2017-07-08 16:26:00

DRC: Je, kweli uchaguzi utafanyika nchini humo kwa Mwaka 2017?


Utawala bora kimsingi unazingatia utawala wa sheria, kanuni sanjari na kuheshimu haki msingi za binadamu. Ni utawala unaojipambanua kwa kusimama kidete kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa inayopekenyua maisha ya wananchi wengi duniani. Uonevu ni mwiko katika nchi inayozingatia utawala bora. Mambo haya yananogeshwa na ukweli, uwazi, uwajibikaji na utekelezaji wa maamuzi yanayotolewa kwenye vikao na mikutano halali. Utawala bora unazingatia pia demokrasia, yaani utawala wa watu, hii ikiwa ni pamoja na kufanya chaguzi huru na za haki. Haya ndiyo mambo msingi ambayo familia ya Mungu nchini DRC inayatamani ili kuhakikisha kwamba, haki, amani na maridhiano vinatawala tena baada ya kipindi kirefu cha vita na kinzani za kisiasa ambazo zinakwamisha mchakato wa wananchi kujiletea maendeleo endelevu!

Askofu mkuu Marcel Utembi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC anatumaini kwamba, licha ya changamoto kubwa zilizoko kwa sasa, lakini uchaguzi mkuu utafanyika nchini DRC kama ulivyopangwa. Ni matumaini ya Maaskofu Katoliki nchini DRC kwamba, Serikali ya Rais Joseph Kabila haitabadili maamuzi kuhusu uchaguzi huu, ili kuanza mchakato wa haki, amani na maridhiano miongoni mwa wananchi wa DRC ambao wamechoshwa na vita isiyokuwa na kichwa wala miguu!

Hivi karibuni, Rais Joseph Kabila amekutana na kuzungumza na Askofu mkuu Marcel Utembi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC. Yale yaliyozungumzwa na viongozi hawa wawili yanabaki kuwa nyeti na kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki nchini DRC linaendelea kufuatilia kwa karibu zaidi mchakato mzima wa demokrasia na utawala bora nchini DRC, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba, uchaguzi mkuu unafanyika kama ulivyopangwa. Ili kuondokana na mkwamo wa kisiasa ambao umejitokeza hivi karibuni kutokana na sababu mbali mbali, Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linaitaka Serikali kutekeleza kwa dhati kabisa Mkataba wa Mtakatifu Silvester uliotiwa mkwaju hapo tarehe 31 Desemba 2016 na kuamua kwamba, DRC itapaswa kufanya uchaguzi mkuu katika kipindi cha Mwaka 2017. Mkataba huu ni msingi katika utekelezaji wa utawala wa sheria na kwamba, wale wote waliotia mkwaju katika Mkataba huu wanapaswa kuuheshimu na kuuzingatia kwa dhati kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa DRC.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.









All the contents on this site are copyrighted ©.