2017-07-29 14:19:00

Kifo cha Mtoto Charlie Gard, kimewagusa na kuwatikisa watu wengi!


Watu wengi sana wameguswa na kifo cha mtoto mgonjwa Charlie Gard ambaye wazazi wake wamesimama kidete kupambana na ukiritimba wa mahakama, ili mtoto wao aweze kupatiwa tiba nje ya Uingereza, lakini ikashindikana kutokana na hali ya mtoto mwenyewe kuwa mbaya zaidi na hatimaye, tarehe 28 Julai 2017 mtoto Charlie Gard amefariki dunia, huku akiwa ameacha huzuni na simanzi kubwa kwa watu wenye mapenzi mema! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, anapenda kuchukua nafasi hii kumkumbuka na kumwombea Marehemu Charlie Gard; wazazi wake pamoja na wale wote walionesha upendo wa dhati kwake!

Wakati huo huo, Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales anasikitika sana kutokana na habari za kifo cha Mtoto Charlie Gard. Anapenda kuchukua nafasi hii kutoa salam zake za rambi rambi kwa wazazi walionesha upendo wa dhati kabisa bila kupungua hata chembe moja. Anapenda kuwahakikishia sala zake binafsi pamoja na za Jumuiya ya Waamini wa Kanisa Katoliki katika ujumla wao. Wanamwombea, ili Mwenyezi Mungu, aweze kumpokea Mtoto Charlie Gard miongoni mwa wateule wake. Awatie shime na kuwafariji wazazi, ndugu na jamaa wanaoomboleza kutokana na msiba huu mzito. Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales, linawashukuru wafanyakazi wa Hospitali “Great Ormond Street” waliojitahidi kumhudumia mtoto Charlie Gard katika maisha yake mafupi hapa duniani. Kanisa linatambua na kuthamini weledi na rasilimali iliyotolewa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, kila mtoto anapata tiba muafaka pamoja na faraja kwa familia zao, bila shaka watakuwa wameguswa sana na msiba huu. Na sasa apumzike kwa amani.

Kwa upande wake, Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia anasikita sana kwa kifo cha mtoto Charlie Gard ambaye amevuta hisia za watu wengi ndani na nje ya Italia. Katika kipindi hiki cha majonzi na huzuni, anapenda kuwahakikishia wazazi, ndugu na jamaa ya marehemu uwepo wao wa karibu kwa njia ya sala. Bwana Chris Gard na mkewe Connie Yates, wamekuwa kweli ni mfano bora wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kila mtu anawajibika kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha uhai wa binadamu, tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Ni matumaini ya Kardinali Gualtiero Bassetti kwamba, Malaika Charlie, huko mbinguni atakuwa faraja kwa wazazi wake katika kipindi hiki kigumu cha historia ya maisha yao. Wakati mwingine, majonzi yanakuwa makubwa kiasi cha kuwatumbukiza watu katika ugonjwa wa sonona.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha anasema, mtoto Charlie Gard, sasa amepumzika kwa amani na kwamba, watu wengi wanaona fahari sana kwa mtoto huyu ambaye wazazi wake wamepambana kiume, dhidi ya utamaduni wa kifo! Kwa wale waliotaka kunyofoa mrija wa maisha hata kabla ya wakati wake, wamekutana na wazazi wenye imani na msimamo thabiti kuhusu zawadi ya uhai. Hii ni familia ambayo imezungukwa na sala pamoja na faraja kubwa kutoka kwa watu mashuhuri duniani, bila kuwasahau watu wa kawaida. Askofu mkuu Vincenzo Paglia anakaza kusema, huruma na upendo wa Mungu ni wa milele, kamwe hawezi kunyofoa mrija wa matumaini kwa waja wake. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuanza kujikita katika utamaduni wa kuwasindikiza wagonjwa katika hatua za mwisho wa maisha yao hapa duniani, kwa kulinda, kuheshimu na kudumisha utu wa binadamu.

Huu ni wakati wa kujikita na kusema bila kumung’unya maneno kwamba, utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika: kifo laini; hali ya kutowajali wagonjwa pamoja na huduma ya upendeleo kwa baadhi ya vigogo, ni mambo ambayo kamwe hayawezi kukubalika. Maendeleo makubwa ya sayansi ya tiba ya mwanadamu, yasaidie kukuza na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kukubali kuwasindikiza wagonjwa katika safari yao ya mwisho hapa duniani kwa heshima na taadhima; maendeleo haya yawasaidie watu kupata tiba hata katika mateso na mahangaiko yao ya ndani! Kuwanyima tiba kwa “machozi ya mamba” kama kielelezo cha huruma ni kufuru dhidi ya utu na heshima ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.