2017-07-15 06:58:00

Kanisa linaimarika zaidi katika umaskini, mateso na madhulumu!


Umaskini, mateso na manyanyaso ni kama nguzo tatu zinazolitia nguvu Kanisa. Itakumbukwa kwamba tarehe 16 na 17 Juni, 2017, takribani wakatoliki 350 wa makabila ya Hmong, Kmhmu, Lao na Karen wamekutana Belleville-Illinois nchini Marekani kwa heshima ya kumbukumbu ya wafiadini 17 wa nchi ya Laos, ikiwa ni ishara ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha na imani ya wafiadini hao. Kardinali Louis-Marie Ling Mangkhanekhoun, Msimamizi wa kitume wa Paksè, anaelezea maisha ya Kanisa katika umaskini, mateso na manyanyaso, na sababu za yeye kupewa heshima ya Ukardinali, hivi karibuni.

Kardinali Ling anakumbusha maneno ya Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 26 Januari 2017, wakati maaskofu wa Laos walipofanya hija ya kitume, ad limina, mjini Vatican, inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano. Baba Mtakatifu Francisko aliwaambia Maaskofu wa Laos kwamba: nguvu ya Kanisa imejisimika kwenye makanisa mahalia, na kwa namna ya pekee makanisa machanga, yanayoteseka na manyonge zaidi duniani. Kufuati mtazamo huo, Kardinali Louis-Marie Ling Mangkhanekhoun anasema, nguvu ya Kanisa ipo katika uvumilivu na nia njema ya kuukubali ukweli kuhusu imani. Hivi ndivyo alipofika kwenye hitimisho ya fikra zake kwamba, umaskini, mateso na manyanyaso ni kama nguzo imara za Kanisa.

Nchini Laos kuna wakatoliki 45,000 ambao ni asilimia moja tu (1%) ya wakazi nchini humo. Wakatoliki hawa wanahudumiwa na mapadri 28, na watawa 98 katika parokia 218. mwaka 2015, katika mahojinao na Shirika la habari za Kanisa barani Asia, AsiaNews, Kardinali Ling alisema kwamba Kanisa la Laos bado ni changa ma linaishuhudia imani kati ya maadui wengi. Itakumbukwa kwamba mwaka 1975 katika utawala wa kikomunisti wa Pathet Lao, wamisionari walifukuzwa, wakatoliki wakateswa, mapadri wakawekwa ndani, akiwemo Ling mwenyewe ambaye alikuwa gerezani kwa miaka mitatu.

Leo hii nchi ya Laos ina  mahusiano mazuri na nchi na jumuiya zingine duniani, uchumi unapanda lakini bado hali za watu ni maskini na wanaishi kwa kutegemea misaada kutoka nje. Serikali ina sheria kali za uhuru wa kuabudu na uhuru wa kujieleza kwa vyombo vya habari. Kwa upande wa Kanisa, mapadri wana ruhusa ya kuadhimisha misa palipo na parokia tu na sio vinginevyo, wala Kanisa haliruhusiwi kujenga parokia zingine.

Uchaguzi wa Kardinali wa kwanza nchini Laos, Kardinali Ling, ni ishara nzuri ya matumaini kwa Jumuiya mahalia ya Laos kujenga mahusiano ya kidiplomasia na Vatican. Kardinali Ling anaahidi kulifanyia kazi suala la mahusiano mazuri ya kidiplomasia kati ya serikali ya nchi hiyo na Vatican. Mahusiano na wabudisti ni mazuri, lakini changamoto ipo kati ya wakatoliki na wakristo wa madhehebu mengine, kwani namna ya kuielewa Injili na kuihubiri ni tofauti, anasema Kardinali Ling. Baba Mtakatifu Francisko baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, tarehe 21 Mei 2017, alitangaza nia ya kuwapa heshima ya Ukardinali maaskofu watano, ambao wamesimikwa rasmi tarehe 28 Juni 2017, mmoja wao akiwa Kardinali Ling.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.