2017-07-06 14:58:00

Maandalizi ya Kumbu kumbu ya Miaka 30 ya Roho ya Assisi yapamba moto!


Mkutano wa kimataifa unaoandaliwa kila mwaka na Jumuiya ya Mt. Egidio kwa ajili ya majadiliano ya amani kati ya dini mbali mbali na dunia ya utamaduni, yajulikanayo kama “Roho ya Assisi”, utafanyika Ujerumani Septemba 10 – 12, 2017. Mkutano huu ulianzishwa baada ya siku ya sala kwa ajili ya amani iliyoandaliwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II mwaka 1986. Katika maandalizi ya mkutano huo siku ya Ijumaa tarehe 29 Juni 2017, ambapo majimbo ya Osnabrück na Münster yatakuwa wenyeji, imetolewa taarifa kwamba Chancellor Angela Merkel atashiriki pia katika mkutano huo mwezi Septemba.

Cesare Zucconi wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio anakumbusha hali ya vita, ugaidi na kinzani katika jamii nyingi duniani, iwe mwaliko kwa watu wa dini mbali mbali kuungana katika kutafuta kutokomeza ghasia kwa mtazamo wa pamoja na wa kiekumene. Uwezekano wa kubadili dunia upo na ni mkubwa, watu wasikate tamaa waendelee kushirkiana. Katika mkutano huo, kutakuwepo pia watu kadhaa kutoka nchi zenye vita watakaotoa ushuhuda. Askofu Franz Joseph Bode, anawaalika washiriki kusikiliza ushuhuda wa watu hao, sio kama hadithi ya kufikirika, bali kuwa mwaliko kushiriki kikamilifu kutafuta amani. Itakumbukwa katika mkutano wa mwaka uliopita, 2016 huko Assisi nchini Italia, ambapo yalikuwa maadhimisho ya miaka 30 ya Siku hiyo ya Sala kuombea amani, Baba Mtakatifu Francisko alishiriki na akasisitiza kusema, hakuna vita takatifu, amani ndio takatifu.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.