2017-07-06 16:14:00

Mwilisheni fadhila ya unyenyekevu katika huduma kwa watu wa Mungu!


Leo tuitafakari fadhila ya unyenyekevu kama nyenzo muhimu ya kuustawisha ufalme wa Mungu hapa duniani. Katekisimu ya Kanisa Katolikia inatufundisha hivi: “Bwana analalamikia matajiri kwa sababu wanapata faraja zao katika wingi wa mali zao. Wenye kiburi wanatafuta uwezo za kidunia wakati maskini wa roho anatafuta ufalme wa mbinguni. Kujiachia kwa maongozi ya Bwana wa mbinguni kunatufanya huru na kutuondolea wasiwasi kuhusu kesho. Kumtumainia Mungu ni matayarisho ya hali ya kubarikiwa ya maskini.” (KKK 2547). Mistari hii michache ya Mafundisho ya Kanisa inautofautisha unyenyekevu na kiburi; inatufafanulia jinsi ambavyo mwanadamu katika kiburi chake anavyoutupilia mbali ufalme wa Mungu lakini katika unyenyekevu unaojieleza katika umaskini wa roho anakuwa ameunganika na Mungu.

Katika Injili, Kristo anatumia taswira ya mtoto mchanga kuelezea fadhila ya unyenyekevu. Kristo anasema: “Nakushukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafumbulia watoto wachanga”. Haiba ya mtoto mchanga ni ya kupokea. Daima yupo tayari kupokea Elimu na maelekezo mapya anayopatiwa kwa ajili ya kukomaa kimwili, kiakili na kiroho. Mtoto mchanga anatuonesha usikivu na utii. Hali ya kuwa mtoto mchanga ni hali ya kujiona u mtupu na utegemezi. Mtoto mchanga anajisikia huru na salama kwa mzazi wake na anajitegemeza mzima mzima. Kuwa na hali ya mtoto mchanga mbele ya Mwenyezi Mungu ni kujikabidhi kwake na kujitegemeza katika yote. Ni ile hali ya kujiona kuwa bila Yeye hauwezi kufanya chochote. Katika hali hii ndipo tunaweza kuyapokea maongozi yake na hivyo kuustawisha ufalme wake hapa duniani.

Kristo anaitukuza hali hiyo tofauti na kuwa “wenye hekima na akili”. Hii haimaanishi Kristo kudharau hali ya kuwa na hekima na akili. Yeye anaitofautisha hekima na akili ya watu wa ulimwengu ambayo inamuondoa Mungu. Watu aliokuwa anawahubiria walijikinai kuwa wakamilifu na wenye kujua vyote. Hekima na akili za kidunia hazitoi fursa kwa kuweka utegemezi kwa Mungu. Kiburi cha mwanadamu cha kutaka kuwa na hekima na akili nyingi kilimtenga na Mwenyezi Mungu na ndipo ikawa mwanzo wa dhambi ya ulimwengu. Hekima na akili ni tunu njema kwa mwanadamu katika kuutambua ukweli wa Mungu na kuustawisha. Mapaji haya ni tunu kutoka kwa Mungu mwenyewe. Mapaji haya hayapaswi kututenga na Mungu bali yanatuelekeza kuwa wanyenyekevu na kumsikiliza Yeye aliye asili ya Elimu yote.

Ujio wa Kristo hapa duniani, kama unavyotabiriwa na Nabii Zekaria ni katika hali ya unyenyekevu. “Tazama mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu amepanda punda, naam, mwana-punda, mtoto wa punda”. Ni mfalme anayekuja si kadiri ya taratibu na mazoea ya jamii bali katika hali ya unyenyekevu, katika hali duni. Pengine ilionekana kuwa ni kichekesho. Hali kama hii huonekana katika jamii yetu ya leo ambapo wengi husita kufuata njia ya upole na unyenyekevu kufikia mafanikio. Waswahili wanasema “pole pole ndiyo mwendo” na “haraka haraka haina baraka”. Lakini wanadamu wengi leo hii hawana uvumilivu  na hivyo mambo ya chapuchapu hufagiliwa sana. Lazima kupata jina haraka hata kama kwa njia za uovu au hata kama kwa kuutimbilia mbali ukweli.

