2017-07-24 13:45:00

Majadiliano ya kidini na kiekumene yasaidie kuzima kiu ya amani!


Familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kuendelea kujikita zaidi na zaidi katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni katika ukweli, uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni jukumu la waamini wa dini zote kujenga na kudumisha mshikamano, umoja, upendo na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba,  msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu, ndicho kilio kikuu cha familia ya Mungu Afrika ya kati. 

Haya ni kati ya mawazo makuu yaliyotoleewa na Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini katika ujumbe wake aliowaandikia wajumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati, CERAC,  katika mkutano wao wa mwaka Yaoundè, Cameroon na Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, amehudhuria. Katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano, Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot anasema, majadiliano ya kidini na kiekumene ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa, lakini kwa wakati huu huko Afrika ya kati.

Misimamo mikali ya kidini na kiimani inaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao sanjari na kuvuruga mafungamano, mshikamano na umoja wa kitaifa! Watu wamechoka na vita na sasa wanataka amani, jina jipya la ustawi na maendeleo ya watu! Vita na ghasia inayoendelea Kaskazini mwa Chad, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Gabon na Congo, Brazzaville inatishia usalama, amani, ustawi na maendeleo ya watu zaidi ya milioni 46, ndiyo maana watu wanataka mchakato wa upatanisho na amani upatiwe kipaumbele cha pekee huko Afrika ya Kati. Misimamo mikali ya kidini na kiimani inaendelea kusababisha vita na kupandikiza mbegu ya hofu, chuki na uhasama kati ya watu. Itakumbukwa kwamba, Mkutano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika ya Kati uliongozwa na kauli mbiu “ majadiliano ya kidini na kiekumene Afrika ya Kati, ni magumu, lakini ni jambo linalowezekana.

Viongozi wa Kanisa, watawa na waamini katika ujumla wao, wamekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene huko Afrika ya Kati hasa zaidi nchini Algeria na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Watu wajifunze kuheshimu na kuthamini tofauti msingi na kwamba, huu ni utajiri unaopaswa kukumbatiwa ili kujenga umoja katika utofauti kwa ajili ya ustawi wa wengine! Tofauti kati ya watu kisiwe ni chanzo cha vita, ghasia na mipasuko ya kijamii. Waamini wakiwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya umoja, amani, upendo na mshikamano, hata Serikali zao zitahamasika kukuza na kudumisha: ustawi na maendeleo ya wengi; kwa kuunda mazingira bora zaidi yatakayosaidia maboresho ya fursa za kazi, ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii; mambo msingi katika kudumisha amani na ustawi wa watu. Kila mwananchi ajitahidi kuwa kweli ni chombo cha amani mahali alipo. 

Amani na utulivu anasema Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot itasaidia kutumia kikamilifu rasilimali, utajiri na nguvu kazi ya vijana wa kizazi kipya inayowajumuisha vijana wenye umri kati ya miaka 14- 25, ambao ni zaidi ya milioni 200 Barani Afrika. Benki ya Maendeleo Kimataifa inasema kwamba, idadi hii ya watu inaweza kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2045. Lakini kwa bahati mbaya sana, asilimia 60% ya vijana wa kizazi kipya Barani Afrika hawana fursa za ajira, hasa katika nchi zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara na Kaskazini mwa Afrika. Hii ni hatari kubwa inayoweza kutumiwa na wajanja wachache kwa ajili kuvuruga amani na mshikamano wa kitaifa Barani Afrika kama inavyojionesha katika baadhi ya nchi kwa kuwatumbukiza vijana katika wimbi la misimamo mikali ya kidini na kiimani  kwa kuwapatia fedha kidogo ya kujikimu, lakini madhara yake ni maafa makubwa kwa watu na mali zao!

Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram nchini Nigeria, Al Shabaab nchini Somalia pamoja na vikundi vyote vyenye misimamo mikali ya kidini na kiimani ni matunda ya ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Ndiyo maana Kanisa halina budi kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitahi ya mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari na kuendelea kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema ili kukabiliana na changamoto zinazowasibu vijana wa kizazi kipya, tayari kuzipatia ufumbuzi wa kudumu kama sehemu ya mchakato unaopania kukuza na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Kanisa, Serikali na wadau mbali mbali wa maendeleo endelevu ya bnadamu, hawana budi kuwekeza zaidi katika elimu makini, itakayowakomboa vijana na kuwajengea uwezo wa kupambana na changamoto zinazowasibu kila siku ya maisha. Elimu ya ufundi na kilimo bora ni muhimu sana katika kupambana ukosefu wa fursa za ajira! Si vijana wote watakaoweza kubahatika kuendelea na elimu ya juu na vyuo vikuu, lakini vijana wengi wanaweza kupatiwa mafunzo ya ufundi yatayowasaidia kuchangia ustawi na maendeleo yao binafsi na jamii katika ujumla wake!

Majadiliano ya kidini na kiekumene yajikite katika kujenga, kukuza na kudumisha umoja, udugu na urafiki kati ya watu, ili waweze kusaidiana kwa hali na mali. Dini na Serikali zikishikamana katika huduma makini, zinaweza kusaidia kudhibiti wimbi kubwa la wahamiaji wa kiuchumi linalotafuta fursa bora zaidi za maisha nje ya Bara la Afrika, lakini kwa bahati mbaya, linajikuta likitumbukia katika tumbo la bahari ya Mediterrania na huko linakua ni kaburi lisilo na alama kwa wahamiaji na wakimbizi hawa! Majadiliano ya kidni yasaidie kupambana na tabia ya kutumia umaskini na unyonge wa vijana kwa ajili ya kupandikiza utamaduni wa kifo, chuki na uhasama kwa kisingizio cha imani na misimamo mikali ya kidini na kiimani.

Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot anakaza kusema, hata viongozi wa dini ya Kiislam wanayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanalinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kwa kuondokana na mambo yanayoweza kusababisha misimamo mikali ya kidini. Viongozi wa kidini wanapaswa kuandaliwa na kufundwa vyema kuhusu misingi, kanuni na maadili ya dini husika na kwamba, kimsingi dini ni chombo cha haki, amani na utulivu. Majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa Majandokasisi ni dhana inayoweza kufanyiwa kazi Barani Afrika, ili kweza kuwandaa viongozi watakaosimama kidete katika majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ukarimu, upendo na udugu ni mambo msingi yanayoweza kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Majadiliano ya waamini wa dini za Jadi Barani Afrika yapewe pia uzito unaostahili, vinginevyo tuhuma za imani za kishirikina zitaendelea kuzagaa kama umande wa asubuhi, kiasi cha kuwafanya hata Wakristo wenyewe kuwa ni watu wenye maisha ya undumilakuwili! Utu na heshima ya binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; haki msingi za binadamu ni mambo muhimu sana yanayoweza kukoleza mafungamano ya kijamii. Kumbe, majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na familia ya Mungu Barani Afrika kama sehemu ya ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani, udugu na umoja, ili kudumisha demokrasia ya kweli na utawala bora. Kila mtu anawajibika kutengeneza mazingira bora yatakayowawezesha watu kujisikia kuwa ndugu wamoja, licha ya tofauti zao, kwa kuonesha upendo na ukarimu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.