2017-07-13 15:09:00

Njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi ni muhimu Venezuela


Askofu mkuu Diego Rafael Padròn, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela anasema, kuna haja kwa Serikali pamoja na wapinzani kusitisha ghasia na mapigano na kuanza tena mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kusitisha umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia! Tangu machafuko ya kisiasa yaibuke nchini Venezuela watu wengi wamepoteza maisha na kwamba, shughuli za uzalishaji na huduma zinaendelea kusua sua kiasi kwamba, baada ya muda si mrefu, wananchi wengi wa Venezuela watambukia katika dimbwi la umaskini mkubwa.

Hapa kuna haja ya kuwashirikisha wadau mbali mbali watakaosaidia kurejesha tena hali ya usalama, haki, amani na maridhiano kati ya watu. Miezi mitatu imekuwa kweli ni miezi ya shida na patashika nguo kuchanika, kiasi kwamba, watu wanaanza kukata tamaa na wanasiasa “wamegangamara na kushupalia maamuzi yao” kana kwamba, hakuna kinachotendeka! Kumekuwepo na uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu, zaidi ya watu tisini wamekwisha kupoteza maisha, sawa na wastani wa mtu mmoja anayeuwawa kila siku. Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela linasema, kuitisha Bunge kwa ajili ya kura ya maoni ni kupoteza muda pamoja na kutozingatia ustawi na mafao ya wengi.

Mara ya mwisho, Venezuela ilibadili Katiba kunako mwaka 1999! Changamoto kubwa kwa sasa nchini Venezuela si Katiba mpya mbayo kimsingi ni sheria mama, bali suluhu ya matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi wa Venezuela kwa wakati huu yaani: Ukosefu wa mahitaji msingi ya binadamu: chakula, malazi, huduma bora ya elimu na afya, ustawi na maendeleo ya jamii! Venezuela inapaswa kusimamia haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Haya ndiyo mambo msingi yanayopaswa kuvaliwa njuga na Serikali ya Rais Maduro kuliko kutaka kura ya maoni ambayo haina tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya watu.

Kanisa nchini Venezuela linaendelea na maisha na utume wake, ingawa linakabiliwa na hali ngumu sana, lakini anasema Askofu mkuu Diego Rafael Padròn, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela hakuna dhuluma dhidi ya Kanisa. Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela litaendelea kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, litawasaidia wananchi kudai haki zao msingi kwa njia ya amani. Matatizo na changamoto mamboleo, zisiwakatishe tamaa waamini, bali waendelee kumtumainia Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.