2017-07-20 14:27:00

Sinodi ya Maaskofu: Kanisa linataka kuchonga na kuwasikiliza vijana!


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana yataanza kutimua vumbi mwezi Oktoba, 2018 kwa kuongozwa na kauli: Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Kanisa linataka kujenga na kuendeleza utamaduni wa kuwasikiliza vijana kwa dhati, ili kuwasaidia kukua na kukomaa katika hija ya maisha yao ya kiroho na kiutu, tayari kutekeleza dhamana na wajibu wao ndani na nje ya Kanisa. Maadhimisho ya Sinodi ni kipindi muafaka kabisa kwa ajili ya kuwasikiliza vijana ambao ndio watakaokuwa wahusika wakuu.

Vijana wanapaswa kushirikisha mambo msingi yanayofumbatwa katika sakafu ya mioyo yao, changamoto wanazokabiliana nazo katika ujana pamoja na matumaini waliyo nayo kwa siku za baadaye, kwani ujana ni mali na fainali ni uzeeni! Hivi karibuni, Kardinali Baldisseri ameshiriki katika mkutano maalum wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè iliyoanzishwa na Fra Roger. Kwa muda wa juma zima, Kardinali Baldisseri anasema, amejichanganya na vijana wa kizazi kipya kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Kwa wakati huu, mada tete miongoni mwa vijana wengi ni: familia, ajira, urafiki na mapenzi! Haya ni mambo msingi ambayo Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè imeyapembua kwa kina na mapana, kwa kuwahusisha vijana wenyewe ili kuyaangalia yote haya katika mwanga wa Injili ya Kristo! Fra Roger katika maisha na utume wake alikazia kwa namna ya pekee kabisa umoja miongoni mwa vijana; umuhimu wa kazi kama njia ya kutosheleza mahitaji msingi ya familia ili ziweze kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Alipenda kuwahimiza vijana kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho, hasa kwa kukumbuka kwamba, hii ni tema ambayo ilivaliwa njuga na Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Jumuiya hii hapo tarehe 5 Oktoba 1986.

Kumbe, Jumuiya ya Taizè inafumbata kwa namna ya pekee kabisa maisha ya kimonaki yanayorutubishwa kwa njia ya: Sala, Tafakari ya kina ya Neno la Mungu, Ukimya na Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa! Kila siku walau kuna vijana zaidi ya 2500 wanaosindikizwa na Wamonaki katika maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Ni mkusanyiko wa vijana wanaosindikizana na kuambatana na wazazi, mapadre na wakati mwingine na maaskofu wao mahalia. Huu ni mfano bora sana wa kuigwa katika kukuza na kudumisha Injili ya umoja, upendo, udugu, amani na mshikamano wa dhati. Ni mahali pa kutafakari na kutafuta uwepo wa Mungu katika maisha ya vijana; amani na utulivu wa ndani; upatanisho pamoja na utajiri wa maisha ya kiroho.

Haya ni maisha yanayofumbatwa katika: ukweli na uwazi; uaminifu na nia njema. Hii ni Jumuiya inayowaunda na kuwafunda vijana kutembea kwa pamoja licha ya tofauti zao za kitamaduni, lugha na madhehebu yao, lakini wote kwa pamoja wanajisikia kuwa ni watoto wapendwa wa Mungu wanaohamasishwa kuambata tunu msingi za Kiinjili na kuzitolea ushuhuda! Kardinali Baldisseri anasema katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, kwa sasa Mama Kanisa anawasikiliza vijana wanataka kusema nini katika maisha na vipaumbele vyao. Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu imekwisha kuchapisha “Hati ya Maandalizi” itakayosaidia kutengeneza “Hati ya Kutendea Kazi” ijulikanayo kama “Instrumentum Laboris”.

Hati hii iliambatanishwa na barua kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko aliyowaandikia vijana, akiwachangamotisha kujenga jamii inayofumbatwa katika, haki, udugu na mapendo! Vijana wanaweza kuchangia mawazo yao kwa njia  mbali mbali zilizobainishwa na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu na kwamba, wanaweza kutuma maoni yao moja kwa moja kwenye Sekretari ili yaweze kufanyiwa kazi. Kwa wale vijana wanaopenda kutumia sana mitandao ya kijamii, wanaweza pia kutuma maoni yao kwa njia ya tovuti ya Sinodi ya vijana kwa anuani ifuatayo:

www.youth.synod2018.va.

Huko kuna vijana wengi ambao wanapenda kuwasiliana na jirani zao. Vijana wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kushirikisha mawazo, mang’amuzi pamoja na vipaumbele vyao. Watambue kwamba, katika historia kuna watu ambao wamejisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Kumbe hata wao wanaweza kuendeleza mchakato huu wa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kuhusu kigezo kikuu cha miito kwa vijana wote ni Kristo Yesu anayewaalika vijana wa nyakati zote kumfuasa ili kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wa Mataifa. Huu ni ushuhuda wa upendo kwa Mungu na jirani unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku!

Baba Mtakatifu anapenda kuwahamasisha viongozi wa Kanisa kuwa karibu zaidi na vijana wa kizazi kipya, ili kuweza kushiriki nao matumaini, mahangaiko na changamoto wanazokabiliana nazo katika mwanga wa imani, matumaini na mapendo. Vijana watambue kwamba, ndani ya Kanisa kuna watu wenye uzoefu mkubwa wa maisha, tunu na karama mbali mbali wanazoweza kujifunza na hatimaye, kuzigeuza kuwa ni sehemu ya utajiri wa majiundo yao: kiroho na kimwili. Lugha inayotumiwa na Mama Kanisa katika maisha na utume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya inapaswa kupyaishwa zaidi kama njia ya kusoma alama za nyakati.

Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anawaalika vijana wa kizazi kipya kutafakari kwa kina na mapana Injili na hatimaye, kuweza kuimwilisha katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vyao. Wajitahidi kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Waoneshe ari na moyo wa kuthubutu kutenda jambo jema kwa jirani zao wenye shida zaidi. Ikumbukwe kwamba, ukarimu wa Kikristo unapata chimbuko lake katika mchakato unaowawezesha waamini kushiriki katika kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu, ili kila mtu aweze kweli kupata utimilifu wa maisha na furaha ya kweli katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.