2017-07-28 14:29:00

Askofu Rwoma: Mwaka wa Padre: Dumisheni utii; shindeni ubaya kwa wema


Askofu Desiderius Rwoma, alizaliwa kunako tarehe 8 Mei 1947, Jimboni Bukoba. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi akapadrishwa na Askofu Nestori Timanywa kunako tarehe 28 Julai 1974.  Kwa miaka mingi alikuwa ni Gombera wa Seminari Ndogo ya Rubya, Mlezi wa maisha ya kiroho wa Shirika la Masista wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, Jimbo Katoliki Bukoba na Makamu Askofu Jimbo Katoliki Bukoba.  Tarehe 19 Aprili 1999 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Singida, kufuatia kifo cha Askofu Bernard Mabula.

Aliwekwa wakfu kuwa Askofu na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam hapo tarehe 11 Julai 1999, kwenye Kanisa kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo Katoliki Singida. Tarehe 15 Januari 2013 akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Bukoba na msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki Singida, hadi kufikia tarehe 5 Julai 2015, alipong’atuka kutoka madarakani baada ya Baba Mtakatifu Francisko kumteua Mheshimiwa Padre Edward Mapunda kuwa Askofu awamu ya tatu, Jimbo Katoliki Singida.

Yote haya unayapata kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, wakati huu Kanisa nchini Tanzania linaadhimisha Jubilei ya Mwaka wa Padre, kwa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya wito na maisha ya kipadre kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Tanzania. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Desiderius Rwoma katika safari ya maisha yake ya kipadre alikumbana na changamoto nyingi lakini hakukata tamaa! Daima alipata ushirikiano mzuri kutoka kwa wazazi na walezi wake, waliomtia shime hata pale ambapo mbele yake kulionekana kuwa na giza nene, kutokana na hali ya familia, uwezo na karama ambazo amekirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya sifa na utukufu wa watu wake.

Anakiri kwamba, wosia aliopewa na Baba yake mzazi tangu siku ile ya kwanza alipoanza safari ya malezi na majiundo ya kikasisi kwa kumtaka “kuinamisha shingo” yaani kuonesha utii ni changamoto ambayo imemwezesha kusonga mbele katika safari ya maisha yake ya Kipadre na kiutu, hadi ukamilifu wa Daraja ya Upadre, kwa kuwekwa wakfu kuwa ni Askofu. Jambo la msingi kwa Padre anasema, ni kuhakikisha kwamba, anaupenda, anauthamini na kuulinda Upadre wake kwa hali na mali: kwa akili zake zote, kwa moyo wake wote na kwa nguvu zake zote!

Mambo mengine wanaweza kumnyang’anya, lakini daima ajitahidi kuukumbatia Upadre wake. Adhabu yoyote anaweza kuipokea na kuifanya, ili kuboresha maisha, wito na utume wake kama Padre. Hii inatokana na ukweli kwamba, zawadi ya wito na maisha ya kipadre imehifadhiwa katika chombo cha udongo kinachopaswa kuboreshwa kwa njia ya: Sala, tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Mapadre waupende sana wito wao!

Askofu Desiderius Rwoma anasema, Jambo la pili ambalo Mapadre wanapaswa kuzingatia ni kushinda uovu kwa wema, kauli mbiu aliyoitumia wakati wa maaadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 40 ya Upadre wake uliotukuka. Anatambua kwamba, fadhila ya unyenyekevu na uvumilivu zimemsaidia sana katika safari ya maisha na utume wake. Amekutana na changamoto nyingi, lakini akaweza kuzivuka kwa njia ya unyenyekevu na uvumilivu; kwa kutenda wema na kushinda ubaya. Na kwa njia hii, Mwenyezi Mungu akamkirimia neema na baraka katika maisha na utume wake.

Askofu Desiderius Rwoma anawataka Mapadre kuwa wanyenyekevu, wavumilivu na watiifu kwa Kristo na Kanisa lake. Daima wajitahidi kumwiga Kristo Mtumishi wa watu na wala siyo Kristo Mfalme huko wanaweza kuelemewa na ubinafsi, wakashindwa kutekeleza dhamana hii nyeti; wawe tayari kuwa ni mashuhuda amini kwa kumwiga Kristo Nabii wa ukweli na huruma ya Mungu kwa waja wake. Kristo Yesu, Mtumishi, ni kielelezo makini cha Padre katika ulimwengu mamboleo; ni sura ya mvuto na mashiko kwa watu wa Mungu, hasa wakati huu Kanisa nchini Tanzania linapoadhimisha Mwaka wa Padre. Daraja takatifu ni zawadi na neema ya Mungu kwa waja wake, kwa ajili ya huduma kwa mambo matakatifu. Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba, anawataka Mapadre kuwa na kiasi katika maisha; waheshimu na kuthamini wito na maisha yao ya Kipadre. Wawe na  busara na hekima katika kufikiri, kuamua na kutenda, daima wajitahidi kujiweka chini ya ulinzi na maongozi ya Mwenyezi Mungu kama udongo wa mfinyanzi, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwatumia kadiri ya mahitaji ya Kanisa kwa kuzingatia: karama, uwezo na nafasi katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.