2017-07-24 09:55:00

Papa Francisko: Asiyekuwa na dhambi anyooshe mkono!


Mfano wa ngano safi na magugu ni kielelezo makini cha uwepo wa ubaya na dhambi duniani, kinachoonesha uvumilivu wa Mwenyezi Mungu kwa binadamu mdhambi, anayepewa nafasi na fursa ya kutubu na kuongoka. Mavuno yatakayofanyika siku ya mwisho yanawaonesha wahusika wakuu ambao ni: mkuu wa shamba ambaye ni Mwenyezi Mungu anayepandikiza mbegu njema shambani mwake na upande wa pili ni adui shetani anayepandikiza magugu, yaani dhambi na ubaya wa moyo katika maisha ya mwanadamu. Huu ni mfano unaonesha pia mielekeo miwili tofauti juu ya ngano safi na magugu shambani.

Wafanyakazi wanataka kuyaondoa magugu haraka iwezekanavyo ili kutoa nafasi ya ngano safi kukua pasi na msongo wa ubaya, lakini mwenye shamba anaguswa sana na wokovu wa ngano yake, anaogopa kwamba, pengine kwa kuyang’oa magugu, wanaweza pia kung’oa ngano safi. Ndiyo maana Yesu anasema wema na ubaya duniani ni sawa na chanda na pete, ni vigumu kuweza kuutenganisha na hatimaye, kutupilia mbali ubaya wa moyo na dhambi. Ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayeweza kutenganisha ukweli huu, mwisho wa nyakati, atakapokuwa anatoa hukumu ya mwisho. Huu ni uwanja unaonesha uhuru wa Mkristo katika kuamua na kutenda mema, jambo linalohitaji mang’amuzi ya kutosha!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 23 Julai 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana. Baba Mtakatifu anahimiza umuhimu wa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kutegemea huruma yake, ili kufanya uamuzi wa busara kwa uvumilivu. Nia ya kutaka kuwa ngano safi ni changamoto na hitaji la watu wote, ili kuondokana na nguvu, vishawishi vya shetani na mambo yake yote.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, uvumilivu una maanisha kwa namna ya pekee kabisa, kulichagua Kanisa ambalo ni chachu isiyoogopa kuchafuka kwa kutibu na kuganga madonda ya watoto wake badala ya kutafuta Kanisa linalofikirika, yaani “Kanisa la watakatifu na wateule wa Mungu”, linalotaka kuhukumu hata kabla ya wakati, kwa kuwaangalia wale waliomo kwenye Ufalme wa Mungu na wale wanaokaa pembeni wakiangalia kwa jicho la husuda!

Kristo Yesu ni hekima ya Mungu iliyomwilishwa, awasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutambua kwamba, wema na uzuri; ubaya na dhambi ni mambo ambayo kamwe hayawezi kutambulikana kwa kuzingatia mipaka ya kijiografia au makundi ya watu! Wema na ubaya vinafumbatwa katika moyo wa binadamu, vinapita katika moyo wa kila mmoja wao: kwani wote ni wadhambi wametindikiwa neema ya Mungu kutokana na udhaifu wao wa kibinadamu! Baba Mtakatifu amewaalika waamini wanaojidai kuwa wao ni watakatifu na wala dhambi haimo kabisa ndani mwao, wanyooshe mkono! Hapa, kukawa na kimya kikuu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, kila mtu akainamisha kichwa chini kwa kutambua kwamba ni mdhambi anahitaji huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake!

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, Kristo Yesu, aliyezaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu, amewakomboa binadamu kutoka katika utumwa wa lindi la dhambi na mauti, kwa kuwajalia neema ya kuweza kutembea katika mwanga wa maisha mapya. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, amewakirimia waja wake Sakramenti ya Upatanisho, kwani, daima wanahitaji kusamehewa dhambi zao. Waamini wawe na ujasiri wa kutambua dhambi inayowapekenya katika undani wa maisha yao, wanapoona dhambi zinazotendwa na watu wengine na kamwe wasiwe ni watu wenye haraka ya kuhukumu!

Kristo Yesu anawafundisha waja wake namna tofauti ya kuangalia dhambi na ukweli wa maisha duniani. Wawe tayari kutambua nyakati za Mungu, ambazo kamwe si mali yao; wawe na ujasiri wa kutambua jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anaangalia, kwani hata yale yaliyoonekana kuwa kama magugu yanaweza kuwa ngano safi. Hii ndiyo dhana inayofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; tumaini katika maisha ya Kikristo! Bikira Maria aliyetambua na kupokea kweli katika uhalisia wa maisha yake anasema Baba Mtakatifu awasaidie waamini kutambua kwamba, licha ya kuzungukwa na dhambi pamoja na ubaya wa moyo; kuna wema na uzuri; mambo yanayofichua kazi ya shetani, lakini jambo la msingi ni kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu anayeongoza historia ya maisha ya mwanadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.