2017-07-08 16:03:00

WYD 2019: Vijana mjifunzeni Kristo kupitia shule ya Bikira Maria


Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 itaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Idadi kubwa ya familia ya Mungu Amerika ya Kusini inaundwa na vijana wa kizazi kipya, lakini kwa bahati mbaya sana, wengi wao wanakabiliwa na ukosefu wa fursa za ajira, hawa ndio ambao Kanisa linataka kuwaonjesha upendo na huruma ya Mungu kwa njia ya sera na mikakati makini ya utume wa vijana.

Nembo ya maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko Panama imechorwa na Ambar Calvo, kijana mwenye umri wa miaka 20 anayesoma kwenye Chuo Kikuu Panama ndiye aliyeshinda shindano la kutunga nembo ya maadhimisho haya baada ya kuwabwaga washiriki wengine 103. Nembo hii imehakikiwa na jopo la watalaam waliotaalaumiwa katika masuala ya taalimungu, uchumi na masoko na hatimaye, kupitishwa rasmi na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, kwani ndilo lenye dhamana ya kuandaa na kusimamia maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

Askofu mkuu Josè Domingo Ulloa Mendieta wa Jimbo kuu la Panama ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Panama anawapongeza na kuwashukuru vijana waliojitokeza kuonesha na kushirikisha karama na kipaji chao cha ugunduzi. Lakini nembo ya kijana Ambar Calvo iligusa na kukonga nyoyo za wengi kutokana na ujumbe unaowakilishwa kwenye nembo hii. Huu ndiyo ujumbe ambao Panama inataka kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa kuonesha ukarimu na upendo unaobubujika kutoka kwa familia ya Mungu nchini Panama.

Huu ni upendo shirikishi unaowaambata wote pasi na ubaguzi, changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika ulimwengu mamboleo, ambapo ubinafsi na uchoyo vinaendelea kutawala katika nyoyo za watu wengi! Nembo inaonesha: imani, ukarimu na majitoleo ya Bikira Maria aliyekubali kupokea mpango wa Mungu katika maisha yake, akawa kweli ni Mama wa Mungu na Kanisa! Vijana wanahamasishwa kufanya hija ya maisha ya kiroho huko Panama kuanzia tarehe 22 hadi 27 Januari 2019 ili kumjifunza Yesu kutoka katika shule ya Bikira Maria. Vijana wanahamasishwa kushiriki katika Njia ya Msalaba, kiini cha ufunuo na huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Vijana wa kizazi kipya wanahamasishwa kukubali na kupokea mpango wa Mungu katika maisha yao kama alivyofanya Bikira Maria kwa kukubali mpango wa Mungu katika maisha yake, leo hii vizazi vyote wanamwita Mwenyeheri!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.