2017-07-12 10:14:00

Mshikamano wa udugu na upendo kwa watu wanaoteseka kwa njaa Afrika


Baba Mtakatifu Francisko anasema, kila mtu anayo haki ya kuwa na uhakika wa usalama wa chakula sanjari na kuwezeshwa kupambana na baa la umaskini na magonjwa. Haya yanawezekana ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itajikita katika ujenzi wa utamaduni wa upendo na mshikamano unaongozwa na kanuni auni! Kuna nchi ambazo zinashindwa kuzalisha na hatimaye kujitosheleza kwa chakula kutokana na sababu mbali mbali kwa mfano: kiwango chake cha maendeleo, umaskini, athari za mabadiliko ya tabianchi sanjari na vita pamoja na ghasia zinazowafanya watu wengi kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kilimo!

Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland, kwa kuguswa na mahangaiko ya watu zaidi ya milioni 25 wanaoteseka kutoka na baa la njaa huko Kenya, Sudan ya Kusini, Somalia na Ethiopia, limeamua kwamba, Jumamosi tarehe  22 na Jumapili tarehe 23 Julai 2017 kukusanya mchango maalum kwa ajili ya kusaidia wananchi wanaoteseka kutokana na baa la njaa Barani Afrika. Mchango huu utasimamiwa na kuratibiwa na Shirika la Maendeleo la Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland, Tròcare.

Askofu mkuu Eamon Martin, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland anasema, pengine watu wanaweza kupigwa bumbuwazi kutokana na idadi kubwa ya watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa Barani Afrika! Lakini, jambo msingi ambalo wanapaswa kukumbuka ni kwamba, nyuma ya namba hizi zinazotisha, kuna watu wanaoteseka na kufa kutokana na baa la njaa, kumbe wanahitaji kuonjeshwa huruma inayomwilishwa katika matendo, kama kielelezo cha imani tendaji! Nchi kadhaa, Barani Afrika zimekumbwa na ukame wa kutisha, hali ambayo inatishia usalama nauhakika wa chakula kwa mamilioni ya watu.

Vita, ghasia na mipasuko ya kijamii na kisiasa ni kati ya mambo yanayoendelea kuchangia kukua na kukomaa kwa baa la njaa katika maeneo mengi Barani Afrika. Watu wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na ukame wa kutisha hali ambayo imepelekea wafugaji kupoteza mifugo yao. Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linaialika familia ya Mungu nchini humo kuonesha upendo na mshikamano wa dhati na waathirika wa baa la njaa na ukame Barani Afrika. Askofu William Crean, Mwenyekiti wa Shirika la Maendeleo la Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland, Tròcare anasema, Shirika hili tayari linaendesha shughuli ya huduma ya kuokoa maisha ya watu walioathirika na baa la njaa pamoja na ukame katika maeneo mbali mbali Barani Afrika.

Shirika la Tròcare limekuwa mstari wa mbele kwa ajili ya huduma ya afya ya msingi huko Somalia, nchi ambayo kwa sasa imegeuka kuwa ni uwanja wa vita. Zaidi ya watoto 13, 000 nchini Kenya wanatarajiwa kupewa msaada wa chakula ili kuwawezesha kuendelea na masomo pamoja na kupata maji safi na salama, yatakayowakinga kwa magonjwa ya milipuko yanayojitokeza mara kwa mara katika mazingira kama haya! Inasikitisha kuona kwamba, licha ya Umoja wa Maifa kuomba msaada wa fedha ya dharura kwa ajili ya kupambana na baa la njaa Barani Afrika na Yemen ambako watu wanaendelea kupukutika, lakini, hadi sasa, inaonekana kana kwamba, mataifa yameziba masikio na wala hayataki tena kusikia wimbo wa baa la njaa duniani, ingawa hii ndiyo hali halisi kwa sasa. Hiki ni kipindi cha kuonesha mshikamano wa dhati na waathirika wa baa la njaa na ukame wa kutisha, kielelezo makini cha imani tendaji, kama anavyokaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.