2017-07-07 17:28:00

Mwaka wa Padre Tanzania: Utambulisho wa Padre Mkatoliki!


Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, Miaka 100 ya Upadre Tanzania na Miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Jimbo Katoliki Musoma ni muda muafaka wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani ya Kikristo na wito wa Daraja Takatifu. Ni kipindi cha kuomba toba na msamaha kutokana na mapungufu yaliyotokeza pamoja na kuomba rehema na neema ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, katika Barua yake ya kichungaji inayoongozwa na kauli mbiu “Upendo kwa Utume” anayaangalia matukio yote haya kwa jicho la Sinodi ya kwanza ya Jimbo Katoliki la Musoma; anawaalika Mapadre kufanya tafakari ya kina kuhusu utambulisho wao kama Mapadre wa Kanisa Katoliki, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu.

JUBILEI: WASAA WA TATHMINI: Je, Mwana wa Mtu ajapo ataikuta Imani Duniani?

Adhimisho la Jubilei hizi tatu ni wasaa muafaka kwetu kufanya tathmini ya kina juu ya namna tunavyoitikia wito wa uinjilishaji katika nyakati zetu. Tukiongozwa na swali la Kristo mwenyewe “Je mwana wa mtu ajapo ataikuta imani duniani” (Lk. 18:8) nasi tunaunda maswali yetu ya kujitathmini. Katika maswali hayo tunajiuliza kwa dhati, Miaka 150 baada ya Jubilei hizi, uinjilishaji katika Jimbo letu la Musoma utakuwa na sura gani? Miaka 100 baada ya Jubilei ya Upadre, taswira ya wito wa Upadre katika Jimbo letu itakuwaje? Baada ya miaka 60 ya Jubilei yetu ya Jimbo, Jimbo letu la Musoma litakuwa na hatua ipi katika kujiongoza, kujieneza na kujitegemea?

Majibu ya maswali yetu hayo hayawezi kuja pasipo mikakati madhubuti inayosukumwa na upendo kwa utume tulionao kama wabatizwa. Msingi uliowekwa na Sinodi yetu ya Jimbo. Nawaalika tuiangalie Sinodi yetu ya Kwanza ya Jimbo kama hazina kubwa na ya msingi imara katika kufanya tathmini yetu. Kwa muda wa miaka miwili tulipokuwa tunaiadhimisha, tulifanya tathmini ya kina juu ya masuala mbalimbali ya kichungaji na kimaendeleo katika Jimbo letu. Tathmini hiyo ilifuatiwa na Sera, Maazimio na Matamko ambayo niliyaidhinisha tarehe 23 Novemba 2014. Tunapaswa kuendelea kwa bidii na kwa nguvu zaidi kutekeleza maagizo ya Sinodi yetu.

a.Vitabu vya Sinodi

Utekelezaji wa maagizo haya ya Sinodi utahitaji kwanza ujumbe wa Sinodi umfikie kila muumini katika Jimbo letu. Hivyo napenda kurejea mwaliko nilioutoa wakati tunaihitimisha Sinodi kuwa “Kitabu cha Sinodi kinachobeba Sera, Maazimio na Matamko haya kihifadhiwe na kitumiwe katika Parokia zote, Nyumba zote za Kitawa, Nyumba za Malezi, Jumuiya Ndogondogo za Kikristo, Familia na Taasisi zote za Kanisa Jimboni Musoma." Ni muhimu makundi yote tajwa ya wanafamilia ya Mungu Jimboni Musoma yajipatie kitabu hicho cha Sinodi kama mojawapo ya rejea muhimu.

b.Wakuu wa Taasisi, Idara na Ofisi Mbalimbali Jimboni

Utekelezaji wa Maazimio ya Sinodi katika ujumla wake ni jukumu la familia nzima ya Mungu Jimboni Musoma. Hata hivyo Sinodi haikuacha kukabidhi utekelezaji, uratibu na usimamizi wa baadhi ya mambo kwa Taasisi, Idara au Ofisi mahsusi. Katika mwaka huu wa Jubilei, naomba wahusika katika Taasisi, Idara na Ofisi husika watoe kipaumbele kwa utekelezaji wa mambo yaliyoainishwa kwao na Sinodi. Naiomba Sekretarieti yetu ya Sinodi ambayo sasa tunaipa majukumu ya kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Maagizo ya Sinodi ifanye nao kazi bega kwa bega na kwa ushirikiano.

c.Ziara katika Dekania

Sinodi yetu ilikuwa na mtazamo wa Kichungaji na yote tuliyoyajadili na kuyaazimia yalikuwa ni kwa lengo hilo. Kwa jinsi hii sehemu kubwa ya utekelezaji wa Maagizo yake itawagusa na kuwahitaji Maparoko na wasimamizi wa Parokia, walio wachungaji katika Parokia zetu. Kwa kuwa tayari mwaliko wangu maalumu kuhusu Sinodi ulikwishatumwa kwao,  nitapenda kupata taarifa ya namna utekelezaji wa Maagizo hayo unavyoendelea katika Parokia zetu. Taarifa hizi nitazipokea kiudekano katika mkutano maalumu nitakaofanya na mapadre wote wa Udekano husika kwa tarehe zifuatazo:

