2017-07-20 15:31:00

Padre Mpete: Dumisheni mshikamano katika malezi na makuzi ya miito


Mwongozo Mpya wa Malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”. Uliotolewa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri unakazia:malezi na majiundo ya kipadre yanayopaswa kupyaishwa, kuendelezwa na kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Mama Kanisa. Mwongozo wa sasa unazingatia na kukidhi mahitaji msingi ya malezi na majiundo ya Kipadre ili kuweza kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni mwongozo unaotoa mwelekeo na uwiano sahihi wa malezi: kiutu, kiroho, kiakili na kichungaji kwa njia ya safari ya malezi na majiundo makini ya Kipadre, taratibu, lakini kila jandokasisi akiangaliwa kwa jicho la pekee.

Padre Enhart Mpete, Mkuu wa Kanda ya Tanzania, Shirika la Mapadre wa Upendo, hivi karibuni ameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwapongeza na kuwaaga watanzania waliokuwa wanahitimu masomo yao kwa mwaka 2016-2017. Ameishukuru Jumuiya ya Watanzania inayoishi Roma kwa kusaidiana kuleana, kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa watanzania, hasa ukizingatia kwamba, wako ughaibuni, kwenye changamoto nyingi. Anawashukuru wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya malezi kwa majandokasisi, mapadre na watawa wanaotumwa na Kanisa la Tanzania kwenda Roma kwa ajili ya kujiendeleza zaidi.

Padre Enhart Mpete anakazia umuhimu wa umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa watanzania kama njia ya kupambana upweke hasi unaoweza kumsababishia mtu kupoteza dira na mwongozo wa maisha. Umoja unawawezesha watanzania kufahamiana, kusaidiana kwa hali na mali na kusherehekea matukio mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa na jamii ya watanzania katika ujumla wake. Anawashukuru kwa umoja na mshikamano uliowawezesha Mashemasi wa Shirika la Mapadre Upendo kuhitimu masomo na majiundo yao mjini Roma na sasa tayari wamekwisha kupadrishwa. Amewapongeza pia watawa waliohitimu

Ikumbukwe kwamba, wajibu wa kukuza miito mitakatifu ni wa Jumuiya nzima ya kikristo, na inatakiwa kuutekeleza hasa kwa kuishi maisha bora ya kikristo. Mchango mkubwa unatolewa na familia zikiongozwa na roho ya imani, upendo na uchaji wa Mungu, ambazo hufanywa kama ndiyo seminari ya kwanza; vilevile na parokia zenye uhai tele, ambamo vijana wenyewe wanashiriki. Walimu na wote ambao, kwa namna moja au nyingine, wanahusika katika kutoa malezi kwa watoto na vijana hasa katika vyama vya kikatoliki watakiwa kujitahidi katika kuwafundisha vijana waliokabidhiwa ili kutambua wito mtakatifu na kuufuata kwa hiari. Mapadre wote watakiwa kuonyesha juhudi zao za kitume katika kuiendeleza miito mitakatifu zaidi iwezekanavyo, na kuivutia mioyo ya vijana kupenda upadre kwa maisha yao ya upole, bidii, nidhamu, furaha, pamoja na mifano ya upendo kati yao mapadre na ushirikiano wa kidugu.

Ni wajibu wa Maaskofu kuwatia moyo watu wao kuiendeleza miito na kuona kwamba nguvu zao zote na shughuli zao zote zinafungamana. Ni wajibu wao pia kujitolea bila kikomo, mfano wa baba, ili kuwasaidia wale ambao wanawatambua kuwa wameitwa katika huduma ya Bwana. Ushirikiano huu thabiti wa watu wote wa Mungu katika kuiendeleza miito mitakatifu, ni itikio kwa Maongozi ya Mungu, ambayo hugawa tunu bora zitakiwazo na kusaidia kwa neema yake wale ambao wamechaguliwa na Mungu kushiriki Upadre wa Kristo kidaraja. Maongozi hayo ya Mungu huwaaminisha wahudumu halali wa Kanisa wajibu wa kuwaita wateule watamanio utume huo mkubwa kwa moyo radhi na kwa uhuru wote, baada ya kuthibitishwa kufaa, na kuwawekwa wakfu kwa muhuri wa Roho Mtakatifu kwa ajili ya Ibada ya Mungu na ya huduma ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.