watu wake kwa Neno na Sakramenti za Kanisa; akajitakatifuza kwa sala, toba na wongofu wa ndani uliofumbatwa katika maisha ya unyenyekevu. Aliwaongoza watu wa Mungu katika hija ya maisha, kuelekea kwenye furaha ya uzima wa milele. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu wakati wa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa huko Ars, nchini Ufaransa, tarehe 4 Agosti 2017.

Kardinali Filoni, ametumia nafasi hii kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Majandokasisi pamoja na Wakleri wote wanaotoka katika Makanisa machanga sehemu mbali mbali za dunia, ili kwa maombezi ya Mtakatifu Yohane Maria Vianney, waweze kuwa waaminifu na wadumifu katika maisha na wito wao wa Kipadre. Mtakatifu Yohane Maria Vianney alikuwa anatoka kwenye familia maskini, akakulia katika mazingira magumu baada ya Mapinduzi ya Ufaransa; hakuwa na uwezo mkubwa sana darasani, lakini alibahatika kuwapata walezi waliomsaidia kukamilisha ndoto ya maisha na wito wake wa Kipadre, kiasi cha kujisikia kuwa ni Padre kati ya watu wake na Mkristo kati yao.

Kama Padre, Yohane Maria Vianney alijitahidi kuzama katika utakatifu wa maisha kwa njia ya ufukara, utii na usafi kamili; mambo yaliyomsaidia katika maisha yake kwa kipindi cha miaka 73. Alijitahidi kufuata njia ya utakatifu wa maisha, waamini wakatambua ndani mwake ushuhuda wa maisha yaliyojikita katika maneno na matendo; yakawa na mavuto na mashiko kwa watu wake. Wadhambi wakakimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, Padre Yohane Maria Vianney akawepo kwenye Kiti cha huruma ya Mungu, kila wakati walipohitaji kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao.

Ni Padre aliyejenga urafiki wa dhati na Kristo Yesu, mwenye moyo mpole na mnyenyekevu; ukawa ni dira na mwongozo wa maisha na wito wake wa Kipadre kwa muda wa miaka 40. Alionesha Ibada kwa Bikira Maria, akawa ni chombo cha ukarimu na upendo kwa watu wa Mungu. Katika kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 150 tangu alipofariki dunia, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alisikika akisema, Mtakatifu Yohane Maria Vianney ni mfano bora wa kuigwa na Mapadre wote duniani katika maisha, wito, ari na moyo wa utekelezaji wa shughuli zake za kichungaji miongoni mwa watu wa Mungu.

Hii ni changamoto kwa waamini kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kukimbilia katika Sakramenti ya upatanisho. Alitekeleza dhamana na wajibu wake wa kichungaji kwa moyo wa upole, unyenyekevu na ukarimu. Akajitahidi kumfuasa Kristo mchungaji mwema, kiasi cha kujisadaka kwenda kuwatangazia watu: huruma na upendo wa Mungu, sehemu zile ambazo Mapadre wengine waliziangalia kwa “macho ya kengeza” kwani zilikuwa kijijini, hakuna “matanuzi”. Huko ndiko ambako Mtakatifu Yohane Maria Vianney aliweza “kujichimbia” ili kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu mdhambi.

Mapadre wanakumbushwa kwamba, wamateuliwa kati ya watu kwa ajili ya mambo matakatifu na huduma kwa familia ya Mungu na wala wao si wafanyakazi wa mshahara kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anakazia mara kwa mara anapokutana na Wakleri. Mapadre wajitahidi kuwa ni watu wa kiasi, wenye huruma na upendo; watu wa furaha na utulivu wa ndani; watu wenye bashasha na tabasamu la kukata na shoka! Hii inatokana na sababu kwamba, Kristo hawapendi Mapadre wenye nyuso zilizokunjamana utadhani wameonjeshwa “pili pili kichaa”.

Mwenyezi Mungu amelijalia Kanisa lake Mtakatifu Yohane Maria Vianney ili kwa njia ya ushuhuda wa maisha na wito wake: aweze kuwakirimia waamini huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho na huduma makini katika shughuli za kichungaji. Tasaufi yake ya maisha ya kiroho iwe ni chemchemi ya majiundo makini na endelevu miongoni mwa Majandokasisi pamoja na Wakleri. Madhabahu ya Mtakatifu Yohane Maria Vianney, yaendelee kuwa ni chemchemi ya: wema na utakatifu wa maisha; sala na neema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Mapadre wajitahidi kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu; harufu safi ya utakatifu wa maisha. Heri na baraka ziwaendelee Maparoko wote duniani na wale watakaobahatika kuteuliwa kuwa Maparoko katika wito na maisha yao ya Kipadre.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.