2017-07-12 14:27:00

Umoja wa Ulaya wekezeni katika mchakato wa haki, amani na upatanisho!


Baraza la Makanisa Ulaya, CEC, linayounganisha Makanisa zaidi ya 115 lililoanzishwa kunako mwaka 1959, lenye makao yake makuu mjini Brussels, Ubelgiji, linaitaka Jumuiya ya Ulaya kuwekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa amani na upatanisho, badala ya mwelekeo wa sasa wa kutaka kuwekeza zaidi katika nguvu za kijeshi. Mwezi Juni, Tume ya Ulaya iliwasilisha mpango mkakati mpya wa kuanzisha Mfuko wa Ulinzi Barani Ulaya, unaopania pamoja na mambo mengine, kutoa msaada wa fedha kwa viwanda vya silaha Barani Ulaya pamoja na kuimarisha sera na mikakati ya ulinzi na usalama. Baraza la Makanisa Ulaya linapinga hatua hii kwani inataka kuugeuza Umoja wa Ulaya kuwa ni mshikamano wa kijeshi.

Kadiri ya maelezo ya Tume ya Ulaya, Mfuko wa Ulinzi Barani Ulaya utapaswa kuchangia tafiti na maendeleo ya utengenezaji wa silaha kiasi cha Euro milioni 90 hadi ifikapo mwaka 2020 pamoja na kusaidia kutoa ruzuku kwa viwanda vya silaha Barani Ulaya kwa kiasi cha Euro milioni 500 ifikapo mwaka 2020. Baraza la Makanisa Ulaya linasema, si busara kutumia kiasi kikubwa cha fedha ya umma kwa ajili ya kutoa ruzuku kwa viwanda vya silaha badala ya kuzielekeza katika mchakato wa upatanisho, amani, utulivu, ustawi na maendeleo ya wengi; mambo msingi yanayoweza kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi wenyewe!

Umoja wa Ulaya kama mradi ulioanzishwa kukuza na kudumisha amani, unapaswa kujielekeza zaidi katika mchakato wa kuzuia vita, kinzani na mipasuko ya kijamii badala ya kutenga bajeti kwa ajili ya kugharimia viwanda vya silaha vinavyopandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo. Kumbe, rasilimali watu na fedha havina budi kuelezwa zaidi katika mchakato wa ujenzi wa amani kama kipaumbele kwa Bara la Ulaya. Fedha hii itumike kugharimia ukuaji wa uchumi, utakaosaidia kutengeneza fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya pamoja na kuangalia vipaumbele vilivyopo kwa sasa. Baraza la Makanisa Ulaya linayataka Makanisa katika Mataifa ya Ulaya, kushiriki kikamilifu katika mjadala huu, ili hatimaye, fedha ya walipa kodi itumike zaidi katika ukuaji wa uchumi na wala isiwe ni sababu ya kuanza kugharimia utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.