Mikutano hii ikitimiza lengo lake itachochea utekelezaji wa Maagizo ya Sinodi na itatoa mwamko mpya katika kutekeleza wajibu wetu wa uinjilishaji. Tathmini kwa Utambulisho wa Mapadre (Priestly Identity): Jubilei ya miaka 100 ya upadre katika Tanzania inatupa kwa namna ya pekee zaidi sisi mapadre wasaa wa kujitathmini. Hapa tunaliona bayana mbele yetu swali ambalo Kristo aliwauliza wanafunzi wake “watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?” (Mt. 16:13). Katika swali hii ni sisi tunasimama mbele ya wanafunzi wetu na kuwahoji “watu husema sisi mapadre ni akina nani?” Swali hili la msingi kwetu kujitathmini linagusa undani wa utambulisho wetu kama mapadre.

Katika Mausia ya Kitume Pastores Dabo Vobis, Mt. Papa Yohane Paulo II anaelezea dhana ya  Utambulisho wa Mapadre kwa maneno haya: “Mapadre ni wawakilishi wa kisakramenti wa Yesu Kristo - kiongozi na mchungaji ambao kwa mamlaka waliyopewa hutangaza neno lake na huendeleza kazi yake ya ukombozi hasa kwa njia ya sakramenti za ubatizo, Kitubio na Ekaristi wakiyatolea mapendo yao kama zawadi ya nafsi zao nzima kwa kundi walilokabidhiwa ili walikusanye na kulipeleka kwa Baba kwa njia ya Kristo katika Roho Mtakatifu.

Wengi wetu tunaifahamu simulizi inayovutia sana kumhusu Mtakatifu Maksimiliano Kolbe, Padre na Mfiadini. Katika siku ya kifo chake alipokuwa gerezani Auschwitz, Poland  alijitolea auawe badala ya  mfungwa ambaye angeacha mke na watoto. Katikati ya kilio cha mfungwa huyo ghafla Mt. Kolbe anasema “Mimi hapa najitolea kuuawa badala yake”. “Wewe ni nani?” aliuliza Askari. Mt. Kolbe alijibu bila kusita “Mimi ni Padre Mkatoliki”, akakipokea kifodini. Utambulisho alioukiri Padre mwenzetu, Mt. Maximilian Kolbe, ni utambulisho anaopaswa kuushuhudia kila Padre, kila siku ya maisha yake. “Dhana hii” kama anavyofundisha Papa Mstaafu Benedict XVI “ni ya msingi katika kutekeleza wajibu wetu wa kipadre sasa na hata baadaye”. Nawaalika mapadre kuhuisha utambulisho huu katika tathmini ya Upadre wetu mwaka huu wa Jubilei. Fikra zetu, maneno yetu, kazi zetu na maisha yetu yote kwa ujumla yawe ni ungamo la utambulisho wetu - sisi ni mapadre wakatoliki.

Ili kupyaisha utambulisho wetu huu mambo kadhaa yatafanyika mahsusi katika mwaka huu kwa ajili ya Mapadre. Sala ya kuwaombea mapadre itaanza kusaliwa kote Jimboni kila siku baada ya Misa, katika Mikutano ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo na katika Nyumba za Kitawa. Kila Padre atasali sala maalum ya kujiombea kila siku. Kwa vile dhana ya Utambulisho wa Mapadre haiwezi kutenganishwa na malezi ya wale wanaojiandaa kuingia katika huduma ya Upadre, sala ya kuombea mapadre itasaliwa sambamba na Sala ya kuombea Miito. Semina maalum yenye dhamira ya kuchochea dhana ya Utambulisho wa Mapadre itafanyika kwa mapadre wote wanaofanya utume Jimbo la Musoma.  Mafungo ya Jumla ya Mapadre kwa mwaka huu yatalenga kutafakari dhamira “Watu husema Mwana wa Adamu ni nani - Watu husema sisi Mapadre ni akina nani?” Pamoja na maadhimisho haya katika ngazi ya Jimbo, ninawaalika mapadre katika mikusanyiko ya dekania zetu kuwa na nyakati za semina na mafungo kwa dhamira hizo nilizozitaja hapo juu. Ninapenda kuhitimisha fikra zangu katika Jubilei ya Miaka 100 ya Upadre kwa kurejea utenzi wa kale kuhusu Padre, utenzi unaosadikiwa kutungwa na Mt. Norbert.

Ee Padre, wewe ni nani?

Si kwa uwezo wako, kwa maana umetwaliwa kutoka unyonge

Si kwa ajili yako, kwa maana wewe ni daraja tu la watu

Si kwako, kwa maana wewe ni wa Kanisa

Si kwa walio wako, kwa maana wewe ni mtumishi wa wote

Si wewe, kwa maana wewe ni wa Mungu

Ee Padre, wewe ni nani basi?

+Michael Msonganzila.

ASKOFU WA MUSOMA.

Imetolewa Uaskofuni, Nyamiongo tarehe 10 Mei 2017

 







All the contents on this site are copyrighted ©.