2017-07-17 13:25:00

Utu na heshima ya binadamu inafumbatwa katika: ardhi, makazi na ajira


Utu wa mwanadamu ndicho kipimo cha heshima ya kazi na kwamba kazi ni kwa ajili ya mwanadamu na wala si mwanadamu kwa ajili ya kazi. Hii ni changamoto ya kufanya kazi kwa ushirikiano, kwani kazi pia ni wajibu unaopaswa kutekelezwa na binadamu. Kuanzia tarehe 15 hadi tarehe 21 Julai, 2017, Chama cha Wafanyakazi Wakristo Duniani (MMTC, WBCA, WMCW) kinachotekeleza dhamana na wajibu wake katika nchi 79 duniani, kinafanya mkutano wake huko Avila, Hispania, kama sehemu ya kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Mkutano huu unaongozwa na kauli mbiu “ Ardhi, Makazi na Ajira kwa ajili ya maisha yenye utu” na unahudhuriwa na wajumbe 120.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anakazia umuhimu wa utu na heshima ya binadamu unaofumbatwa kimsingi katika mambo makuu matatu yaani: ardhi, makazi na ajira. Haya ni mambo ambayo yanamwezesha mtu kujisikia kuwa ni sehemu ya familia na jamii katika ujumla wake. Kumbe, kuna haja kwa Chama cha Wafanyakazi Wakristo Duniani kusimama kidete  kulinda na kutetea utu na heshima ya kila binadamu, ili kwamba, asiwepo mtu awaye yote anayetengwa na kusumizwa pembezoni mwa jamii.

Hii ni changamoto makini inayofumbatwa katika imani. Mwenyezi Mungu alimtuma Mwanaye wa pekee duniani, akaja na kuishi katika familia, akashiriki historia ya maisha ya watu wake na kufanya kazi kwa juhudi, bidii na maarifa na hatimaye, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, akamkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi kudumu katika ari na mwamko mpya, daima wakijizatiti kuhakikisha kwamba,  wanatangaza na kushuhudia Injili katika ulimwengu wa wanafanyakazi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.