2017-07-14 16:19:00

Colombia: Vipaumbele: amani na upatanisho wa kweli!


Askofu mkuu Oscar Urbina Ortega wa Jimbo kuu la Villavicencio, ndiye aliyechaguliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia, kuwa Rais wao mpya kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka 2020 na hivyo kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Askofu mkuu Luis Augusto Castro Quiroga, aliyemaliza muda wake. Vipaumbele vyake kwa wakati huu ni mchakato wa haki, amani na upatanisho nchini Colombia, hasa wakati huu wa kipindi cha mpito kutoka katika vita ya wenyewe kwa wenyewe  na kuanza kutembea pamoja kama ndugu wamoja!

Changamoto kubwa mbele ya familia ya Mungu nchini Colombia ni upatanisho na msamaha wa kweli, changamoto itakayoimarishwa na kupyaishwa kwa uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko, mmissionari wa upatanisho. Lengo ni kuganga na kuponya madonda ya vita na utengano kwa mafuta ya huruma, msamaha na upatanisho katika ukweli na uwazi! Ni wakati wa kujikita katika mchakato wa majadiliano kwa kuheshimiana, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Colombia

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko  nchini Colombia kuanzia tarehe 6 – 11 Septemba 2017 ni sehemu ya mchakato wa hija ya Mama Kanisa nchini Colombia kutaka kuenzi maridhiano, haki na amani, baada ya Colombia kuwa katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka zaidi ya hamsini. Kumbe, anasema Askofu mkuu Oscar Urbina Ortega lengo la kwanza la hija ya Baba Mtakatifu ni la kichungaji ili kuimarisha na kudumisha mchakato wa haki, amani na upatanisho.

Kauli mbiu ya hija hii ni “Demos el primer paso” yaani “Tupige hatua ya kwanza” katika mchakato wa ujenzi wa haki, amani na upatanisho kwa kufuata nyayo za Baba Mtakatifu Francisko ambaye anapenda kutangaza Injili ya haki, amani na upatanisho kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani, upendo na udugu mambo msingi katika kukuza na kudumisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili! Familia ya Mungu nchini Colombia inataka kuanza kuandika ukurasa mpya wa maisha yake kwa kujikita katika upatanisho. Hii ni safari nyeti inayohitaji ari na moyo mkuu; uvumilivu na udumifu; kwa kusindikizana na kusaidiana katika ukweli na uwazi.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Colombia ni kwa ajili ya ustawi wa familia ya Mungu nchini humo! Askofu mkuu Luis Augusto Castro Quiroga, aliyemaliza muda wake anakaza kwa kusema hii ni hija ya kichungaji inayojikita katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazopania kukuza ukweli unaofumbata umoja katika utofauti wa wananchi wa Colombia sanjari na kuendelea kutafuta ukweli utakaowaweka huru. Ni wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini kwa kuondokana na maamuzi mbele pamoja na kiburi cha kisiasa na kiitikadi; ili hatimaye, kujenga familia ya Mungu nchini Colombia inayofumbata umoja na ukweli; upatanisho na msamaha wa kweli unaopata chimbuko lake kutoka katika undani wa maisha ya watu. Wongofu wa ndani, toba na msamaha wa kweli, uwasaidie wananchi wa Colombia kuanza maisha mapya, kwa kuheshimiana na kuthaminiana; kwa kusaidiana na kushikamana kama familia ya Mungu inayowajibikiana kwa kutembea kwa pamoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.