2017-07-12 09:00:00

Mshikamano wa Papa Francisko na wananchi wa Ukraine wanaoteseka!


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kuanzia tarehe 11 Julai hadi tarehe 17 Julai 2017 anafanya ziara ya kikazi nchini Ukraine, kama kielelezo cha upendo na mshikamano kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa wananchi wa Ukraine ambao bado wanateseka kutoka na vita. Wengi wao hawana tena makazi ya kudumu na wamejikuta wakilazimika kukimbia nchi yao wenyewe ili kutafuta usalama na hifadhi ya maisha.

Kardinali Sandri yuko nchini Ukraine kwa mwaliko wa Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk wa Jimbo kuu la Kyiv- Halyc na ametumia fursa hii kuwasilisha rasmi salam na baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayewakumbuka wananchi wa Ukraine katika sala na sadaka yake! Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wale wote wanaoendelea kujisadaka  kwa ajili ya kutafuta haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Ukraine kutokata tamaa; Kanisa kwa upande wake, litaendelea kuwa ni chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake kwa njia ya huduma makini kwa watu wanaoteseka kutoka na vita!

Takwimu zilizotolewa hivi karibuni kutoka Ukraine zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watoto 750, 000 ambao afya yao iko hatarini kukumbwa na magonjwa mbali mbali baada ya kukosa maji safi na salama kwa muda wa miaka mitatu ya vita nchini Ukraine. Watu milioni nne wanahitaji msaada wa dharura na kwamba, watu zaidi ya milioni moja wamelazimika kuyakimbia makazi yao ili kutafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Katika safari hii ya kikazi, Kardinali Sandri anaambatana na Askofu mkuu Claudio Gugerotti, Balozi wa Vatican nchini Ukraine. Jumanne, tarehe 11 Julai 2017 Kardinali Sandri alipowasili nchini Ukraine, amekwenda kutoa heshima zake za dhati kwa wahanga wa machafuko ya kisiasa nchini humo.

Jumatano, tarehe 12 Julai 2017, Kanisa nchini Ukraine limeadhimisha Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani. Imekuwa ni fursa kwa Kardinali Sandri kuweza kushiriki katika Liturujia Takatifu na baadaye kusali kwenye kaburi la Marehemu Kardinali Lubomyr Husar, kiongozi aliyelazimika kuishi mafichoni kutokana na dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo huko Ukraine! Licha ya changamoto zote hizi, lakini bado aliendelea kuwa ni mtu mwenye furaha; akabahatika kuwa ni Baba na kiongozi mkuu wa Kanisa la Kikatoliki na Kigiriki nchini Ukraine. Katika hali ya uzee na ugonjwa akaendelea kubaki kati pamoja na watu wake na kuendelea kuwa ni rejea kama Mwalimu wa matumaini. Alikuwa na uwezo wa kuzungumza na kueleweka na wengi, kiasi hata cha kugusa undani wa maisha yao!

Marehemu Kardinali Lubomyr Husar alikuwa na hekima ya Injili; Mkate wa Neno la Mungu uliomegwa kwa ajili ya maskini, wagonjwa pamoja na wale wote waliokuwa wanatafuta utu na heshima yao kama binadamu! Alikuwa anakemea na kukanya kwa ari na moyo mkuu; akaeleza na kufafanua mambo kwa kina na mapana; akawa kweli ni faraja kwa waamini na wale wasioamini; akawa ni shuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo, matumaini na wazi mbele ya mpango wa Mungu kwa watu wa Ukraine kwa siku za usoni. Alibahatika kuwa na neno kwa kila mtu aliyemwendea kwa ushauri; akaonesha utu na upole! Alipenda kujadiliana na vijana wa kizazi kipya na wao wakatambua hazina kubwa iliyokuwa imefichika kwake, wakawa wanamkimbilia kwa wingi! Hivi ndivyo alivyokumbukwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maziko yake!

Kardinali Sandri, Alhamisi, tarehe 13 Julai 2017 anashiriki katika Liturujia Takatifu na kubariki Msalaba kwa ajili ya Mnara wa Kanisa kuu; atatembelea kambi za wakimbizi, atakutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Makanisa pamoja na kufanya nao hija ya kitaifa kwa ajili ya Ibada kwa Bikira Maria, Jumamosi tarehe 15 Julai 2017. Anatarajiwa kushiriki mkesha pamoja na kukutana na vijana kutoka Ukraine. Jumapili, tarehe 16 Julai 2017 atashiriki Liturujia Takatifu na kutembelea Makanisa ambayo yanahifadhi miili ya viongozi wakuu wa Kanisa nchini Ukraine. Tarehe 17 Julai, 2017 Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki anatarajiwa kurejea tena mjini Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.