2017-07-26 15:36:00

Wahenga ni hazina ya jamii katika kurithisha tunu msingi za kijamii


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya watakatifu Yoakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria, katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anakazia umuhimu wa wazee katika maisha ya familia, kwani wao wanadhamana ya kurithisha amana na utajiri wa utu wa binadamu na imani; mambo msingi katika kila jamii! Waamini walei wanahamasishwa kuwa watakatifu, ili kuweza kuyachachua malimwengu kwa harufu ya utakatifu wa maisha; kwa kujibidisha kujenga maisha yao ya kiroho yanayoimarisha mahusiano yao na Mwenyezi Mungu, ili waweze kuangaliwa na Roho Mtakatifu katika medani mbali mbali za maisha. Wanapaswa kuimarisha muungano wao na Kristo Yesu, ili wamjue na kumpenda; daima wakitenga muda wao kwa ajili ya sala, tafakari na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kwa ufupi kabisa, waamini wanaalikwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma, neema na upendo wa Mungu kwa binadamu kama ilivyokuwa kwa watakatifu Yoakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria, ambao Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Julai anaadhimisha kumbu kumbu yao.

Wazazi na walezi wamechangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa watoto wao kuwa watu mashuhuri, wema, lakini zaidi watakatifu na mfano bora wa kuigwa na Jamii hata kwa nyakati hizi. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Watakatifu Yoakim na Anna wazazi wa Bikira Maria. Wao walisaidia sana kumfunda Bikira Maria, kiasi hata cha kupata upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu na hivyo kuteuliwa kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa; tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, Mama wa Kanisa linaloinjilisha na nyota ya uinjilishaji mpya kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.

Wazee wana wajibu na dhamana kubwa ya kuwaimarisha ndugu na jamaa zao katika fadhila ya imani, matumaini na mapendo, sanjari na kuwasaidia watu wao kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu ambaye kamwe hawezi kuwatupa waja wake wanaomkimbilia kwa moyo wa imani na matumaini. Hekima, ujuzi na mapendo ya wazee yasaidie mchakato wa malezi na familia. Lengo ni kuendelea kuihamasisha jamii kuwalinda, kuwatetea na kuwatunza wazee sanjari na kuthamini mchango wao katika ustawi na maendeleo ya familia nzima ya binadamu!

Parokia ya Mtakatifu Anna, iliyoko ndani ya Vatican, imeadhimisha kumbu kumbu ya Watakatifu Yoakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria kwa kusali kwa ajili ya kuombea maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, yatakayotimua vumbi kuanzia mwezi Oktoba, 2018 hapa mjini Vatican kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Kanisa linataka kuwasikiliza vijana wa kizazi kipya, ili kuwasaidia kutembea katika mwanga wa Injili ya Kristo Mfufuka kwa kuwajengea imani, matumaini na mapendo, tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Waamini wamesali pia kwa ajili ya kuombea maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 yatakayoadhimishwa nchini Panama kuanzia tarehe 22- 27 Januari 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema”. Haya ni maadhimisho yaliyoongozwa na Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu. Parokia imesali kwa ajili ya kuombea tukio hili muhimu sana katika maisha na utume wa vijana duniani, ili liweze kufanikiwa vyema kwa kuwashirikisha wahenga ambao kimsingi ni hazina kubwa ya utajiri na urithi wa imani, maadili na utu wema.

Katika maadhimisho haya, wanawake wenye mimba, wameombewa, ili Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa aweze kuwalinda kwa tunza na ulinzi wake wa kimama, ili hatimaye, waweze kujifungua salama salimini na watoto wao kukua na kuongezeka kwa kimo na nguvu, huku wakiwa wamejaa hekima na neema ya Mungu ikiwa juu yao. Wazazi watambue dhamana ya kuwaritisha watoto wao utajiri wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Amri za Mungu na Maisha ya Sala, ili kweli, familia za Kikristo ziweze kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.