2017-07-18 15:22:00

Vatican: Sera na mikakati ya kupambana na baa la njaa duniani


Athari za mabadiliko ya tabianchi yaani: ukame wa kutisha, mafuriko, majanga asilia, vita, ghasia, kinzani na machafuko mbali mbali, ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kusababisha ongezeko kubwa la baa la njaa, ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula na umaskini duniani. Hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa, ili kuweza kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Ili kufanikisha malengo haya, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha pekee kwa uzalishaji katika sekta ya kilimo, kwa kuwawezesha pia wakulima wadogo wadogo wanaochangia uhakika wa usalama kwa familia zao pamoja na kujipatia kipato cha kuweza kuboresha hali ya maisha.

Takwimu zilizotolewa hivi karibuni katika mkutano mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO ualiokuwa unafanyika mjini Roma, kuanzia tarehe 3- 8 Julai 2017, zinaonesha kwamba kuna watu zaidi ya bilioni mbili wanaokabiliwa na uhaba wa chakula na lishe bora; zaidi ya watoto milioni 150 chini ya umri wa miaka 5 wanakabiliwa na utapiamlo wa kutisha duniani. Jambo la kushangaza ni kuona kwamba, wakati ambapo kuna watu wanakufa kwa baa la njaa duniani, lakini hapo hapo pia kuna watu zaidi ya bilioni mbili wanaokabiliwa na uzito wa kutisha, kutokana lishe kupita kiasi!

Wakulima vijijini wanapaswa kuwezeshwa zaidi kwa kupewa mitaji, pembejeo za kilimo na ushauri wa kilimo cha kisasa ili kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo bila kukaa na kusubiri kwamba, vita, ghasia na mipasuko ya kijamii iweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Vijana ambao ndio nguvu kazi na jeuri ya jamii, wanajikuta wakikimbilia mijini kutafuta riziki hali ambayo inagumisha uzalishaji katika sekta ya kilimo vijijini, kwani sehemu kubwa ya nguvu kazi inabaki kuwa ni wazee.

Kumbe, kuna haja ya kuwahamasisha vijana kwa kuwajengea mazingira bora ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa uzalishaji na huduma vijijini sanjari na kutunza amani, jina jipya la maendeleo endelevu! Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Monsinyo Fernando Chica Arellano, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Mashirika ya Chakula na Kilimo ya Umoja wa Mataifa, yenye Makao yake Makuu mjini Roma wakati wa mkutano mkuu wa FAO. Sekta ya kilimo inapaswa kuvaliwa njuga na Serikali husika kwa kutunga na kutekeleza sera na mikakati itakayowanufaisha wakulima vijijini; kwa kushirikiana na sekta binafsi na wananchi wa kawaida vijijini, ili kupambana na hatimaye, kuondokana na baa la njaa duniani, moja ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna nchi 19 duniani ambazo kwa miaka kadhaa zimeendelea kukumbwa na baa la njaa. Hii inatokana na ukweli kwamba, ni nchi zinazokabiliwa na vita, ghasia na machafuko ya mara kwa mara. Baadhi ya nchi hizi zimekumbwa kwa kiasi kikubwa na athari za mabadiliko ya tabianchi kiasi kwamba, zimeendelea kudidimia katika uzalishaji na ukuaji katika shughuli za kiuchumi. Wananchi kutoka katika maeneo haya wanaunda walau asilimia 60% ya watu wanaohitaji msaada wa chakula cha dharura na kwamba, FAO inapaswa kuwapatia watu hawa kipaumbele cha kwanza ili kuokoa maisha yao, changamoto inayohitaji mshikamano unaoongozwa na kauni auni.

Hiki ni kielelezo cha haki jamii inayopaswa pia kumwilishwa katika sekta ya kilimo kwa kuwa na uhakika wa soko la mazao ya kilimo yanayozalishwa na wakulima vijijini, kuliko tabia ya sasa ambayo kuna soko huria, linaloongozwa na nguvu ya kiuchumi! Uporaji wa maeneo makubwa ya ardhi unaofanywa na Makampuni makubwa kwenye nchi changa zaidi duniani kwa ajili ya kuzalisha nishati uoto ni hatari sana kwa uhakika na usalama wa chakula duniani. Takwimu zinaonesha kwamba, hali hii ni mbaya sana kwa nchi kadhaa Barani Afrika anasema Monsinyo Fernando Chica Arellano.

Kanuni ya mshikamano wa kimataifa inapaswa kuongoza matumizi na ugawanaji wa mapato ya kazi ya mikono ya wanadamu, ili kweli iweze kuwafaidia watu wengi zaidi kuliko mwelekeo wa sasa wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine! Mshikamano huu usimikwe katika ushirikiano wa teknolojia rafiki na mazingira katika mchakato mzima wa uzalishaji, uvunaji, usambazaji na masoko. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika elimu ya kilimo bora na cha kisasa ili kuondokana na kilimo cha kujihami.

