2017-07-19 15:48:00

Ziara ya Kardinali Parolin Russia inapania kujenga madaraja na amani


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni cha Italia, RAI UNO anasema, mwezi Agosti, 2017 anatarajia kufanya safari ya kikazi nchini Russia, kama msaidizi wa karibu sana wa Baba Mtakatifu Francisko ambaye anataka kutangaza Injili ya amani na kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu! Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujielekeza zaidi katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kujenga na kudumisha mazingira ya haki na amani.

Akiwa nchini Russia, Kardinali Parolin anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Rais Vladimir Puttin wa Russia na kwamba, tangu sasa anapenda kujiaminisha chini ya ulinzi, tunza na maongozi ya Roho Mtakatifu, ili kuendeleza uhusiano wa dhati uliopo kati ya Russia na Vatican sanjari na kuendeleza majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki la Kanisa la Kiorthodox. Itakuwa ni nafasi ya kuweza kujadiliana ana kwa ana na Rais Putin kuhusu mustakabali wa wananchi walioko huko Mashariki ya kati; mateso na mahangaiko ya wananchi wa Siria na Ukraine, nchi ambazo Russia ina mkono wake huko!

Hizi ni kati ya nchi ambazo Kardinali Parolin amezitembelea kama kielelezo cha mshikamano wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na watu wanaoteseka kutokana na vita! Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa diplomasia ya Vatican anakazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana kwa hali na mali huku ikiongozwa na kanuni auni ili kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa mbali mbali zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Vatican inapenda kukuza na kudumisha amani duniani kama kichocheo kikuu cha maendeleo endelevu ya binadamu yanayofumbatwa katika haki, ustawi na mafao ya wengi! Kwa mtazamo huu, Vatican inapenda kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi;  kwa watu kukutana na kuzungumza; kufahamiana na hatimaye kuweza kuelewana, kila upande ukijitahidi kujenga mazingira yatakayowakutanisha, ili hatimaye, waweze kushirikiana katika umoja na udugu. Hii ndiyo sera na mbinu mkakati wa diplomasia ya Vatican inayovaliwa njuga kwa wakati huu na Baba Mtakatifu Francisko, ili kujenga na kuimarisha udugu ambao si tu kufanana bali kufaana!

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, haya ni mambo msingi yanayofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani wa mtu binafsi; ni mambo yanayogusa sakafu ya moyo na akili ya binadamu; ili kujenga na kurobesha mahusiano na mafungamano kati ya jamii na jamii na kati ya taifa moja na jingine. Watu wakiambata huruma ya Mungu katika maisha na vipaumbele vyao, mambo mengi kuhusu mahusiano ya kijamii na kimataifa yanaweza kuboreka zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anawachangamotisha watu kubomoa kuta za utengano, ubinafsi na uchoyo sanjari na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Anawataka watu kuchuchumilia mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kusaidiana; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, hawa ambao ndio wale “akina yakhe, pangu pakavu tia mchuzi”; watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha; ili hatimaye, kuondokana na umaskini wa maisha ya kiroho na kiutu!

Programu hii ya Televisheni inagusia kwa muhtasari hija 19 za Kichungaji Kimataifa ambazo zimetekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko tangu alipoingia katika uongozi kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Katika safari zote hizi, Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kisiasa na kiutu na kitamaduni; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 6 hadi tarehe 11 Septemba, 2017 anatarajiwa kufanya hija ya kichungaji nchini Colombia inayoongozwa na kauli mbiu “Tupige hatua ya kwanza”. Hii itakuwa ni hija yake ya ishirini kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Mahojiano haya yamewashirikisha hata na “vigogo” wakuu kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican kama Askofu Marcelo Sanchez Sorondo, Mkuu wa Taasisi za Kipapa za Sayansi na Sayansi Jamii. Baba Mtakatifu Francisko anapokutana na viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa, daima anapenda kukazia umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha haki jamii, kwani katika Mafundisho Jamii, Kanisa linapenda kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi. Kanisa linapenda kuwatetea na kuwasaidia maskini; wakimbizi na wahamiaji; watu wanaoteseka na kunyanyaswa kutoka na mifumo ya utumwa mamboleo.

Kwa upande wake, Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri anasema, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kulihamasisha Kanisa kutoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake kwa kujenga madaraja ya watu kukutana. Ndiyo maana anataka hata majiundo ya awali na endelevu ya Wakleri yazingatie mambo msingi katika maisha ya waamini, daima wakijitahidi kwenda pembezoni mwa maisha ya watu ili kuweza kuunganisha utu na utajiri wa maisha ya kiroho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.