Tukitembea katika ukweli hakuna sababu ya kufanya mbwembwe na matambo ya kidunia ili kujitambulisha mbele za watu. Fadhila ya unyenyekevu inatupeleka katika ukweli. Mbegu isipokuwa tayari kufa na kuoza haiwezi kuzaa matunda. Tukiingalia mbegu ya mbuyu tunaweza kuidharau ila katika ukimya huoza na kuzaa mti mkubwa. Yeye anayejenga katika ukimya na unyenyekevu hukubali makosa na kurekebisha, hujifunza katika mambo ya wengine na huthamini vipawa vya wengine. Kujenga katika unyenyekevu hudumisha umoja na mshikamano. Kinyume chake wenye kelele na tambo huwa kama moto wa nyikani ambao huwaka na kuenea kwa haraka lakini huishia. Tukumbuke kwamba “ngoma inayovuma sana ndiyo inayopasuka”.

Jamii tuishiyo leo hii inapima mafanikio na ukuu katika mambo yanayoshikika na kuonekana. Lakini tujiulize swali: ni nini yaliyo mafanikio ya ukweli? Kipimo chake ni nini? Dunia yetu mamboleo inayaona mafanikio bila uwepo wa Mungu lakini katika ukweli mafanikio yoyote ambayo hayaujengi ufalme wa Mungu huishia kuwa ni utupu na yasiyodumu. Kazi yote ya uumbaji ni kazi ya Mungu na yenye kumfunua Mungu. Huwezi kutenganisha chochote hapa duniani na Mwenyezi Mungu. Hivyo mafanikio yote yanapaswa kushuhudia matunda ya ufalme wake, yaani haki, usawa, mshikamano, udugu, msamaha na tunu nyinginezo nyingi. Haimfaidii kitu mtu kuwa na uwezo au mamlaka ambayo hayamuunganishi na mwenzake na hivyo kutodhihirisha tunu na ufalme wa mbinguni.

Leo hii wengi hushindwa kuhudumia kwa sababu ya haya au kuona si kutenda kadiri ya hadhi zao. Aliyetunukiwa Shahada ya Udaktari anaona kudharaulika kuwekwa katika jukwaa la kuwafundisha watoto wa shule ya msingi. Yeye ni wa matawi na juu na hivyo aonekane katika vyuo vikuu na vinavyorandana navyo. Unaweza vipi kuweza kufundisha mambo magumu kama huwezi kufundisha yale ya chini na ya kawaida kama si njia ya kujitafutia umaarufu tu kwa kukaa katika vyuo na Taasisi zenye majina? Daktari bingwa haweza kutibu katika zahanati ya kijiji bali katika hospitali kubwa na yenye jina. Hivi Malaria anayoumwa mtoto wa kule Mpitimbi Songea ina tofauti na Malaria anayougua mtoto wa Masaki? Hakuna lolote ni kukosa unyenyekevu na kutafuta jina tu. Yote haya yanatoa changamoto na kujiuliza namna tuipokeavyo huduma yoyote tunayokirimiwa. Je, ni kwa ajili ya kulikuza jina langu au kwa ajili ya kuustawisha ufalme wa mbinguni?

Karama na vipawa vyote tunapewa na Mungu. Sisi tunakuwa wajumbe wake kwa ajili ya kufikisha upendo wa Mungu kwa wengine. Tulitafakari wakati wa sherehe ya Pentekoste kuwa karama zote hizo katika utofauti wake ni utendaji wa Roho Mtakatifu kwa sababu hii ni kazi ya Mungu. Tunapozigeuza kuwa zetu na matunda ya juhudi zetu hupoteza lengo lake.Tabibu anayepaswa kutibu watu ataingia katika kishawishi cha kuiuza huduma yake na kuwa chanzo cha kuwanyonya wengine kwa njia ya kutoa huduma ghali sana au kuuza dawa kwa bei ghali kwa nia ya kujinufaisha binafsi katika kipato. Hakuna utayari wa kujimithilisha na Kristo kwa kujivika upole na unyenyekevu ili wote waonje upendo wa Mungu kwa njia ya huduma yako.

“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wanguni mwepesi”. Hii ndiyo njia tunayowekewa mbele yetu kuustawisha ufalme wa mbinguni. Njia hii ni Kristo ambaye ni mfalme anayeutawadha ufalme wake si kwa mabavu bali kwa upole, si kwa makelele na tambo bali kwa ukimya na si kwa kujiinua bali katika hali ya chini akiachilia yote kujidhihirisha yenyewe. Hii ni kwa sababu ufalme wake ni wa ukweli na ukweli hudumu daima. Mtume Paulo anatukumbusha kwamba Roho wa Kristo yu ndani mwetu hivyo tusiishi kwa kufuata matendo ya mwili bali matendo ya Roho.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.