Hali hii inawezekana, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itajikita zaidi katika kanuni maadili na mshikamano unaoratibiwa na kanuni auni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Mafanikio katika mchakato mzima wa uzalishaji katika sekta ya kilimo na chakula yanahitaji ushirikiano, uwajibikaji na mafungamano ya haki jamii yanayogusa medani mbali mbali za maisha ya watu kuanzia: katika sera na maboresho ya miundo mbinu ya kilimo; sheria na kanuni za nchi zinazowawezesha wakulima kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za nchi husika pamoja na kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na utunzaji na matumizi bora ya chakula kinachozalishwa!

Ni kashfa kubwa kuona watu wanakufa kwa baa la njaa duniani, na wengine wanashindwa hata “kujikuna” kutokana na shibe ambayo wahenga wanasema, eti ni “mwana malegeza”. Hapa watu hawana budi kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi, ili kuokoa maisha ya watu wanaoogelea katika baa la njaa na watoto wanaopoteza maisha yao kutokana na utapiamlo wa kutisha sehemu mbali mbali za dunia!

Jumuiya ya Kimataifa anasema Monsinyo Fernando Chica Arellano haina budi kujielekeza katika matumizi bora ya rasilimali maji kwa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji unaowajibisha na kuzingatia kanuni maadili na utu wema. Baa la njaa duniani kwa sasa linaendelea kutishia maisha ya mamilioni ya watu kuliko hata ilivyowahi kutokea tangu baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Maeneo yaliyoathirika ni pamoja na Yemeni ambako kuna mamilioni ya watu wanaoteseka na kufa kutokana na njaa ya kutisha, Sudan ya Kusini inayochangiwa pia na vita ya wenyewe kwa wenyewe pamoja na mpasuko wa kisiasa na kijamii; Somalia ambayo kwa miaka mingi imegeuka kuwa ni uwanja wa vita na machafuko na Nigeria, ambako mashambulizi ya kigaidi yamepelekea wakulima wengi kushindwa kufanya kazi mashambani.

FAO imetoa kipaumbele cha kwanza kwa kuhakikisha kwamba, inasaidia kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kupambana na baa la umaskini wa hali na kipato duniani; kwa kuendelea kuratibu matumizi bora zaidi ya rasilimali maji kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kuendelea kuwawezesha wakulima wadogo wadogo vijijini na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kupambana na vita, ghasia na mipasuko ya kijamii, ili amani iweze kurejea tena na hivyo kuwapatia watu nafasi ya kujihusisha na shughuli za uzalishaji katika sekta ya kilimo, kwani bila haki, amani na maridhiano kati ya watu, juhudi, sera na mikakati yote hii ni bure tu, kwani itatoweka na kufutika kama ndoto ya mchana!

Wajumbe wa FAO wamekazia pamoja na mambo mengine, utawala bora; matumizi sahihi ya ardhi; utekelezaji wa Mwongozo wa Uhakika wa Usalama wa Chakula wa Mwaka 2004 pamoja na kuendelea kushikamana katika mchakato wa kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa pamoja na kuanzisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira. Yote haya yanawezekana ikiwa Serikali na wadau mbali mbali wataendelea kushirikiana pamoja na Sekta binafsi; kwa Jumuiya ya Kimataifa kuchangia kwa hali na mali katika utekelezaji wa maamuzi yanayofikiwa kwenye vikao halali vya Jumuiya ya Kimataifa, kwani bila rasilimali fedha, sera na mikakati yote hii itashindwa kutekelezeka.

Mapambano dhidi ya baa la njaa duniani ni kati ya vipaumbele vya kwanza vya FAO katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Lakini bila ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa kwa hali na mali anasema Monsinyo Fernando Chica Arellano, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Mashirika ya Chakula na Kilimo ya Umoja wa Mataifa, yenye Makao yake Makuu mjini Roma, itaendelea kubaki kuwa ni ndoto ya mchana!

Umefika wakati wa kutenda kwa dhati na kuachana na propaganda zisizo na mvuto wala mashiko! Watu wote wahusishwe kwenye mapambano ya baa la njaa duniani na kamwe asiwepo mtu anayetengwa katika mapambano haya kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Watu wawajibike katika matumizi sahihi ya ardhi na rasilimali maji; wajikite katika kutunza na kuendeleza misitu na kwamba, maisha ya binadamu na mahitaji yake msingi yapewe kipaumbele cha kwanza!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.