2017-08-02 14:04:00

Kanisa Katoliki nchini Malawi kupongezwa kwa ajili ya ukarimu!


Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kwa niaba ya Baba Mtakatifu, Francisco, ameshukuru Kanisa Katoliki nchini Malawi kwa ukarimu wake kuchangia kwenye Mfuko wa mshikamano wa kimisionari ulimwenguni  ili  kuendeleza utume wa uinjilishaji.Katika barua iliyotumwa kwake Padre Vincent Mwakhwawa, ambaye ni Mkurugenzi wa Taifa wa  Baraza la Kimisionari  nchini Malawi, Askofu Mkuu wa Rugambwa amesema Mkutano Mkuu wa 2017 wa Baraza la Kipapa  la Kimisionari  umetoa shukrani kubwa kwa mchango wa fedha kutoka Malawi  pia kushiriki katika shughuli mbalimbali za kimisionari  zilizofanywa mwaka 2016.

Askofu Mkuu wa Rugambwa amesema hivi karibuni kuwa lengo kuu la mkutano mkuu ulikuwa ni kutafakari juu ya utambulisho, shughuli za uinjilishaji na mbinu za ushirikiano katika umoja na katika  utume wa Kanisa. Kwa njia hiyo pia  anawashukuru yeye mwenyewe  binafsi pia Wakurugenzi wote wa Taifa ambao wamewasilisha ripoti ya fedha ya shughuli zilizofanywa na sadaka zilizokusanywa kwa ajili ya shughuli za kimisionari kwa mwaka 2016 kwenye Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Aidha  amesema, ni shukrani hasa kwa bidii na utume wa kujitolea uliofanywa na shughuli mbalimbali za uhuishaji wa kimisionari na mafunzo ambayo yameandaliwa na kufanyika kwa roho ya ulimwengu wa Baraza la kipapa la  Mashirika ya  kimisionari nchini  Malawi.

Kwa mujibu wa Padre Mwakhwawa, Malawi imechangia jumla ya kwacha  25,697,276.61, ni kwacha zilizokusanywa  mwaka wa 2016 katika Jumapili ya sikukuu ya kimisionari, Utoto Mtakatifu na Jumapili ya kuombea miito, ukilinganisha na ukusanyaji wa mwaka 2015 ambao ulikuwa na kiasi cha kwacha 18,471,559.00 na hii inawakilisha ongezeko la  39.12%. Kutokana  na  ishara ya Askofu Mkuu wa Rugambwa kutuma barua ya shukurani kwa niaba ya Baba MtaktifuFrancisko, hata Padre Mwakhwawa ameshukuru pia Wakatoliki waaminifu wa Malawi ambao wamechangia kwa ukarimu na kutoa sadaka zao kwa ajili ya  uokovu wa roho nyingi duniani.

Padre anawashukuru pia makuhani wote wa maparokia ambao wanawafundisha watu na kuwakumbusha juu ya wajibu wa kikristo wa kuhubiri Injili katika ulimwengu wote kwa  kupitia maombi yao na sadaka za kujitoa kifedha. Zaidi ya yote, ni baraka kwa watu wa Malawi ambao wanaweza kubadilisha maisha ya watu na kujenga jumuiya ya imani ndani na nje ya Malawi kwa michango yao. Kwa njia ya sadaka hizi, watu wengi wataweza kusaidiwa kikamilifu. Ameongeza, mchango kutoka Kanisa Katoliki nchini Malawi ni ishara ya ukatoliki na mshikamano  wa Kanisa la Ulimwengu katika kuhubiri Injili ulimwengumi kote.

Aidha amesema, sadaka hiyo inaashiria ukomavu wa imani ya Katoliki nchini Malawi. Mkristo aliyeitwa na Yesu Kristo, lazima awajibike kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu wote. Kwa namna hiyo Wakatoliki katika kutoa mchango huo ni kuonyesha kwamba wao ni Wakristo hai na waliokomaa ambao wanaelewa ujumbe na maana ya utume katika  ulimwengu huu. Amemalizia akihimiza na kuwatia moyo wakatoliki wote wa Malawi kuendelea zaidi kuwa na ukarimu na zawadi za kiroho bila kujali changamoto za kiuchumi zinazo kabili nchi hiyo.

Sr Angela Rwezaula 
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.