2017-07-27 06:50:00

Wimbi kubwa la wakimbizi lisishughulikiwe kama moto wa mabua!


Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuzihama nchi zao kutokana na vita, ghasia, vurugu, dhuluma za kidini, kisiasa na kikabila, nyanyaso, njaa, umaskini, ukosefu wa fursa za ajira pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbali mbali za dunia linazidi kuongezeka na kwamba, sasa hii ni changamoto pevu na endelevu kwa Jumuiya ya Kimataifa. Ni fursa makini ya kuweza pia kutumia wimbi hili kubwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi yanayofumbatwa katika mshikamano wa kidugu.

Ikumbukwe kwamba, hawa ni watu wenye heshima, utu, utamaduni, mila, desturi na historia yao ambayo kamwe haiwezi kufutika kutokana na shida pamoja na changamoto zinazowaandama katika maisha. Ni watu wanaotafuta hifadhi ya maisha, uhakika wa usalama na maisha bora zaidi kuliko walikotoka. Dhana ya wahamiaji na wakimbizi ni sehemu ya vinasaba vya historia ya mwanadamu na daima wamekuwa ni changamoto kubwa na pale ambapo Jamii imeweza kutumia vyema changamoto hii, imekuwa ni kichocheo kikuu cha maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili.

Takwimu zinaonesha kwamba, hivi karibuni zaidi ya wakimbizi na wahamiaji 81, 292 wametia nanga ya matumaini kwenye fukwe za Jumuiya ya Ulaya kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kati yao asilimia 85% wako nchini Italia, ndiyo maana Serikali ya Italia inaitaka Jumuiya ya Ulaya kuwajibika kwa kuonesha mshikamano katika kukabiliana na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji Barani Ulaya kwa kuwekeza katika rasilimali fedha ili kuwahudumia vyema wakimbizi hawa kwa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki zao msingi. Wakimbizi na wahamiaji ni changamoto ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imeibua sera za utaifa, uchoyo na ubinafsi ambao umetumiwa na baadhi ya wanasiasa kutaka kujitafutia umaarufu wa kisiasa kwa kuwajengea wananchi hofu juu ya uwepo wa wakimbizi na wahamiaji sanjari na usalama wa maisha na mali zao!

Tabia na mwelekeo huu, umewajengea baadhi ya wananchi kuwa na chuki na uhasama dhidi ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi Barani Ulaya! Lakini, Baba Mtakatifu Francisko, daima amewataka waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kujenga mshikamano wa umoja, upendo na udugu na wakimbizi pamoja na wahamiaji, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, si rahisi kuweza kuishughulikia changamoto hii pasi na umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa.

Takwimu zinaoneasha kwamba, watu wanaoomba hifadhi ya kisiasa wameongezeka maradufu katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Hali ni mbaya sana huko Sudan ya Kusini kadiri ya takwimu zilizotolea hivi karibuni na Shirika la Kuwahudumia Watoto Wadogo la Umoja wa Mataifa, UNICEF, zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watoto milioni moja kutoka Sudan ya Kusini wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kama wakimbizi wanaohifadhiwa huko Uganda, Kenya na Ethiopia. Hatima ya watoto hawa kwa siku za usoni iko mashakani!

Vita, ghasia, kinzani na mipasuko ya kijamii kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2015 imepungua lakini waathirika wa majanga haya wameongezeka maradufu kufikia watu 150, 000 kwa mwaka 2015. Hii inaonesha kwamba, utamaduni wa kifo dhidi ya Injili ya uhai na matumaini imeongezeka sana duniani, kwani utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi si mali kitu, kinachotafutwa hapa ni faida kubwa inayotokana na biashara haramu ya silaha duniani. Na matokeo yake ni ongezeko kubwa la wimbi la wakimbizi na wahamiaji, wanaotumbukizwa tena kwenye biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo.

Asilimia 60% ya wananchi wa Siria wamelazimika kuikimbia nchi yao kutokana na vita ambayo inaendelea kupandikiza utamaduni wa kifo! Jambo hili linasikitisha sana! Huu ni mchango ambao umetolewa hivi karibuni na Kardinali Peitro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika maadhimisho ya Siku ya Wahamiaji Duniani kwa mwaka 2017 iliyoandaliwa na Kituo cha Kuwahudumia Wakimbizi cha Shirika la Wayesuit mjini Roma “Centro Astalli”. Majadiliano haya yamefanyika kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian kati ya Kardinali Pietro Parolin na Ferruccio De Bortoli na kuratibiwa na Padre Federico Lombardi, Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger, Papa Benedikto XVI.

Kardinali Parolin anasema, changamoto kubwa wakati wa vita ni kutafuta amani ili kuweza kuidumisha. Hii ndiyo diplomasia inayotekelezwa na Vatican sehemu mbali mbali za dunia. Wazo kuu ni kupambana na mambo ambayo yanaweza kusababisha vita yaani njaa na umaskini! Ikumbukwe kwamba, mahali palipo na vita, ghasia na mipasuko ya kijamii hapo kuna njaa, umaskini na magonjwa! Tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko amekazia kuhusu umuhimu wa diplomasia ya Vatican kufumbatwa katika amani, kwa kusimama kidete kupambana na baa la njaa na umaskini duniani; kwa kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote kwani kuna mamilioni ya watu wanaoathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa fursa za ajira na maendeleo endelevu!

Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na Jumuiya ya Kimataifa kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu, ili kuweza kukabiliana na changamoto kubwa na endelevu ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Mataifa yatambue kwamba, yanategemeana na kukamilishana na kwamba, binadamu ni kiumbe jamii. Kwa njia, hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuwa ni alama ya matumaini kwa wale waliokata tamaa ya maisha kutokana na sababu mbali mbali.

Kardinali Pietro Parolin anakumbusha kwamba, utambulisho wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya unafumbatwa katika mwingiliano wa watu, tamaduni na mapokeo mbali mbali, dhana inayoweza kuisaidia Jamii kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine kutokana na uchoyo, utaifa na ubinafsi usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wengi. Umoja na udugu ni chachu ya kutajirishana kwani hakuna mtu ambaye hana hata kidogo cha kuweza kutoa na kuwashirikisha wengine! Maskini hata katika umaskini wao wanao utajiri mkubwa unaoweza kuwasaidia wengine kutajirika katika maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni!

Watu wawe na ujasiri wa kujenga umoja, udugu na mshikamano. Haki ya uraia ni jambo ambalo linapaswa kupewa uzito wa pekee na wala lisiwe ni mbereko kwa baadhi ya wanasiasa wanaotaka kujitafutia umaarufu usiokuwa na tija kwa mafao ya wengi. Kumbe, kuna haja ya kuheshimu na kuthamini sheria, haki na wajibu ili kupata maridhiano katika mambo msingi. Vinginevyo anasema Kardinali Parolin, haki ya uraia inageuka kuwa ni ngumu kiasi hata cha kushindwa kupewa ufumbuzi wa kudumu. Changamoto ya wakimbizi inapaswa kushughulikiwa kwa kuwa na sera makini na endelevu na kamwe lisishughulikiwe kama “moto wa mabua”. Vatican inatambua mchango mkubwa ambao umeendelea kutolewa na Serikali ya Italia kwa ajili ya kuokoa maisha ya wakimbizi na wahamiaji pamoja na huduma mbali mbali kama ambavyo anakiri Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.